NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.
Wadau katika mapambano dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wametakiwa kuongeza juhudi katika kuvifichua vitendo hivyo ili viweze kuchukuliwa hatua na kukomeshwa kabisa ndani ya jamii.
Wito huo umetolea na Bibi Jeanne Clark kutoka Ubalozi wa Marekani wakati alipokuwa akizungumza na wadau hao ikiwa ni pamoja na wanasheria kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashkata , Maafisa wa Jinsia, wanaharakati kutoka Jumuiya ya Waandishi wa habari Tanzania Tamwa pamoja na wanafunzi kutoka Skuli za Madungu na Chuo cha Mwalim nyerere na Utumishi wa Umma Kisiwani Pemba huko katika Ukumbi wa maktaba ya American Conner Chake Chake ikiwa ni miongoni mwa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Amesema Udhalilishaji una maana pana hivyo ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake na popote alipo kuhakikisha anapinga aina zote za vitendo vya udhalilishaji ili jamii iweze kubaki salama.
Kwa upande wao wadau hao wamesema licha ya kwamba juhudi mbali mbali zimekuwa zikichukuliwa katika kupambana na vitendo hivyo bado elimu zaidi inahitajika kwa jamii ili iweze kufahamu athari ya vitendo hivyo kijamii, kisiasa na kiutamaduni huku wakivitaka vyombo vya sheria kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao.
Wamesema Vitendo vya Udhalilishaji vimekuwa vikifanyika kila sehemu ndani ya jamii ikiwa ni ndani ya familia, maskulini, kwenye nyumba za ibada na hata kwenye sehemu za kazi hivyo ni vyema kuzitumia siku 16 kwa kujadili na kutafakari namna ya kuongeza juhudi katika mapambano hao.
Siku 16 za kupinga ukatili na udhalilishaji zimekuwa zikiadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 November hadi tarhe 10 Disemba ya kila mwaka ulimwenguni kote.
MWISHO.