Monday, November 25

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi atoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Dk. Mohamed Seif Khatib

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kufuatia kifo cha Dk. Mohamed Seif Khatib aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar pamoja na Mjumbe wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma.
Kifo cha Dk. Mohamed Seif Khatib kimetokea leo (Februari 15,2021) katika Hospitali ya Al-Rahma, jijini Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa kesho saa nne huko kijijini kwao Umbuji, Jimbo la Uzini, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa amepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Dk. Mohamed Seif Khatib.
Salamu hizo zilieleza kwamba yeye binafsi, familia yake pamoja na wananchi wa Zanzibar na wa Tanzania kwa ujumla wamesikitishwa na kuhuzunishwa na kifo hicho.
“Mimi namfahamu Dk. Mohamed Seif Khatib kuwa ni kiongozi mahiri, aliyependa kazi, mvumilivu na aliekuwa na mashirikiano mazuri na wenzake wote ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar”, ilieleza sehemu ya salamu hizo za rambirambi.
Aidha, kupitia salamu hizo za rambirambi, Rais Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu kuwapa moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hichi kigumu cha msiba, familia, marafiki, ndugu pamoja na wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
Salamu hizo ziliendelea kumuomba MwenyeziMungu kumpa rehma na kumjaalia makaazi mema peponi. Amin.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
Mwandishi wa Habari wa Rais wa Zanzibar.