Friday, November 15

Bank ya NBC imesaini hati ya makubaliano na taasisi za SMZ Kuongeza Ukusanyaji Wa Mapato Zanzibar

Na Mukrim Mohamed.-  UNGUJA.
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imesaini hati ya Makubaliano (MOU) na taasisi sita za Serikali ya Mapinduzi Zanzbar (SMZ) yanayotoa fursa kwa benki hiyo kutumika kukusanya malipo mbalimbali ya Serikali kupitia mtandao na mfumo na wa kidijitali wa benki hiyo.
Makubaliano hayo yanayohusisha Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mfuko wa Hifadhi Jamii Zanzibar (ZSSF), Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS), Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Idara ya Ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi- Zanzibar (ZPPP) na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yanatajwa kuwa mbali na kurahisiha huduma ya malipo kwa wananchi pia yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuzuia upotevu wa mapato ya serikali.
Hafla ya utiaji Saini makubaliano hayo imefanyika Jana November 21. 2023 katika hotel ya Golden Tulip Airport Zanzibar, ikiongozwa na Waziri Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Saada Mkuya huku ikihusisha uwepo wa viongozi waandamizi wa mashirika hayo pamoja na maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi.
Akizungumzia kwenye hafla hiyo,  Waziri Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Saada Mkuya pamoja na kuwapongeza wadau hao kwa ushirikiano huo alisema hatua hiyo inakwenda sambamba na adhima ya serikali ya SMZ kuelekea kukamilisha mfumo wake wa Serikali mtandao.
“Hatua hii ya leo kwa kiasi kikubwa inaunga mkono jitihada za serikali kuitumia vizuri  teknolojia na mifumo ya kielektroniki katika shughuli zake hususani katika ukusanyaji wa mapato. Hatua hii inatusaidia katika kurahisisha huduma za malipo mbalimbali kwa wananchi, kuongeza kasi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na zaidi pia kuzia mianya ya upotevu wa mapato ya serikali…tunawapongeza sana NBC na wadau wote kwa hatua hii,’’ alipongeza.
Kwa mujibu wa Waziri Sada Mkuya kupitia makubaliano hayo yanayohusisha taasisi kubwa za serikali ya SMZ,  wananchi watanufaika moja kwa moja kupitia faida mbali mbali za kiuchumi na kijamii huku pia akibainisha kuwa mfumo utasaidia kuchochea suala zima la utawala bora kupitia uwazi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi alisema ushirikiano huo ni muendelezo wa makubaliano ya awali ambayo kwa kiasi kikubwa yanaonyesha dhamira thabiti ya Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar katika kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato yake kupitia mfumo wa  Kielektroniki  yaani (GEPG) au ZanMalipo.
“Kupitia makubaliano haya wananchi sasa wataweza kutumia mtandao wa Benki ya NBC kufanya malipo ya Serikali na ankara mbalimbali kupitia mtandao wa Benki ya NBC.’’
‘’Malipo hayo yanaweza kufanyika kupitia matawi yetu mawili yaliyopo hapa Zanzibar na pia kupitia zaidi ya mawakala wetu 207 waliopo kila kona ya Unguja na Pemba na pia kupitia huduma zetu za kidijitali yaani huduma za benki kwa njia simu (NBC Kiganjani ) na huduma zetu kupitia mtandao.’’ Alieleza
Wakijadili kuhusu ushirikiano huo Kamishna Mkuu wa ZRA Yusuph Mwenda, Mkurugenzi Mkuu  wa ZBS Yusuph Majid Nassor, Kamishna wa ZPPP  Dkt. Bill Kiwia na Meneja wa Fedha ZECO Riziki Faqih walitaja ushirikiano huo kama nyezo muhimu sio tu katika kukusanya mapato na kuongeza urahisi wa kusimamia mchakato wa kifedha bali pia ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi Zanzibar.
“Kupitia mfumo huu ni wazi kwamba tunakwenda kushuhudia ongezeko kubwa la mapato yetu kwa kuwa utasaidia sana kwanza kuondoa usumbufu uliokuwa unawakabili wananchi wengi kutembelea ofisi mbalimbali ili tu kufanya malipo mbalimbali ya serikali ikiwemo kodi na tozo za mamlaka za serikali na pia itachochea kasi ya malipo hayo kwa kuwa wananchi watatimiza wajibu huo kwa wingi wao kwa kuzingatia kwamba benki ya NBC ina mifumo rahisi nay a kisasa zaidi,’’ alisema.
MWISHO.