Sunday, November 24

Profesa Mnyaa azindua Ofisi za Kikosi cha KMKM na Chuo Cha Mafunzo Wete.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WAZIRI wa Uchukuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, amesema utekelezaji wa mradi wa Ofisi Kikosi cha KMKM na Chuo Cha Mafunzo Wete, ni jambo la faraja katika suala zima la kuimarisha ulinzi na usalama, katika ukanda huu kwa sababu utawezesha kupunguza biashara  haramu za magendo mbali mbali.

Alisema ujenzi huo utasaidia kuzuia uharibifu wa mazingira ya bahari, pamoja na kuzuia uhamiaji haramu katika eneo hili, jambo ambalo litasaidia kuimarisha usalama wa Taifa na uchumi kwa ujumla.

Hayo yameelezwa katika hotuba yake iliyosomwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Lela Mohamed Mussa, mara baada ya kufungua Hanga, Ofisi za Utawala za KMKM na Ofisi ya Kamanda Mkuu zoni ya Pemba Chuo cha Mafunzo huko Wete, ikiwa ni shamra shamra za miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisema matarajio ya Serikali ni  kwamba wananchi wa Wete na maeneo jirani, watashirikiana kikamilifu na maafisa na wapiganaji wa kikosi cha KMKM katika kupashana habari mbalimbali za kimagendo, uharibifu wa mazingira ya bahari na wahamiaji haramu kutoka nchi za jirani.

Aidha alisema matarajio ya Serikali baada ya kumalizika kwa mradi wa KMKM Wete na Gando, kipindi kilichopita utaenda kushuhudia mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika kikosi hicho Pemba.

Alisema fedha zilizotumika kwenye kujenga mazingira mazuri ya kambi hizo ni deni na kuzilipa kwao ni kuzidisha juhudi za kiutendaji na kitelejensia kuhakikisha hakuna anayejaribu kuendesha shughuli za kimagendo, shughuli za kuharibu mazingira ya bahari na shughuli za kiharamia.

“Ujenzi wa miradi hii utekelezaji wa vitendo wa malengo halisi ya Mapidnizi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambapo marehemu Sheikh Abeidi Amani Karume alipenda kuona wazanzibari wakishika dola yao na kuitumikia nchi yao katika mazingira bora ya kazi,”alisema.

Waziri Lela alisema katika kuhakikisha huduma ya urekebishaji tabia zinaboreka nchini, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikitoa fedha kwa chuo cha Mafunzo, kwa lengo la kuweza kutekeleza programu za kuwarekebisha tabia, wale wote waliotiwa hatiani na kuwekwa vizuizini.

Alisema pamoja na kutekeleza miradi ya mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa majengo ya ofisi na mahanga, sambamba  kuushauri uongozi wa Chuo Cha Mafunzo kwamba wakati umefika wa kukaa chini, na kufanya tathmini ya kina juu ya dhana ama nadharia iliyoasisiwa na Mwasisi wetu wa Mapinduzi Mzee Abeid Amani Karume kwa kukataa na kufuta neno Magereza na kukiita Kikosi hiki Chuo cha Mafunzo.

“Falsafa hii ya Chuo cha Mafunzo ndiyo kwa sasa duniani, inafanyiwa kazi na mataifa mbali mbali kwa lengo la kuhakikisha, wale wote waliohukumiwa vifungo wanapomaliza wanakuwa raia wema na kutoa mchango wao wa kiuchumi, kijamii na kisiasa,”alisema.

“Ni vyema nasi tukamsaidia kivitendo Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kuwatengeneza wanafunzi na mahabusu tulio nao kuwa raia wema na sio kuona mwanafunzi ama mahabusu, anamaliza kifungo au kizuizi baada ya mwezi anarudi tena kwa kufanya kosa kubwa zaidi ya lile la mwanzo,”alisema.

Akitoa salamu za wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mkuu wa Mkoa huo Salama Mbarouk Khatib, alisema haya majengo hayakuwa rahisi kupatikana kwani kazi kubwa imefanyika, hivyo aliwataka wananchi kutambua thamani ya vikosi hivyo katika suala zima la kusaidia jamii.

Aidha aliwataka kutoa mashirikiano ya pamoja, ikiwemo kutoa taarifa juu ya magendo kwani yanapokua yanaongezeka katika nchi, uchumi utadidimia, baada ya kupata maendeleo tutadhoofika kimaendeleo kutokana na magendo kuwepo.

“Niwape salamu wale wanaochukua karafuu zetu na kuzipeleka nchini Mombasa, sisi tunasema iwe jua au mvua, kelele za mlango hazimuumizi mwenye nyumba, ifike pahali tuseme heshma ya karafuu ya Zanzibar ibakie Zanzibar,”alisema.

Akisoma taarifa ya Kitaalamu juu ya ujenzi wamajengo hayo, Naibu katibu Mkuu Idara Maalumu za SMZ Mikidadi Mbarouk Mzee, alisema ujenzi wa hanga la wapiganaji wa KMKM na Ofisi za Utawala za KMKM zilikadiriwa kugharimu shilingi Bilioni Bilioni 1,110,004,850/= na mradi wa ujenzi wa jengo la ofisi ya zoni ya chuo cha mafunzo hadi kukamilika kwake ulikadiriwa kugharimu shilingi bilioni 1,317,871,119/= ambapo hadi sasa zimetumika 1,400,000,000/= sawa na asilimia 106.

Alisema kukamilika kwa miradi hiyo, kutaondosha changamoto ya uhaba wa Ofisi na Makaazi pamoja na kuongeza ufanisi katika kazi na kutimiza azma ya serikali kuwajengea mazingira bora ya kiutendaji watendaji wake.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar Khamis Bakar Khamis, alisema majengo hayo yamejengwa na vikosi hivyo husika, ni jambo la kujivunia sana kuona wanauwezo wakujenga majengo yao wenyewe bila ya kutegemea msaada kutoka kwengine.

Alisema jambo la kufurahisha kabisa ni kwamba fedha za ujenzi wa majengo hayo zimetoka serikalini, hilo ni jambo zuri huku akiomba serikali kuwapatia fedha Zaidi, kwani majengo hayo yatawasaidia kufanya kazi ipasavyo kwa ari na hamasa Zaidi.

MWISHO