Monday, March 17

Milele Zanzibar Foundation imekabidhi boti ya Kuvukia kwa wananchi wa kisiwa cha Mwambe Shamiani

NA ABDI SULEIMAN.

TAASISI ya Milele Zanzibar Foundation imekabidhi boti ya Kuvukia (Ambulace bot) yenye uwezo wakuchukua watu 20, kwa wananchi wa kisiwa cha Mwambe Shamiani Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa na thamani ya shilingi Milioni 39.8/=.

Boti hiyo imekabidhiwa kwa uongozi wa Wilaya ya Mkoani, kwa ajili ya kuwakabidhi wanajamii wa Kisiwa cha Mwambe Shamiani, hafla iliyofanyika katika bandari ya Mwambe Bwegeza Shehia ya Mwambe.

Akizungumza na wananchi na kamati maalumu ya kusimamia boti hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Issa Juma Ali aliwataka wananchi hao kutambua kuwa boti hiyo sio ya kuvulia samaki, bali inapaswa kutumika kwa kuvushia wanafunzi, wakati wakwenda na kurudi skuli, akinamama wajawaziti na wagonjwa.

Alisema kuwepo kwa boti hiyo itaweza kuwarahisishia wananchi wa mwambe Shamiani, kuondokana na usumbufu waliokuwa wakiupata, licha ya Wawekezaji kusaidia huduma za kuvusha wananchi pale weanapopatwa na tatizo.

“Sisi Serikali kwanza tunaishukuru taasisi hii ya milele, imekua mstari wambele katika kusaidia wananchi huduma mbali mbali, elimu, afya, maji na leo imeweza kutusaidia boti hii ya kuvukia hili ni jambo la faraja kwetu”alisema.

Aidha aliwataka wananchi kutambua kuwa chombo hicho hakifungamani na siasa za chama chochote, bali kimetolewa kwa ajili ya kusaidia wananchi, huku akiwasihi kutokukupeleka maji makubwa kwa kuepusha kukiharibu.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Wilaya, aliwakata wananchi kukitunza na kukithamini chombo hicho ili kiweze kudumu kwa muda mrefu na kuwasaidia, sambamba na Serikali kutokumvumilia mtu yoyote atakae weza kuiba au kuharibu vifaa vilivyomo humo.

Kwa upande wake mratib wa Milele Zanzibar Foundation Ofisi ya Pemba, Abdalla Said Abdalla alisema taasisi hiyo imeweza kutoa huduma mbali mbali katika kusaidia wananchi Vijijini Unguja na Pemba.

Alisema wananchi wa Mwambe Shamiani wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo sekta ya usafiri kutoka kisiwani kwenda ngambu ya pili, hivyo taasisi hiyo imelazimika kuwapatia boti na kuwa Kisiwa cha kwanza kupatiwa usafiri huo.

“Hichi chombo kinapakia watu wachache tu abiria 20 ikiwa watoto watano na watu wazima 15, pia kila anayepanda anatakiwa kuvaa vifaa vya uwokozi ndio malengo ya chombo”alisema.

Hata hivyo aliwataka wananchi wa kisiwa cha Mwambe Shamiani, kuhakikisha chombo hicho hawakitumii kwa shuhuli za uvuvi bali wanakitumia kwa ajili ya kuvushia wananchi tu.

Naye sheha wa shehia ya Mwambe Shamiani Safia Khamis Mgwali, akizungumza kwa niaba ya wananchi wake aliahidi kukitunza na kukithamini, pamoja na kukitumia kwa malengo yaliokusudiwa.

Alisema atahakikisha chombo hicho anakisimamia ipasavyo, licha ya kuwepo kwa kamati ndogo ilioanzishwa ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.