Sunday, November 24

“Fanyeni kazi kwa mashirikiano ili kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020/2025”.Mhe Hemed

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikabidhi magodoro kwa wahudumu wa vituo vya Afya vilivyomo katika jimbo la Chaani vilivyotolewa kwa ushirikiano wa Viongozi wa jimbo hilo (Mbunge na Muwakilishi) (PICHA NA OMPR.)

Mjumbe wa kamati kuu ya halimashauri kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewashauri watendaji wa chama na serikali kufanya kazi kwa mashirikiano ili kusimamia vyema utekelezaji wa wa Ilani ya CCM ya 2020/2025.

Mhe. Hemed alitoa ushauri huo  katika halfa ya kukabdhi magodoro kwa vituo  vya afya vya Jimbo la Chaani, vilivyotolewa kwa ushirikiano baina ya Mbunge na Muwakilishi wa Jimbo hilo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zao walizozitoa wakati wa kampeni.

Alisema kuna kila sababu kwa viongozi hao kushirikiana kwani kufanya hivyo kutasaidia serikali kutekeleza miradi mbali mbali sambamba na utekelezaji wa ilani ya CCM na ahadi zilizotolewa wakati wa Kampeni.

Makamu wa Pili wa Rais aliwapongeza viongozi hao wa jimbo kwa ushirikiano waliounesha kwa kuwatumikia wananchi na kuanza kutimiza ahadi zao mapema na kueleza kuwa kitendo hicho kitasadia kukijengea heshima chama pamoja na kutengeneza mazingira mazuri kwa chaguzi zijazo.

Akizungumzia suala la uwajibikaji kwa watendaji wa vituo vya Afya na maeneo mengine Mhe. Hemed aliwataka viongozi wa chama kwa kushirikiana na kamati zao za ngazi ya Mkoa na Wilaya kutembelea katika vituo ili kujiridhisha juu ya huduma zinazotolewa na watendaji.

“Ni lazima chama na serikali wafanye kazi pamoja’ Alisitiza Makamu wa Pili.

Akijibu ombi la Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Mhe. Hemed alisema serikali imetoa maelekezo kwa wizara ya Afya kupeleka maombi maalum juu ya wataalamu wanaowahitaji katika sekta hiyo na serikali itatoa kibali maalum kwa ajili kufanya uwajiri.

Aidha, Mhe. Hemed alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu kunyakua dawa za serikali kitendo ambacho kinakwenda kinyume na maadili yao ya kazi jambo linarudisha nyuma jitihada za serikali katika kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Alitanabahisha kwamba serikali serikali haitomvumia mtumishi yeyote atakaebanika kufanya vitendo hivyo vya wizi wa dawa kutokana na kitendo hicho kuwanyima wananchi kupata matibabu.

“Ole wake kuanzia sasa mtumishi atakaebanika kufanya vitendo hivyo serikali itamchukulia hatua kali za kisheria” Alisema Mhe. Hemed

Akizungumzia suala la upatikaji wa dawa kwa wananchi Mhe. Alilieza serikali tayari imeshanza kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawa hivyo viongozi wa mikoa na wananchi wasiwe na hofu katika upatikanaji wake.

Akigusia sula la kesi za udhalilishaji alisema wakuu wa Mkoa lazima wafuatilie kwa karibu nyendo za masheha katika maeneo yao kwa kuwakataza kufanya suluhu juu ya kesi hizo kwani serikali chombo cha kutunga sheria kimeshapitisha sheria ya kuondoa dhamana kwa makosa hayo.

“Nakuagiza Mkuu wa Mkoa kumchukulia hatua sheha yeyote atakaekwenda kinyume na agizo hili la serikasli, suluhu hazihitajiki”

Akitoa Salumu za Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Mkoa wa Kaskazini unafanya kazi kwa mashirikiano lakini zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya Afya ikiwemo Uhaba wa vifaa tiba, Dawa pamoja na idadi ndogo ya watumishi katika Kada ya Afya.

Mhe. Ayoub akitolea mfano suala la watumishi alisema wilaya ya kaskazini “A’ inahitaji watumishi wasiopungua mia tano (500) katika kutatua changamoto ikiwemo katika sekta ya Afya kwa vituo vya Afya Kumi na Saba (17) vilivyomo katika wilaya hiyo.

Alisema katika Mkoa wa kaskazini kulikuwepo kwa changamoto ya kuhamishwa au kuhama kwa watumishi wa sekta ya Afya, lakini kwa sasa serikali ya mkoa hatomruhushu mtumishi kuondoa katika sehemu aliopangiwa endapo hakutakuwa na sababu ya msingi.

“Mhe. Makamu wa Pili nikuhakikishie kwa sasa hakuna mtumishi atakehama katika mkoa huu bila ya sababu ya msingi” Alisema Mhe. Ayoub

Vile vile, Mkuu huyo wa Mkoa alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa uongozi wa serikali ya Mkoa wa kaskazini utapeleka rasilimali ya mchanga bure katika miradi yote ile itakayoibuliwa na serikali kwa lengo la kufanikisha ukamilikaji ili itoe tija kwa wananchi.

Kwa upande wao Viongozi wa jimbo hilo Mhe. Mbunge na Muwakilishi, walisema utoaji wa Magodoro katika vituo vya Afya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, pamoja na ahadi walizozitoa wakati wakiomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo hilo.

Walieleza Magodoro hayo 65 walioyatoa yanagharimu jumla ya Millioni Kumi na Saba Laki Nane na Sabini na tano (17,875,000/) wamethibitishwa kuwa na ubora unaohitajika kwa ajili ya vituo vya Afya vitakavyokabidhiwa.

Aidha, viongozi hao wa jimbo la Chaani waliahidi kukifanyia ukarabati kituo cha Afya cha Chaani Masingini  ambacho kitagharimu jumla ya Shilingi Milioni  Mia na Ishirini na Tano (125,0000,000/),ambapo Shilingi Milioni 50 zitatoka katika mfuko wa jimbo.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya uongozi wa chama cha mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Mwenyekiti wa Mkoa Ndugu Iddi Ali Ame alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais kuwa Chama cha mapinduzi kitaendeleza ushirikiano wake na serikali kwa ngazi ya Mkoa na wilaya kwa ajili ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Pamoja na mambo mengi Mwenyekiti huyo aliema chama cha mapinduzi kinalaani vikali juu ya vitendo vya udhalilishaji vilivyoshamiri katika visiwa vya Zanzibar na kuahidi kuwa chama kinaungana pamoja na serikali katika kupiga vita jambo hilo.

Makamu wa Pili wa Rais amekabidhi magodoro hayo kwa vituo vya Afya vya jimbo hilo ikiwemo Kivunge magodoro 25, Masingini magodoro 20,kikobweni Magodoro 5, Pwani mchangani magodoro 5 na Magodoro 10 kwa ajili ya kundi maalum la chama cha mapinduzi.

 

Wachezaji wa sarakasi kutoka mkoa wa Kaskazini Unguja wakionesha umahiri wao juu ya uchezaji wa mitindo tofauti mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika hafla ya makabidhioano ya vifaa vya Afya.

Kassim Abdi

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.