Monday, November 25

Miaka 40 ya kupanda na kushuka kwa Maalim Seif

  • Ezekiel Kamwaga
  • Mchambuzi
17 Februari 2021
Maisha ya utu uzima ya mwanasiasa mkongwe mpinzni wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad (76), ni maisha ya subira na uvumilivu.

Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, hakuna mwanasiasa wa Tanzania aliyepitia njia aliyopita Makamu Rais huyu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Alipomaliza sekondari mwaka 1963 akiwa mmoja wa wanafunzi waliofaulu vizuri visiwani Zanzibar, alitakiwa kujiunga katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa masomo ya shahada ya kwanza lakini wakati ulipofika, alikuta kuna katazo la serikali kutaka vijana wa Kizanzibari wabaki kwanza kujaza nafasi zilizoachwa na wakoloni.

Ilibidi asubiri hadi mwaka 1972 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa SMZ, Abeid Amani Karume – aliyeweka katazo la vijana kwenda kusoma chuo kikuu, ndipo hatimaye alipopata ruhusa ya kwenda kujiunga na UDSM alikosomea shahada yake ya Sayansi ya Siasa.

Maalim Seif alifikiriwa na wengi kuwa angekuwa mrithi wa Ali Hassan Mwinyi kama Rais wa Zanzibar mara baada ya Rais huyo wa Awamu ya Pili kupitishwa kuwania nafasi hiyo mwaka 1985.

Mwinyi na Maalim Seif walifanya kazi nzuri kama timu kwa pamoja katika kipindi kifupi cha kati ya mwaka 1984 hadi 1985 wakati walipojikuta wakishika nyadhifa mbili za juu za uongozi wa Zanzibar; Rais na Waziri Kiongozi mtawalia, na ilitarajiwa kuwa Maalim angeendeleza pale walipoishia.

Hata hivyo, Maalim alitakiwa kusubiri na badala yake nafasi hiyo ikaenda Idris Abdul Wakil, mwanasiasa aliyekosa mvuto wa kisiasa kiasi cha kupata nusu ya kura zote za urais katika uchaguzi wa mwaka 1985 ingawa alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo.

MAA

Maalim Seif alibaki kusubiri kwa sababu umri ulikuwa upande wake. Wakati hayo yakitokea, Maalim alikuwa ndiyo kwanza yuko mwanzoni mwa miaka yake 40 ya kwanza duniani – na kwa busara za wakati ule, alikuwa bado kijana na nafasi hiyo angeweza kuipata baadaye.

Mwaka 1988, kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka za siri za serikali, Maalim Seif aliondolewa katika wadhifa wake huo wa Waziri Kiongozi na kuvuliwa nyadhifa zake zote ndani ya CCM. Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa mwanasiasa huyo ambaye wakati fulani akionekana kipenzi cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mwaka 1989 tuhuma zake hizo ziliondolewa lakini bado akawekwa kizuizini kama mfungwa wa kisiasa na akaachiwa mwaka 1991 wakati Tanzania ilipoanza mageuzi ya kuelekea mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Pasi na shaka, subra na dhamira ya kutaka kuwatumikia Wazanzibari katika nafasi ya juu ndiyo iliyomfanya atoke kizuizini akiwa na ari ileile aliyoingia nayo.

Hii ni hadithi ya mtu aliyepata kuwa msomi mashuhuri, akaja kuwa kiongozi wa kuaminika wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiasi cha kupewa wadhifa wa Katibu wa Kamati ya Uchumi ya chama hicho; mojawapo kati ya nafasi nyeti kabisa wakati chama kikiwa kimeshika hatamu ya uongozi – akiwa na umri wa chini ya miaka 40.

Maalim Seif, katika muktadha huu, ndiye Waziri Kiongozi pekee na Makamu wa Rais wa Tanzania ambaye alipitia kadhia hii ya kuwekwa kuzuizini kwa muda wa takribani miaka miwili.

Rais Abood Jumbe Mwinyi, aliyemteua Maalim Seif kuwa Waziri Kiongozi kwa mara ya kwanza, naye aliishi Mji Mwema, Dar es Salaam kwa takribani miaka 30 baada ya kung’olewa kwenye Urais mwaka 1984, hahesabiki kama alikuwa kizuizini kwa sababu aliishi uraiani – hata kama nyendo zake zote zilikuwa zikichunguzwa na hakuwahi kuruhusiwa kurudi kuishi kwao Zanzibar.

Anashinda lakini hapewi?

Katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995, Maalim Seif aliwania Urais kupitia Chama cha Wananchi (CUF), alichokiasisi yeye na wenzake akina Shaabani Mloo, mara baada ya kuachiwa kutoka kizuizini.

Uchaguzi ule ulikuwa wa kihistoria kwa sababu matokeo ya kwanza yaliyotolewa na chombo cha habari – kituo cha televisheni cha DTV, yalimpa ushindi Maalim Seif dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma.

Hata hivyo, matokeo ya mwisho yaliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), yalitoa ushindi wa asilimia 50.24 kwa CCM dhidi ya asilimia 49.76 za CUF.

Matokeo hayo nusura yavuruge amani ya Zanzibar. Ni matokeo ambayo pia yaliishtua CCM kwa sababu ilishindwa vibaya katika kisiwa cha Pemba anakotoka Maalim kiasi cha kutopata kiti hata kimoja cha ubunge wala Uwakilishi. Kimsingi, katika mfumo wa vyama vingi, Pemba imekuwa ngome isiyotetereka ya Maalim Seif.

Ni subra ya Maalim Seif ndiyo iliyokipitisha chama chake katika kipindi cha kati ya mwaka 1995 hadi mwaka 2000.

Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Maalim aliwania nafasi hiyo na Amani Karume wa Zanzibar ambaye kupitishwa kwake na CCM kulikuwa na mizengwe ya kichama iliyoleta mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa visiwa hivyo.

Wakati matokeo yalipotangazwa, Maalim alitangazwa kupata asilimia 32.96 huku Karume akitangazwa kupata asilimia 67.04.

Matokeo hayo yaliwatia hasira wafuasi wa Maalim Seif kiasi kwamba Januari 28, 2001, waliandamana kupinga matokeo katika tukio lililosababisha mauaji na Wazanzibari kukimbia nchi yao.

Maalim

Wafuasi wa Maalim Seif wanaamini kwamba katika chaguzi zote alizoshiriki kama mgombea urais wa Zanzibar – 1995,2000, 2005,2010, 2015 na mwishowe 2020, mwanasiasa huyu kutoka Pemba hakuwahi kushinda ila hakuwahi kutangazwa kushinda.

Ni Maalim Seif huyuhuyu ambaye alikubali kukiingiza chama chake katika mazungumzo yaliyojulikana kwa jina la Mwafaka I, II na III, mar azote kwa lengo la kuleta maridhiano ya kisiasa katika visiwa vya Zanzibar.

Ni wazi kwamba katika historia ya kisiasa ya Tanzania, hakuna mwanasiasa mmoja ambaye anaweza kujidai kuwa na ufuasi na kudumu na wafuasi wake kwa muda mrefu kumzidi Maalim.

Kete hiyo ndiyo iliyomfanya kukubali kushiriki katika mazungumzo ya maridhiano hata kama wakati mwingine jambo hilo lilileta shida hata kati ya viongozi wenzake na wanachama wenye misimamo mikali.

Mwaka 2010, Maalim Seif alikubali wadhifa wa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar iliyoundwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, uliompa ushindi aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Magu

Kuundwa kwa Serikali hiyo kulitokana na mazungumzo yaliyoanza kwa siri kati ya Maalim na Karume – katika kipindi ambacho wahafidhina wa pande zote mbili walikuwa wakikataa mazungumzo ya aina yoyote. Pamoja na kulaumiwa na wahafidhina wa chama chake, Maalim aliingia katika serikali na Zanzibar ikapitia katika kipindi cha kwanza cha siasa za kistaarabu tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Uchaguzi wa mwaka 2015 ulileta mgogoro mkubwa wa kisiasa ndani ya chama alichokiasisi cha CUF. Mgogoro huo ulikuwa dhidi ya kambi ya wanachama waliomuunga mkono na wale waliokuwa katika kambi ya Profesa Ibrahim Lipumba – Mwenyekiti wa CUF.

Chanzo cha mgogoro huo kilitokana na uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo Lipumba alitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo akipinga kitendo cha CUF kumuunga mkono aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi huo, Edward Lowassa.

Baada ya uchaguzi huo, Lipumba alidai kwamba barua yake ya kujiuzulu Uenyekiti wa CUF haikuwa imejibiwa kama taratibu za chama hicho zinavyotaka na hivyo kimsingi yeye bado ni Mwenyekiti.

Mgogoro ukaanzia hapo.

Baada ya misuguano ya takribani miaka mitatu ikiwamo kupeleka kesi mahakamani na kufukuzana katika chama, subra ya Maalim Seif ilifikia kikomo na akatangaza kuhama CUF na kujiunga na ACT Wazalendo – katika tukio litakalobaki katika historia kwa sababu hotuba ya dakika nane ya Maalim kutangaza kuhama chama ilibadili upepo wa siasa za Zanzibar.

Katika dakika hizo nane, chama cha ACT Wazalendo kilibadilika kutoka chama cha kawaida cha kisiasa na kuwa chama kikuu cha kisiasa cha Zanzibar.

Katika kusimika hilo, Desemba 8, 2020, Maalim Seif – kwa mara ya pili katika historia ya Zanzibar, aliapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Ndoto ambayo haijatimia

ndoto

Siku moja nilishangazwa sana na maelezo ya kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa CCM Taifa aliponieleza kwamba endapo Maalim Seif angepata nafasi ya kuongoza Zanzibar kama Rais, nchi hiyo ingepiga hatua kuliko katika wakati wa kiongozi yeyote yule wa visiwa hivyo.

mAALIM

Ni bahati mbaya tu kwamba hadi leo, ndoto yake hiyo ya kuingia Ikulu ya Zanzibar kama kiongozi namba moja haijatimia.

Dunia ina historia ya viongozi wengi wazuri ambao ama ama walifanikiwa kutimiza ndoto zao baada ya muda wa miaka mingi kupita na wengine ambao bado wanakimbiza ndoto zao hizo hadi leo.

Pengine, Maalim Seif anaweza kuingia katika vitabu vya rekodi kama Rais Bora ambaye Zanzibar haikupata kuwa naye.

Labda Mwenyezi Mungu alimuumba kuja duniani si kwa sababu ya kuwa Rais – bali kwa sababu nyingine ambayo historia itakuja kutuonyesha.