NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WAJASIRIAMALI wa kikundi cha mboga mboga ‘Green House’ kilichopo shehia ya Tumbe Mashariki wameiomba Serikali kuwapatia mafunzo, ili wawe na utaalamu wa kukabiliana na magonjwa yanayokumba kwenye mazao yao.
Walisema kuwa, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maradhi kwenye kilimo chao cha mboga mboga, ingawa wanashindwa kukabiliana nayo kutokana na kukosa utaalamu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika shamba lao huko Tumbe, wakulima hao walieleza kuwa elimu ni muhimu kwao kwani itawasaidia katika kutatua baadhi ya changamoto.
“Tunahitaji mafunzo ya hali ya juu, kwani tunalima na kuzalisha kwa wingi lakini mwisho wa siku tunajikuta na mavuno kidogo kutokana na kuwa mazao hayo hukumbwa na magonjwa”, walisema wakulima hao.
Mwenyekiti wa kikundi hicho Ali Juma Shaib alisema, wanajitahidi kulima mboga mboga za aina mbali mbali kwa lengo la kujikomboa kiuchumi, ingawa bado wanakwama kutokana na changamoto zinazowakabili.
Alisema kuwa, iwapo watapatiwa elimu ya kilimo wataweza kujifunza vitu mbali mbali na kutafuta mbinu ya kuweza kuondosha maradhi, ambayo husababisha kupukutika kwa mazao yao yakiwa karibu na kuvunwa.
“Kwa kweli nguvu zetu zinapotea bila kupata faida, kwa sababu hatujui kitu gani kinakumba katika mazao yetu, hivyo tupatiwe utaalamu ili tupambane na hali hii wenyewe”, alisema Mwenyekiti huyo.
Kwa upande wake Mjumbe wa kikundi hicho Adam Khamis Mohamed alisema, hawajahi kutembelewa na wataalamu hali ambayo inawasikitisha sana, kwani hawapati kujifunza vitu.
“Tunataka tupambane na wadudu ambao hutuharibia na kutukatisha tama katika kuendelea na kilimo hicho, hivyo wataalamu angalau wapite kutukagua ili kupata maelekezo yao”, alisema.
Nae Mjumbe Mchanga Salim Ali alisema kuwa, pia wanahitaji maji ya kumwagilia katika kilimo hicho, ili kuweza kustawi vizuri na kupata mazao bora.
“Tunalima mchicha, mabilingani, tungule, nyanya chungu, mabamia, pilipili, ambapo yote hayo yanahitaji maji ili yaweze kustawi vizuri”, alisema dada huyo.
Mjumbe wa kikundi hicho Faudhia Khamis Massoud alisema, ili kilimo chao kiwe imara na kupata mazao bora, ipo haja ya kusaidiwa pembejeo ikiwemo mbolea, dawa, mbegu za kisasa, keni za kutia maji na majembe.
“Iwapo tutasaidiwa kutatuliwa changamoto zinazotukabili tunaweza kufanikiwa kufikia lengo, kwani soko lipo kiasi hivyo tutapata fedha ya kujikimu”, alieleza.
Kombo Khamis Ali aliiomba Serikali kuwawezesha vijana ambao wamejikita katika shughuli mbali mbali za ujasiriamali, kwa kuwapatia nyenzo muhimu za kufanyia kazi pamoja na elimu, ili wajikwamue na maisha duni.
“Hii itatupa hamasa kubwa sana ya kujituma zaidi na kuacha kufanya mambo yasiyofaa ndani ya jamii, hivyo ipo haja ya kusaidiwa ili kufanikiwa, hali ambayo itawavutia na wengine waliojipweteka”, alisema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni Hamad Mbwana Shehe alisema kuwa, wataalamu wa kilimo kutoka Halmashauri tayari wameshafika kuwapa taaluma wakulima hao, ingawa inategemea na walivyoipokea.
Alisema kuwa, wanapokuwa na tatizo wanaombwa wafike kwa sheha wa shehia yao, ambapo atawapelekea bwana shamba, ili aweze kuwasaidia kutatua changamoto zinazowakabili.
“Au waje hapa Halmashauri kueleza tatizo lao, tutawasaidia kuwapa taaluma, na pale hali itakaporuhusu pia tutawasaidia na vitendea kazi, kwani tunaamini lengo lao ni kujikwamua kimaisha”, alisema Mkurugenzi huyo.
Alifahamisha kuwa, wana program maalumu za kuwafikia wanavikundi hao wa ‘Green house’ zilizopo katika Wilaya yao na kuwapeleka katika Wilaya nyengine kujifunza kwa wenzao ambao kilimo chao imeonekana kunawiri vizuri.
Kikundi hicho cha vijana chenye wanachama 18 wakiwemo wanawake tisa na wanaume tisa, kimeanzishwa mwaka 2020 kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.