Saturday, December 28

22 wameshafanyiwa upasuaji   na kuondolewa mtoto wa jicho katika kambi maalum  Hospitali ya Wete Pemba.

 NA KHADIJA KOMBO – PEMBA.

Wananchi Kisiwani Pemba, wametakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao ikiwemo afya ya macho ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Afya ya Macho  kutoka Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Fatma Omar Juma alipokuwa akizungumza na wagonjwa wa macho ambao tayari wameshafanyiwa upasuaji   na kuondolewa mtoto wa jicho huko katika kambi maalum ya matibabu hayo katika Hospitali ya Wete Pemba.

Amesema hivi sasa kuna maradhi mengi yanayoweza kujitokeza kutokana na sababu mbali mbali hivyo ni vyema wanajamii kuchukua tahadhari ya kupima afya zao mara kwa mara ili waweze kupata tiba mapema iwapo watagundulika na maradhi  na kuondoa kabisa magonjwa hayo.

Pia Dr. Fatma amewataka wagonjwa hao kufuata miko na maelekezo waliyopewa na Daktati ili kunusuru matizo zaidi yanayoweza kuwapata.

Kwa upande wao wagonjwa hao  wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya afya kwa kuandaa utaratibu wa kuweka kambi maalum ya matibabu ya macho kila baada ya muda ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.

Kambi hiyo inaendelea na matibabu ya mtoto wa jicho  katika hospitali ya Wete ambapo inatarajia kuwafanyia matibabu wananchi zaidi ya mia moja na tayari wagonjwa 22 wamesha patiwa matibabu.

 

 

MWISHO.