Sunday, November 24

Wizara ya Habari yazindua shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kufanya usafi Wilaya ya Mkoani.

Na Maryam Talib – Pemba

Ofisa Mdhamin Wizara Habari Utamaduni na Michezo Mfamau Lali Mfamau katika kuelekea kuadhimisha miaka (60) ya Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar aliwataka wananchi wa maeneo tofauti kujenga Utamaduni wa kusafisha katika maeneo yao yaliyowazunguka kwa lengo la kuepusha kujitokeza kwa maradhi hususani ya miripuko ikiwemo kipindupindu.

Mfamau aliyaeleza hayo alipokuwa akifanya usafi akiwa na watendaji wenzake wa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba pamoja na wanachi wa Wilaya ya Mkoani huko wilayani kwao.

Alisema kuwa ijengwe tabia hiyo ya kufanya usafi na sio kusubiri kila kipindi Fulani au Serikali itangaze tarehe ya kufanya usafi wananchi wenye wanapaswa kujenga utamaduni huo kwa kujipangia muda wa kulitekeleza zoezi hilo.

“Nawaombeni wananchi wenzangu zoezi hili iwe ni utamaduni wetu kwa faida afya zetu”alisema Mdhamini huyo.

Afisa Utumishi Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Khamis Masoud Khamis alisema kwa upande wake siku ya leo imekuwa ni ya faraja kwa kufanya usafi katika maeneo ya Mkoani ikiwa ni shamra shamra ya kutimiza miaka (60) ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

“Tumefarajika sana sisi wafanyakazi wa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni namichezo kwa kuona wenzetu wa Mkoani wamekuwa na mwitikio mkubwa kwenye zoezi hili la usafi ambalo ni moja wapo ya hekeheke za miaka (60) ya mapinduzi”alisema mtumishi huyo.

Kijana mwenye umri wa miaka (12)Mkaazi wa Wilaya ya Mkoani Mohamed akiwa katika zoezi la usafi alisema amefurahishwa sana na ujio wa watu wa Wizara ya Habari kwenda kutia nguvu katika Wilaya yao kwenye suala la usafi jambo ambalo ni muhimu hasahasa kwa kulinda afya zao.

“Naomba zoezi hili la usafi tuliendeleze hata kama haujafika muda wa kusherehekea Mapinduzi”alisema mtoto huyo.

 

MWISHO.