AFISA Mdhamini Ofisi ya Rais Katiba sheria Utumishi na utawala bora Halima Khamis Ali, amewataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo kuzidisha mashirikianao katika kufanya kazi, kwani ni jambo muhimu litakalopeleka mabadiliko makubwa sana.
Hali yaliyaeleza hayo mara baada ya kumalizika kwa makabidhiano ya ofisi hiyo, huko katika ukumbi wa wizara hiyo Gombani Chake Chake Pemba.
Alisema mashirikiano yakiwepo basi hakuna kitakacholala, hata utendaji wa taasisi utaweza kubadilika kwa wafanyakazi, huku akiahidi kuondosha makundi baina ya wafanyakazi katika ofisi.
“Leo tumekutana wakuu wa maidara vizuri kuheshimiana na kufanya kazi kwa kufuata miongozo, huku tukikumbuka kuwa wizara yetu ni wizara muhimu katika kusimamia sheria na kanuni za wafanyakazi, isije ikawa sisi ndio wavunjaji wakubwa wa kanuni na sheria hizo”alisema.
Hata hivyo aliwataka watumishi hao kuhakikisha wanatambua thamani ya wizara hiyo, kila mtu kutekeleza majukumu yake kikamilifu, huku akiahidi kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
Wakati huo huo naye afisa mdhamini Ofisi ya makamu wa kwanza wa Rais Ahmed Abubakar Mohamed, alishukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, kwa kumuamini na kumpatia nafasi hiyo ya kuongoza Wizara.
Aidha aliahidi kutekeleza majukumu yake kikamilifu, kwa kushirikiana na watendaji mbali mbali kutoka katika wizara hiyo, ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya nane.
Kwa upande wake Fatma Marouzuk, aliwataka wafanyakazi wenzake kuoendeleza mashirikiano kwa viongozi wao wapya, kama walivyokuwa kwa viongozi waliopita.