Thursday, November 14

Wasaidizi wa sheria wafutiwa ada Zanzibar-Waziri Haroun

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman, ametangaza rasmin kufuta ada ya usajili kwa wasaidizi wa sheria.

Hayo aliyasema wakati akifunga jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa kisheria huko katika ukumbi wa chuo cha utalii Maruhubi Unguja.

Alisema ameamua kuondosha ada hiyo, ili kuwaondoshea gharama katika utendaji wao wa kuwasaidia wananchi katika changamoto zinazowakabili.

Haroun alisema ufutaji wa ada hiyo, kwa sasa unawahusu watoa msaada wa kisheria wanaojisajili mmoja mmoja wakiwemo wasaidizi wa sheria, mawakili, mavakili na wanasheria ambao hujisajili kama watoa msaada wa kisheria.

“Nafahamu kuwa wasaidizi wa sheria mnalipa ada ya shilingi 20,000 kuanzia sasa natangaza rasmin kuifuta ada hiyo,”alisema.

Alieleza kwamba hapo,V baadae wizara itaangalia uwezekano wa kuondosha ada hiyo na hata kwa taasisi ambazo zimejikita kutoa msaada wa kisheria.

Aidha Haroun alisema kazi inayofanywa na watoa msaada wa kisheria, ni kubwa na inathaminiwa sana na jamii pamoja na viongozi wakuu kutokana na juhudi wanazozichukua.

Kutokana na hayo, alisema bado wanahitajia kujiimarisha zaidi na kupata uzoefu na elimu, ili kupata tija ambayo itafanikisha kuzidi kutoa msaada kwa jamii husika.

Hata hivyo Waziri Haroun, alizishauri taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa sheria ikiwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu, skuli ya sheria na Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria kushikamana kwa lengo la kuwaimarisha watendaji hao.

Hivyo alizitaka taasisi hizo kuandaa kikao cha pamoja, ambacho kitasaidia kufika mahali watendaji hao waweze kujua kwamba wapo katika sehemu na viongozi wao wanawaangalia.

Alisema ana azma ya kuangalia zaidi maslahi ya watoa msaada wa kisheria, ili mambo yao yawe mazuri zaidi na kufanikisha utendaji wao wa kazi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais,Katiba Sheria,Utumishi na Utawala Bora Omar Haji Gora, alisema kufanyika kwa jukwaa hilo kunasaidia wahusika kuimarika katika kutekeleza wajibu wao.

Alisema katika kufikia malengo wamekua wakishirikiana na sekta nyengine, katika kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, Hanifa Ramadhan Said alisema katika jukwaa hilo la tatu washiriki waliondoka na maazimio tisa ambayo yatakua chachu katika kuleta maendeleo.

Aliyataja baadhi ya maazimio kua ni kuhakikisha jukwaa lijalo linawashirikisha washiriki kutoka nje ya Tanzania, wahusika wa sekta ya sheria kuunda kikosi kazi na kufanya ushawishi katika uidhinishaji wa bajeti na uingizaji wa fedha ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu.

Azimio jengine ni Wizara inayohusika na msaada wa kisheria kusimamia uandaaji na utekelezaji wa mpango kazi wa pamoja, vyama vya wanasheria na mawakili wakishirikiana na wahusika wa msaada wa kisheria watawahamasisha mawakili katika uwakilishi mahakamani.

Jengine Skuli ya sheria Zanzibar iweke ulazima kwa wanafunzi wanaosomea uwakili kuvutumia vituo vya msaada wa kisheria kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo, wizara husika ianzishe kanzidata ya kitaifa na mfumo jumuishi wa kidigitali wa ukusanyaji taarifa za msaada wa kisheria kwa kushirikiana na wahusika.

MWISHO