Monday, November 25

MHE. HEMED: SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA WAANDISHI WA HABARI NCHINI

 

Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi itaendelea kuthamini mchango mzuri unaotolewa na waandishi wa habari Zanzibar katika kuawahabarisha wananchi juu ya matukio mbali mbali yanayoendelea nchini.
Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo wakati akizungmza na Kamati maalum ya waandishi wa habari iliongozwa na viongozi kutoka taasisi tofauti ikiwemo Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar , Jumuiya ya waandishi wa habari za mazingira Zanzibar (WAHAMAZA) waliofika Afisini kwake Vuga jijini Zanzibar kwa ajili ya kujitambusha.
Amesema kutokana na mchango unaotolewa na wandishi wa habari katika kutoa taarifa zake kwa haraka imeibua shauku mara dufu kwa wananchi katika kufuatilia vyombo vya habari kwa lengo la kupata taarifa sahihi dhidi ya hatua zinazochukuliwa na serikali yao.
Akigusia suala la wafanyabishara Makamu wa Pili wa Rais amewaomba waandishi kutumia kalamu zao vizuri katika kuwaelimisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla juu ya wajibu wao na umuhimu wa  kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wanakamati  Mwenyekiti wa Kamati ya wanahabari Zanzibar Farouk Karim amemueleza Makamu wa Pili wa Rais kwamba Waandishi wa habari Zanzibar wanafurahishwa na muelekeo wa serikali ya awamu ya nane ilianza nao hasa katika muktadha mzima wa kurejesha nidhamu kwa watumishi wa serikali pamoja na watumishi katika sekta zinazojitegemea.
Pia Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kumualika Makamu wa Pili wa Rais katika kongamano la wanahabari linatarajiwa kufanyika Machi 01, mwaka ambapo Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi likijumuisha na Waheshimiwa mawaziri pamoja na makatibu wakuu.
Kwa upande wake Afisa Uhusiano kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Mussa Yussuf akitoa shukrani kwa niaba ya kamati iliofika kujitambulisha kwa Makamu wa Pili wa Rais amemuomba Mhe. Makamu wa Pili kuwahimiza maafisa habari waliopo katika taasisi nyengine za serikali kutoa taarifa kwa wananchi kwa lengo la kujenga uwelewa juu ya masula muhimu yanayotekelezwa na serikali yao.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)