NA ZUHURA JUMA, PEMBA
TANI 20 za mchele mbovu pamoja na tende tani 4.1 zimeteketezwa katika shehia ya Pujini Wilaya ya Chake Chake baada ya kuonekana bidhaa hizo hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza baada ya uteketezaji wa bidhaa hizo Mkurugenzi wa Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) Pemba, Nassir Salum Buheti alisema bidhaa hizo zimepatika kwenye maduka tofauti tofauti na maghala katika Wilaya ya Mkoani kufuatia operesheni yao ya kukagua bidhaa.
Alisema kuwa, kwa mashirikiano ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani na Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba walifanikiwa kukamata bidhaa hizo tani 24.1 za mchele na tende ambazo zimepitiwa na muda na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
“Zoezi hili la kukagua bidhaa ni endelevu na tunaendelea katika Wilaya nyengine, ili kuhakikisha bidhaa zote za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba vinakuwa salama na vyenye ubora kwa ajili ya kutumika kwenye jamii”, alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alifahamisha kuwa, katika operesheni hiyo walibaini kuwepo watu wanaokusanya mchele na bidhaa nyengne kwa lengo la kutoa sadaka ambazo huhifadhi kwenye majumba yao, kitu ambacho sio sahihi.
“Na hii tende ambayo imeshapitiwa na muda mwenyewe kaiweka kwa ajili ya kutoa sadaka, wafanyabiashara hii haifai kwani munahatarisha maisha ya watu”, alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, wanapita shehia zote kukagua maduka na maghala (bubu) ambayo hayatambuliki, ili kuhakikisha yatakuwa salama na bidhaa zinakuwa na ubora.
Pia Mkurugenzi huyo alisema, katika uteketezaji huo wa bidhaa walishirikiana na Taasisi ya Viwango Pemba (ZBS) ambao wao walikamata nusu tani ya unga wa sembe, ambapo waliangamiza bidhaa hizo kwa pamoja.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Chakula kutoka ZFDA Pemba, Saade Omar Hamad alisema taasisi hiyo imejipanga katika kuhakikisha wananchi wanakula vyakula salama na vyenye ubora.
“Hatutokubali Pemba ikawa ni jaa la kupitisha vyakula vibovu, wafanyabiashara mlielewe hilo, hakikisheni mnaleta bidhaa ambazo hazijaishiwa na muda na zenye ubora”, alifahamisha.
Mkuu huyo alisema, mtu yeyote atakaetoa msaada kisiwani Pemba lazima ahakikishe anafika Ofisi ya ZFDA kwa ajili ya kukaguliwa bidhaa hiyo, ili isije ikaleta mardhara kwa wananchi.
Nae Afisa Ukaguzi na Udhibiti Ubora kutoka ZBS Pemba Lulu Hamad Mussa alisema, kwa kushirikiana na ZFDA wanateketeza bidhaa hizo, ambapo wao walikuwa na unga wa sembe nusu tani walioukamata kwa mzalishaji ambae anatumia leseni ya ubora ya ZBS kwa bidhaa yake.
“Tunapotoa leseni tunakuwa tunafuatilia na ndio maana tulikamata bidhaa ya mzalishaji huyu ikiwa tayari imeshapitiwa na muda kwa kugundua kuna kiwango kikubwa Cha sumu kuvu kuliko ile inayohitajika kuwemo katika bidhaa hiyo”, alisema Afisa huyo.
Alisema kuwa, wamechukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kumsimamisha uzalishaji huo mpaka pale atakapoboresha na kuhakikisha wanaendelea kuondosha bidhaa hiyo masokoni, ili kuona athari hiyo haimpati mwananchi.
ZFDA kwa kushirikiana na ZBS Pemba wameteketeza tani 24.1 za mchele mbovu na tende, pamoja na nusu tani ya unga wa sembe ambavyo havifai kwa matumizi ya binadamu.