Thursday, December 26

JET yatoa mafunzo kwa waandishi wa habari 20

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

 CHAMA cha Waandishi wa habari za Mazingira Tanzania (JET), kinawakutanisha waandishi wa habari 20 kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania bara na Zanzibar, kwa ajili ya kuwapatia mafunzo juu ya masuala mbali mbali.

Chama hicho kimesema waandishi hao wataweza kupatiwa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya uhifadhi wa korido, hususan kupambana na uhalifu haramu wa Misitu, kupamba na uhalifu wa wanyamapori, Mabadiliko ya Tabianchi, jinsia na uhifadhi wa bioanuai, kupambana na uhalifu wa wanyamapori.

Akizungumza na mwandishi wa habari Mkurugenzi wa JET, John Chikomo alisema mafunzo hayo ni sehemu ya mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili Tanzania .

Chikomo alisema shuhuli za tuhifadhi Maliasili ni shughuli za miaka mitano, ambayo inashughulikia tishio kwa Wanyama na viumbe hai nchini Tanzania.

“Kuwapatia mafunzo haya waandishi wa habari watawezeshwa kupata maarifa, ujuzi, mtazamo sahihi wa kuweza kufanya taarifa za uchunguzi hukusu uhifadhi wa viumbe hai na masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Aidha alisema wanahabari watapatiwa uwezo na ujuzi wa masuala ya uhifadhi wa korido, ili kuchunguza, kuripoti na kuchambua uhisiano wa wanyamapori, uhifadhi wa bahari na misitu, biashara haramu na ujangili pamoja na kukuza uhifadhi wa wanyamapori na masuala ya utalii.

Sambamba na hayo mkurugenzi Chikomo, alisema mbali na kutengeneza mtandao kwa kuwaunganisha waandishi wa habari na wadau wa uhifadhi katika ngazi tofauti, waandishi wataboresha ubora wa habari zao kwenye korido, muunganisho wa wanyamapori na masuala ya uhifadhi wa viumbe hai.

Hata hivyo alizitaja koridoo ambazo wanayafanyia kazi ni pamoja na kutembelea Kwakuchinja Korido, inaunganisha mfumo wa Ikolojia wa Tarangire-Manyara(katika Wilaya za Babati na Monduli, Mikoa ya Manyara na Arusha).

Nyengine ni korido ya kigosi Moyowosi_Burugi Chato, inaunganisha Kigosi Moyowosi Complex na Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, jengine ni korido ya Nyerere Selous-Udzungwa unaunganisha hifadhi ya Taifa za Milima ya Nyerere Selous na Udzungwa katika mji wa Ifakara Mkoa wa Morogori.

Aidha korido nyengine ni Amani-nilo unaunganisha hifadhi ya Mazingira ya Amani na hifadhi ya Misitu ya Mazingira ya Nilo katika Wilaya ya Muhenza Mkoani Tanga, eneo Jengine ni korido ya Ruaha Rungwa-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, pori la akiba la Rungwa, mapori ya akiba ya Lukwati, pigi na katavu Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Maeneo mengine korido ya  Rungwa-Inyonga unaounganishwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Mapori ya akiba ya Rungwa na Inyonga katika Wilaya ya Itigi/sikongwe, Mkoani Singira/Tabora, pamoja na korido ya Mahale-Katavi unaounganisha Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale na Katavi Complex katika Wilaya ya Tanganyika na Uvinza Mkoani Katavi na Kigoma.

Hata hivyo alisema kupitia USAID Tuhifadhi Maliasili JET zitaweka mazingira wezeshi kwa waandishi wa habari kufanya ugunguzi na kuripoti masuala ya uhifadhi na kutangaza korido na muunganisho wa wanyamapori na masuala mengine.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper/habari portal.
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355