Thursday, November 14

‘MKAPA’ NA WENZAKE PEMBA WALAZWA RUMANDE

NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAHKAMA kuu Zanzibar kisiwani Pemba, chini ya Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, imewapeleka rumande watumuhimwa wanne wanaokabiliwa na tuhuma za kuua kwa makusudi, akiwemo Ali Mussa Omar ‘Mkapa’ mkaazi wa Wawi wilaya ya Chake chake Pemba.

Watuhumiwa wengine walioanza maisha mapya ya rumande ni mtuhumiwa Yassir Mohamed Juma miaka 23, Anuwari Mussa Omar miaka 30 pamoja na mtuhumiwa Yassir Mussa Omar ‘Makababu’ miaka 29, wote wakaazi wa shehia ya Wawi, wilaya ya Chake chake Pemba.

Awali watuhumiwa hao waliwasili mahakamani hapo, kwa mara ya kwanza, kwa ajili ya kusomewa tuhma zinazowakabili za kumuua kwa maksudi Said Seif Kombo.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashataka Seif Mohamed Khamis akiambatana na mwenzake Mussa Khamis Ali kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaia kufanya mauwaji hayo kwa maksudi.

Ilidai kuwa, watuhumiwa wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo Oktoba 16, mwaka huu, baina ya saa 7:00 mchana na saa 11:00 jioni, katika eneo la Machaomane wilaya ya Chake chake Pemba.

Ilidaiwa na Mwendesha mashtaka huyo kuwa, kufanya hivyo ni kosa kinyume na vifungu vya 189 na 190 vya sheria nambari 6 ya mwaka 2028 sheria ya Zanzibar, iliyopitishwa na baraza la Wawakilishi.

Mara baada ya mwendesha mashtaka huyo kumaliza kazi ya kuwasomea maelezo ya tuhma zinazowakabili, Jaji Ibrahimu wa mahakama kuu Zanzibar, aliwauliza wathumiwa hao, ikiwa wameelewa kosa lao.

‘’Mtuhumiwa nambari moja Anuwari Mussa Omar hadi mtuhumiwa nambari nne Yassir Mohamed Juma, jee mumemsikia Mwendesha mashtaka na mumemuelewa,’’aliwahoji Jaji Ibrahim.

Kwa kila mmoja na kwa wakati wake, walimueleza Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim kuwa, wameyasikia na kuyafahamu vyema maelezo ya kosa lao, ingawa walipoulizwa kuhusu kukubali, walikana kutenda kosa hilo.

‘’Mheshimiwa ni kweli tumeyafahamu maelezo ya kosa letu, lakini tunaiomba mahakama yako tukufu, itupe dhamana ya juu tuhma tunazokabiliana nazo,’’aliomba mtuhumiwa nambari mbili Yassir Mussa Omar ‘Makababu’.

Ombi ambalo Jaji huyo wa mahkama kuu, alilipinga akisema kifungu cha 151 cha sheria Mwenendo wa makosa ya Jinai, nambari 7 ya mwaka 2018, inapinga kutoa dhamana kwa kosa linalowakabili.

‘’Sheria inapinga vikali makosa ya ubakaji, kuingilia maharimu, kubaka kwa kundi, uhaini, wizi wa kutumia silaha, kupatikana na dawa za kulevya kiwango kikubwa na kuua kwa maksudi, kutoa dhamana,’’alifafanua Jaji huyo.

Hata hivyo watuhumiwa hao, waliieleza mahakama hiyo kuu kuwa, wanaewakili katika kesi yao hiyo, ingawa kwa jana hakuweza kufika mahakamani, kutokana na sababu mbali mbali.

Jaji Ibrahim, kisha aliighairisha kesi hiyo, hadi Novemba 30, mwaka huu na kuutaka upande wa mashtaka, kuwasilisha mambo mawili siku hiyo, ikiwemo ushahidi wa maadishi na kufanyike kwa usikilizsaji wa awali ‘PH’ kabla ya kuanza kwa kesi ya msingi.

Wakati huo huo, Jaji Ibrahim Mzee Ibrahim, aliwaambia watuhumiwa hao kuwa, kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, kama watatiwa hatiani, adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.

                  Mwisho