NA ZUHURA JUMA, PEMBA
JUMLA ya kesi 61 za madawa ya kulevya zimeripotika katika kituo cha Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba kuanzia Januari mwaka 2019 hadi Disemba mwaka 2020.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis alisema, mwaka 2019 ziliripotiwa kesi 28 na mwaka 2020 zimeripotiwa kesi 33.
Alisema kuwa, kesi za madawa ya kulevya zimeongezeka kutoka 28 ya mwaka 2019 hadi kufikia kesi 33 kwa mwaka 2020 kutokana na vijana wengi kujiingiza kwenye biashara hiyo haramu.
“Licha ya kufanya doria na kuwakamata waingizaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya lakini bado vijana wanaendelea na biashara hiyo haramu, jambo ambalo ni kosa kisheria”, alisema Kamanda.
Alieleza kuwa, wamekuwa wakipambana katika kutokomeza janga hilo hatari kwa jamii kwa kuwasaka vijana wanaojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya, ili kuweza kuondosha janga hilo.
“Kwa kweli vijana wetu wanapoteza nguvu kazi ya Taifa, kwa sababu wanalewa kupita kiasi, hatima yake wanaiba na kuwafanyia watoto udhalilishaji, kuna kazi nyingi za halali hawafanyi”, alisema.
Alifahamisha kuwa, ipo haja ya kushirikiana pamoja ili kuhakikisha wanawanyanyua vijana katika nyanja mbali bali za kiuchumi ambazo zitawapatia kipato cha halali.
Aliwataka vijana kufanya kazi za halali ikiwemo za kilimo, mifugo na uvuvi ambazo zitawapatia kipato kitakachowasaidia kutatua shida zao na kuhudumia familia zao.
“Madawa ya kulevya ni kazi ya haramu, hivyo itakuletea mashaka katika maisha yako ya hapa duniani na akhera, sisi hatukuachi tukikikamata tutakufikisha mahakamani”, alisema.
Kamanda Sadi alieleza kuwa, kuna bandari bubu zisizopungua 100 katika Mkoa huo ambazo hutumika kuingizia dawa hizo, hivyo mikakati yao ni kuhakikisha wanadhibiti sehemu hizo, ili kupunguza uingizaji wa madawa hayo.
Alisema kuwa, kikosi cha kuzuia magendo Mkoa huo (KMKM) kimekuwa kikifanya doria katika maeneo ya bahari kuhakikisha mkoa haupitishi biashara haramu.
“Kwa kweli wenzetu wa KMKM wanajitahidi kufanya doria katika maeneo ya baharini na sisi tunafanya maeneo yote ya bandari pamoja na mitaani, tunashkuru tunafanikiwa kuwakamata”, alisema Kamanda.
Aliiomba jamii izidishe ushirikiano katika kuhakikisha madawa ya kulevya hayaingizwi wala hayauzwi katika Mkoa wa Kakazini na pia watoe taarifa pale watakaposikia kuna sehemu ama mtu anauza.
Kwa mwezi wa Januari mwaka huu hakuna kesi ya dawa za kulevya iliyoripotiwa.