Mukrim mohammed-Zanzibar
Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) limezindua mpango wake mpya wa kubadili muonekano na taswira yake kijamii na kibiashara hatua ambayo inalenga kuakisi ukuaji wa shirika hilo sambamba maboresho ya huduma zake kwa wateja.
Hatua hiyo mkakati inahusisha mfululizo wa mabadiliko chanya yanayohusisha muonekano mpya wa nembo ya shirika hilo, muonekano wa nyaraka rasmi za ofisi, maboresho ya huduma kwa wateja sambamba na mabadiliko ya muonekano wa ofisi za shirika hilo.
Hafla ya uzinduzi rasmi wa muonekano mpya wa ZIC imefanyika leo Zanzibar, ikiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dkt. Saada Mkuya Salum. Pamoja na Waziri Mkuya pia walikuwepo Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Khadija Issa Said, Balozi wa Bima nchini Wanu Hafidh Ameir (Mb), Mwenyekiti wa Bodi ya ZIC, Ramadhani Mwalimu Khamis, Mkurugenzi Muendeshaji wa ZIC Arafat Haji, wafanyakazi, na wadau mbalimbali wa shirika hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri Mkuya pamoja na kulipongeza shirika hilo kwa mabadiliko hayo alisema muonekano mpya wa ZIC, unaombatana na maboresho zaidi ya huduma zake utasaidia kuboresha zaidi imani ya umma juu ya shirika hilo na sekta ya bima kwa ujumla hatua ambayo itachochea mwamko wa wananchi wengi zaidi katika kutumia huduma za bima.
“Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya bima katika maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii yetu.
Tunatambua pia kuwa sekta ya bima inachangia katika ukuaji wa uchumi, kupunguza umasikini na kuimarisha usalama wa kifedha kwa wananchi wetu.
Na hiyo ndio sababu Serikali ina nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wake na wadau wa sekta ya bima hususani wale wanaoonyesha nia thabiti ya kujiendesha kwa ustadi mkubwa kama ZIC ili kuleta maendeleo katika sekta hii kupitia utoaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi wetu.’’ Alisema.
Katika hotuba yake wakati wa tukio hilo muhimu, Bw. Haji alielezea hamasa yake kuhusu hatua hiyo muhimu, akisisitiza kuwa inatokana na azma thabiti ya ZIC ya kuboresha zaidi muonekano wake kwa jamii kupitia maboresho ya huduma zake ili kukidhi matakwa ya soko la sasa na kukabiliana na ushindani mkubwa katika sekta ya bima.
“Tunapoimarisha nembo yetu na kubadilisha ofisi zetu, hatulengi tu kubadili muonekano wetu kuwa wa kisasa bali pia tulenga kuthibitisha ubora wa huduma zetu ili kuendelea kulinda imani waliyonayo wateja wetu kwetu kama shirika.
Nembo yetu mpya inawakilisha sifa ya weledi, uaminifu, na mawazo ya ubunifu yenye kuakisi kikamilifu lengo la ZIC la kulinda, kuwezesha, na kuhamasisha maendeleo ya watu binafsi na biashara kupitia suluhisho la bima lililoboreshwa,” alielezea.
Hatua ya shirikia hilo imekwenda sambamba na utekelezaji wa programu maalum ya mafunzo kwa wafanyakazi wake ili kuwajengea uwezo wa kwenda sambamba mabadiliko na kasi hiyo mpya inayohusisha ujuzi na weledi kwenye matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma za bima.
“Programu hizi za mafunzo zitawajengea wafanyakazi wetu ujuzi na maarifa muhimu ili kuwapa umakini binafsi, kutoa mrejesho wa haraka kwa wateja na kutoa ushauri wa kitaalamu na unaofaa kwa mahitaji ya wateja wetu. “
“Zaidi pia ofisi zetu zenye muonekano mpya zitasaidia kurahisisha mwingiliano na wateja wetu na hivyo kuongeza mvuto na ufanisi wa huduma zetu.” Aliongeza.
Kwa upande wake Balozi wa Bima nchini Wanu Hafidh Ameir (Mb) alisisitiza zaidi umuhimu wa mashirika ya bima nchini kuwekeza nguvu zaidi kwenye suala zima la utoaji wa elimu kuhusu umuhimu bima kwa wananchi ili kuwavutia zaidi waweze kutumia huduma hiyo muhimu.
“Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na mashirika ya bima nchini katika utoaji wa elimu bado matokeo sio ya kuridhisha sana. Tunahitaji kuongeza nguvu ya elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo hapa Zanzibar. Nawapongeza ZIC kwa huduma ya Bima inayozingatia misingi ya dini ya Kiislamu yaani ‘Takaful’ ambayo ni muhimu sana hapa Zanzibar…wito wangu elimu zaidi iongezwe kwenye huduma kama hii ili jamii ya Waislamu itambue kuwa ipo huduma inayozingatia misingi ya imani ya dini yao,’’ alisema.
Katika hotuba yake, Mwenyekiti wa Bodi ya ZIC, Bwana Ramadhan Mwalim Khamis alisisitiza zaidi dhamira ya kampuni hiyo katika kuendelea kuwa mtoa huduma wa bima mwenye kuaminika zaidi nchini. Alisema jitihada za mabadiliko hayo ni uthibitisho wa dhamira ya ZIC isiyoyumba ya kufikia malengo makubwa zaidi iliyojiwekea.
“Kwa mabadiliko haya tunayoyafanya yanalenga kuboresha sio tu taswira ya shirika lakini pia kutoa kiwango cha huduma na msaada usio na kifani kwa wateja wetu. Hatua hii ya kusisimua katika historia ya miaka 55 ya shirika yanawakilisha hatua muhimu kuelekea kuwa shirika la kutumainiwa zaidi katika utoaji huduma za bima katika ukanda wa Afrika Mashariki,’’ alisema.
Mwisho.