Wednesday, October 30

WADAU WATAKIWA KUONGEZA NGUVU MAPAMBANO DHIDI YA KUPIGA VITA MATUMIZI DAWA ZA KULEVYA ZANZIBAR.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Bi, Harusi Sadi Suleiman, akifungua kongamano la siku moja la kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya Zanzibar, lililoandaliwa na Tume ya Kitaifa ya kuratibu na Udhibiti wa dawa za kulevya, kutoka Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais, lililofanyika katika ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba

   PEMBA

Amref Tanzania kupitia ufadhili wa Kituo cha Serikali ya Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) Tanzania) wameunga na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Wizara ya Afya Zanzibar, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Zanzibar (ZDCEA), Wadau na Wataalam mbalimbali katika Kongamano la kujadili mipango na mikakati ya kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya Zanzibar Tanzania.

Kongamano hilo la maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya Zanzibar yalifanyika chini ya kauli mbiu; “Ushahidi Upo Wazi Tuwekeze Katika Kukinga”na  ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.

Kupitia ufadhili wa CDC Tanzania, Amref Tanzania inashirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, ZDCEA na wadau wengine katika kutoa huduma za waraibu ambapo huduma za Medication-Assisted Treatment (MAT) hutolewa kwa waraibu wa dawa za kulevya katika hospitali ya Kidongo Chekundu Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Harusi Sadi Suleiman amewataka wadau, kuendelea kuunganisha nguvu za pamoja kwenye mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya, ili kutokomeza kabisa Vita vya Matumizi ya Dawa za Kulevya Zanzibar.

Wito huo aliutoa wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya duniani, wakati akizungumza kwa niaba ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud Othman, na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema kuwa matumizi ya dawa za kulevya hususani kwa vijana kuanzia miaka tisa hadi 45 ndani ya jamii, bado ni changamoto inayohitaji kufanyiwa ufumbuzi.

Alisema kuwa jamii ama familia, wakiwa tayari kushirikiana pamoja katika kupiga vita changamoto hiyo, wataweza kuondosha wale wahalifu ambao wanahusika na tatizo hilo nchini.

“Kutokana na tatizo kuwa kubwa siku hadi ndani ya nchi yetu, tuhakikishe tunashirikiana kujua kwamba kazi yakupambana na hilo sio ya mtu mmoja, bali ni jukumu la kila mmoja wetu ili tuweze kusaidia kizazi chenye nguvu kazi ya taifa,” alisema.

Alieleza kuwa matumi ya dawa za kulevya nchini huleta athari mbali mbali, kwa watumiaji ikiwemo kiafya na mwili,jambo ambalo linachangia kuwepo kwa vijana wengi wasio na maendeleo.

Alisema kuwa licha ya jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na mataifa kikanda, na kimataifa kwenye pembe zote za dunia katika kupambana na tatizo hilo, lakini bado ni changamoto kwa kizazi na jamii.

“Tatizo la dawa za kulevya linasadikiwa kwamba linauwezo mkubwa katika kuleta athari kwa watumiaji, kwani mtumiaji anaweza kupata maradhi mabli mbali ikiwemo homa ya ini B na C, Ukimwi, na magonjwa mengine ya zinaa,” alieleza.

Aidha aliitaka jamii kuhakikisha wanapambana na tatizo hilo kwa kusambaratisha mitandao, kuchukua hatua kali bila woga, ili lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa kwa mabadiliko chanya ndani ya nchi kwa maslahi ya jamii.

Kamishna mkuu wa Mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya Pemba Burhani Zuberi Nassoro, akizungumza wakati wa kongamano

Mapema Kamishna mkuu wa Mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya Pemba Burhani Zuberi Nassoro, alieleza kuwa ili changamoto hiyo iweze kuondoka ni vyema jamii kuongeza ushirikiano katika kutaja wahalifu bila woga kwa maslahi ya taifa.

“Kuanzia Mkoa hadi shehia tunadhamiria kuondosha matumizi ya madawa ya kulevya kuanzia maandalizi, viashiria vyote vya madawa ya kulevya, ni lazima jamii yenyewe kutoa taarifa sahihi bila kuogopa kwa maendeleo ya nchi,” alieleza kamishna.

Alieleza kuwa endapo kila mmoja ataweza kuwajibika ipasavyo katika kupiga vita madawa ya kulevya nchini, basi lengo lililokusudiwa litaweza kufikiwa.

“Kumekuwa na maeneo ambayo yameathirika na utumizi wa madawa ya kulevya yamekuwa na changamoto nyingi, ikiwemo kuwepo kwa udhalilishaji, mauaji, wizi, na mengine kama hayo, alisema.

Aidha Kamishna huyo alihakikisha kwamba wataendelea kupambana kwa kuwachukulia hatua kali wale watakapatikana na uhalifu huo bila kumuonea huruma, ili nchi ibaki kuwa salama.

Hata hivyo aliwataka wazazi wenye vijana wa matumzi wa madawa ya kulevya kutowanyanyapaa kwani bado nafasi wanayo ya kuacha na kufikia malengo ambayo waliyatarajia  kuyafikia.

Kwa upande wake kaimu Katibu mkuu Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais Ilyasa P.Haji, alisema kuwa matumizi ya madawa ya kulevya yanawafanya vijana kupoteza malengo yao ambayo walitarajia kuyafikia kimaendeleo.

Miongoni mwa mada tatu ambazo ziliwasilishwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na Dawa za kulevya na afya ya akili, Uhalifu wa dawa za kulevya na hatua za kukabiliqna na Udhaifu, na mada ya tatu ni Sheria namba 8 ya nwaka 2021 ya Mamlaka ya Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya .

 

Akiwasilisha mada ya kwanza kuhusu dawa za kulevya na afya ya akili katika kongamano hilo, Dkt. Ally Yussuf Ally alifahamisha kuwa watumiaji wakubwa wa madawa ya kulevya nchini ni vijana wadogo, ambapo tafiti zinasema kwamba ni zaidi ya vijana elfu 15,000 wanaotumia madawa hayo.

Alisema mambo yanayopelekea athari kwa mtu anaetumia madawa ya kulevya ni pamoja na madawa wenyewe kuingia kwenye damu mishipa ya ubongo iitwayo ‘Limbic system.’

   

Washiriki wa Kongamano la siku moja la kupiga Vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya Zaznibar, wakifuatilia kwa makini kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Bi Harusi Sadi Suleiman, akimkabidhi cheti cha shukrani Rukia Salim Afisa Kinga maswala ya UKIMWI kutoka Amref Tanzania wakati wa kongamano la kuadhimisha siku ya kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya lilofanyika kisiwani Pemba.

Picha ya Pamoja na Mgeni Rasmi, Bi Harusi Sadi Suleiman, katika kongamano la siku moja la kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya Zanzibar, lililoandaliwa na Tume ya Kitaifa ya kuratibu na Udhibiti wa dawa za kulevya, kutoka Ofisi ya Mkamu wa Pili wa Rais, lililofanyika katika ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.