NA ZUHURA JUMA, PEMBA
Mpaka hivi karibuni baadhi ya watoto wa skuli ya Kiuyu Minungwini Pemba, walikuwa wanaposoma mara nyingi wanaangalia hewani, badala ya kufuatilia anachoeleza mwalimu.
Hii ilitokana na kuangalia mawingu kama itanyesha mvua au kunyewa na kunguru kwa vile madarasa yao yalikuwa chini ya miti.
Lakini hatimaye watoto hawa sasa wanafurahia masomo kama wenzao katika skuli nyengine za jirani na mbali ya hapo.
Hayo yote yametokana na uongozi mzuri, mahiri na wenye kuonyesha jitihada za kuwapunguzia matatizo wananchi, kwa mwanama shupavu Nasra Salum Mohamed ambae ni diwani wa Wadi ya Kiuyu.
Ni mmoja wa viongozi wanawake, anayepambana kuwapatia haki zao wananchi waliomo kwenye wadi yake.
Tangu kuchaguliwa kuwa diwani ameshughulikia kero mbali mbali za watu wa eneo hilo, ikiwa ni pamoja na hili la skuli.
Mafanikio yake yanatokana na kushirikiana na wananchi kwa kuzifikisha kero katika sehemu husika, ili kupatiwa ufumbuzi huku akiwajumuisha wananchi wake kuchangia kupata ufumbuzi na sio kubaki wanalalamika tu.
Moja ya kero alizotatua kiongozi huyo, ni ya ujenzi wa madarasa katika skuli mbali mbali kwenye jimbo hilo, ili kuwajengea mazingira bora ya kupata elimu kwa watoto.
Nasra alifanya juhudi mbali mbali kuhakikisha yanapatikana madarasa kwenye skuli zenye upungufu kwa ajili watoto kunapata haki yao ya kusoma bila usumbufu.
Hapo kabla, hasa wakati wa mvua za masika, mvua ikiteremka tu basi huwa ndio mwisho wa masomo kwa siku hiyo.
Na hata vumbi wakati upepo mkali lilileta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi hao.
Katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo, diwani huyo amejenga tabia ya kukutana mara kwa mara na wananchi ili kuzungumzia kero zinazowakabili na kushauriana, ni njia gani inayofaa kumaliza tatizo.
Anasema kadhia iliokuwepo skuli ya Minungwini ya wanafunzi kusoma chini ya mti ambayo iliwakwaza wazee, walimu na wanafunzi, ilimuumiza sana na kuona dawa mujara ni ujenzi wa madarasa mapya.
“Skuli hii ipo karibu na kwangu, muda wote naiona na kunitia unyonge, ndio maana nikaamua kufikisha kero hii sehemu zinazohusika ili ipatiwe ufumbuzi,’’ anasema huku akitabasamu kuonyesha furaha yake kwa mafanikio hayo.
Miongoni mwa juhudi zake zilizozaa matunda ni kuzungumzia kadhia hio katika kila kikao na hatimae likajengwa banda la vyumba vinne, ambapo kimoja kilianza ujenzi wake kwa nguvu za wananchi.
“Jengo hili limesaidia sana kwa sababu wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri na zaidi kwa vile palijengwa pia na choo, kwani shimo lililotumika hapo mwanzo lilijaa na kuzuwiwa kutumika,’’ alieleza.
Diwani huyo pia alishajihisha ujenzi wa vyumba vinne vya skuli ya maandazi Kangagani na kuezeka kituo cha ‘tusome tujifunze’ (tutu) kilichopo Mjinikiuyu.
“Wanapoleta changamoto zao, tunakaa pamoja na kutafuta njia ya kuzitatua, tunaandika barua kuzipeleka sehemu husika na baadae nafuatilia mpaka nihakikishe ufumbuzi umepatikana,’’ anafahamisha.
Nasra siku zote anashirikiana na viongozi wa jimbo na Serikali katika kutatua changamoto mbali mbali za wananchi na kufurahia kwa kuungwa mkono na viongozi pamoja na wananchi.
Mwana mama huyo alianza harakati za kugombea uongozi baada ya Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA Zanzibar) kuanzisha mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi uitwao WEZA na yeye akiwa Katibu wa kikundi.
Anasema, walijengewa uwezo namna ya kujiamini na kuwa jasiri ambapo mafunzo hayo yalimsaidia kuwa na uwezo wa kusimama popote bila ya woga kuelezea jambo.
“Kwa kujiamini nilijiingiza jimboni kugombea nafasi ya udiwani kupitia chama cha Mapinduzi CCM na nikashinda, sasa ninawatumikia wananchi wa wadi yangu na hata wadi iliopo jirani,” anaeleza.
Diwani huyo anafafanua changamoto zinazowakumba wanawake na kushindwa kugombea nafasi za uongozi kuwa ni umasikini unaopelekea kushindwa hata na usafiri wa kufanya kampeni.
‘’Unapotaka kugombea ni lazima utembee maeneo tofauti na watu watakaokusaidia kukutangaza, lakini wakati mwengine tunashindwa kwani vijiji ni vingi na hatuna uwezo,’’ anaongeza
Vile vile, wapo wanawake ambao waume zao au familia zao zinapewa maneno ya watu wa mtaani ili wasijiingize katika uongozi kwa kile wanachodai kuwa, wataharibika na kuwatia aibu, jambo ambalo sio la kweli.
Hivi sasa ni diwani wa Wadi ya Kiuyu kwa kipindi cha pili na ataendelea kuwatumikia wananchi kwa kupigania haki zao.
Ahmada Ali Omar ambae ni mwalimu Mkuu wa skuli ya msingi Minungwini anasema, panapokuwepo viongozi wa Serikali, wizara, madiwani na masheha wanaojali na kuwa tayari kuwatumikia watu, ndio hupatikana maendeleo.
Anasema, anafurahishwa kuona wanaye diwani ambae ana kawaida ya kufika skulini hapo kuangalia maendeleo ya wanafunzi, shida na kero zinazowakwaza walimu na wanafunzi.
‘’Ilikuwa hatuna madarasa ya kutosha kwa wanafunzi na ndio maana baadhi ya wanafunzi walikaa chini ya miti, lakini diwani huyu alijitahidi kutupigania na tukajengewa banda la vyumba vine, moja likianzwa na wananchi,’’ anasimulia
Banda hilo sasa linawanufaisha wanafunzi 473 ambao wanaingia kwa mikondo miwili, asubuhi na jioni.
Mwalimu huyo anasema kwa mtazamo wake, wanawake wanapoingia kwenye vyombo vya maamuzi huwa ni wakombozi kwa sababu huwa na huruma, ni wapambanaji na wafuatiliaji kero za wananchi.
WANANCHI
Fatma Jafar Faki anasema, diwani huyo anawasaidia kutatua changamoto za kijami na kushirikiana nao bega kwa bega.
Mkaazi mwengine wa Kiuyu, Asha Omar Rashid anasema ukiachana na changamoto ya madarasa diwani wao pia ametatua kero ya umeme, maji na barabara katika jimbo lao.
ASASI ZA KIRAIA
Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema, wana mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.
Kwa sasa wanawajengea uwezo zaidi ili wajielewe, wajiamini na wajue namna ya kutengeneza timu ya kampeni katika kufanikisha azma yao.
Kwa Pemba, TAMWA imeshawapatia mafunzo wanawake 70 na wamewaunganisha na wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbali.
Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa PEGAO anaelea, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi za uongozi, wanaonekana juhudi kubwa wanazozifanya katika kutekeleza majukumu yao.
‘’Tulipofanya utafiti kwenye vyama, walituambia kwamba wanapochaguliwa viongozi wanawake hata chama kinaimarika zaidi kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa,’’, anasema.
Anaviomba vyama vya siasa kuona uwezo wa akianamama katika nafasi hizo, kwani wanajitahidi sana kuiunganisha jamii na kutatua changamoto zilizopo.
‘’Wanawake wapewe fursa ya kushiriki katika uongozi, ili maendeleo ya haraka yapatikane, kwani wao hawapendi rushwa bali wanasimamia utekelezaji kwanza.
Kutokana na elimu inayotolewa kila siku kupitia asasi za kiraia ikiwemo TAMWA ya kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu wa mwanamke kuwa kiongozi, sasa wanaingia kwa wingi kuchukua fomu za kugombea.
Na ndio maana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 jumla ya wanawake 74 waligombea udiwani, ambapo wanawake 25 walishinda, huku wanaume 276 waligombea na kushinda 85.
Ambapo mwaka 2015 walioshinda ni madiwani 85 kati ya waliogombea 173.
Kwa kutambua umuhimu wa mwanamke, sera na sheria mbali mbali za Zanzibar zimeeleza kuhusu haki ya wanawake kushiriki katika demokrasia na uongozi.
Kifungu cha 21 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 64 kimeeleza kwamba, kila mzanzibari anayo haki na uhuru wa kushiriki kikamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomuhusu mwanamke na taifa lake.
MWISHO.