PEMBA
Walimu kisiwani Pemba wametakiwa kuacha tabia ya kujiunga na taasisi za mikopo za kausha damu na badala yake kuchukuwa mikopo katika taasisi za uhakika ikiwemo Benk ya NMB.
Akizungumza na walimu na watendaji wa NMB huko katika ukumbi wa Hoteli ya Safari ilioko Tibirinzi kisiwani Pemba mkuu wa mkoa wa Kusini Mattar Zahor Massoud alisema Benk hiyo inakwenda sambamba na kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassana na Rais wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwiyi za kuwapatia huduma za kifedha wananchi karibu na maeneo yao.
Alieleza Benk hiyo imekuwa karibu na wateja wake na kuwajali sambamba na kuboresha na kuwa wabunifu wa huduma mbali mbali ikiwemo mikopo ambazo zinawafanya wateja waliowengi kuchukuwa mikopo kupitia benk hiyo.
Alifahamisha kuwa NMB ni benki ambayo imekuwa karibu sana na jamii ya Watanzania hususan Walimu na kuweza kuwapatia mikopo ya aina mbali mbali inayowawezesha kuendeleza shuhuli zao za kimaisha.
Matar aliwataka Walimu kuelewa kwamba wao ni wafundishaji hivyo mafunzo watakayopatiwa na Watendaji wa Benk hiyo kuyafuatilia kwa kina ili nao wawe mabalozi kwa walimu wengine ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria siku hiyo ambayo ni mahususi kwa NMB kukutana na wateja wao.
Alisema NMB inaelewa umuhimu wa wateja wake na ndio ikaamuwa kuweka siku maalumu ya kukutana na wateja wake kubadilishana mawazo ambapo kwa Pemba walimu wa Skuli wanaongoza kwa kuitumia Benk hiyo.
“ NMB inajuwa umuhimu wenu na ndio ikawapatia fursa hii ya kukutana nanyi ili muweze kutowa mawazo yenu na wao kutowa mawazo yao kwa nia ya kuboresha huduma bora za Benk hii”, alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa aliziomba Benk nyengine kuiga mfano wa NMB kwa kuwa wabunifu wa huduma mbali mbali za Kibenk ili waweze kupata wateja wengi zaidi kama walivyo wenzao wa NMB.
Aidha Matar aliwahimiza Walimu kufunguwa account za watoto wao ili ziweze kuwasaidia katika Elimu kwa vile ndio kitu muhimu na account hiyo ni salama na inamsaada mkubwa kwa watoto.
Aliishauri Benk ya NMB kuanzisha utaratibu wakutowa mafunzo kwa wafanyakazi wastaafu ambao wako karibu na kustaafu ili waweze kujiandaa na mapema kutumia fedha zao kwa kujiwekea malengo.
“ Itakuwa jambo la faraja mukianzisha utaratibu wa kutowa mafunzo kwa wastaafu ili waweze kujiwekea malengo ya matumizi ya fedha pale watapofika muda wa utumishi wao “, alisema.wa upande wake
Ofisa Mdhamini Wizara ya Elimu Pemba , Mohamed Nassor Salim aliitaka Benk ya NMB isiogope kuwapatia mikopo Walimu kwani ajira na utumishi wao uko salama na kwa mujibu wa sheria kwa maana hiyo fedha zao hazitopotea.
Aliwashauri Walimu hao kuendelea kupokea huduma zinazotolewa na Benk hiyo kwani anaiamini na iko salama kwani inasimamia maslahi ya Taifa kwa kuwajengea mazingira salama wateja wao kwa kuwapatia mikopo.
“ Niwasihi Walimu wenzangu kopeni NMB kwa mujibu wa sheria za Utumishi ili muweze kurejesha mikopo yenu kirahisi na bila ya mivutano “, alisema.
Aidha Mdhamini huyo aliwataka walimu kufanyakazi zao kwa kuweka mbele Uzalendo zaidi na kwa uadilifu ili kulinda ajira zao zitakazo wafanya waweze kukopesheka kupitia huduma za kifedha ikiwemo Benk ya NMB.
Hata hivyo aliishukuru Benk hiyo kwa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Elimu jambo ambalo Walimu waliowengi wamekuwa wakipata huduma za mikopo kupitia kwao.
Nae Mwakilishi wa Meneja wa kanda ambae pia ni Meneja wa Benk ya NMB Tawi la Zanzibar Ahmed Nassor alisema Benk hiyo imekuwa na kawaida kila mwaka kukutana na Wadau wake kwa kubadilishana mawazo na kuwajenga kimafunzo juu ya masuala mbali mbali ya kifedha.
Alieleza wameamuwa kukutana na wateja wao ambao wengi ni Walimu wa skuli kwa vile NMB imekuwa na makubaliano na Wizara ya Elimu kuwapatia mikopo Walimu wake ambapo kwa sasa wanao wateja 500 ambao wanapata huduma hizo ambao wote mikutoka Elimu.
“ Niwaombe wanachama wetu muwe makini kujifunza haya mafunzo ambayo munapatiwa hapa ili na nyinyi mukawe mabalozi kwa wale wenzenu wasiokuwepo kwa nia ya kujiendeleza zaidi”, alieleza.
Nae Meneja Mwandamizi kitengo cha Wateja binafsi wa NMB, Quen Kinyamagoha alisema kuwa Benk yao inazohuduma bora za fedha ambazo zinawawezesha kupatiwa mikopo wateja wake popote pale walipo.
Alieleza NMB itaendelea kuwa msuluhishi bora wa huduma za kifedha kwa wateja wake na kuwataka kuwaelimisha wengine kufungua accout kupitia benk hiyo ili waweze kufaidika na fursa zinazotolewa na NMB.
Hata hivyo aliwataka wadau hao kuendelea kuweka fedha zao kupitia Benk hiyo hatimae wapate kufaidika na fursa mbali mbali zinazopatikana kupitia Benk ya NMB.
MWISHO.