Ndugu zangu na wenzangu nyote, najua shauku na hamasa zenu kwa maendeleo ya nchi yetu. Najua imani yenu kwangu, hata wale waliokuwa wakihoji juu ya uwezo wangu au kufaa kwangu kwa nafasi hii walifanya hivyo kwa nia safi na hamu ya kupata mtu atayekidhi haja. Hakuna anayeweza kukidhi vigezo wala viwango vya Maalim.
Hakuna na hatotokea. Mimi sikuwa nimeshindanishwa na yeyote bali nimetiwa katika mezani na kuonekana sio mzito zaidi, bali ninaelekea kwa yale viongozi wetu wa chama waliyoyaona yatafanana na uwezo wa kuendeleza msingi mzuri na madhubuti ambao mzee wetu Marehemu Maalim Seif kwa kushirikiana na Rais wetu Dokta Mwinyi wameujenga.
Kamwe sitojipima mezani ya Maalim daima sitotimia, bali nitajipima katika mezani ya matarajio ya watu wa Znanzibar na hatma ya nchi yao. Shauku na haki ya maendeleo. Haki ya maridhiano, utulivu na mshikamano. Haki ya kuwa pale wanapostahiki. Haki ya kuwa na fahari na nchi yao. Hayo naamini yatapatikana kwa kumsaidia Rais wetu kujenga misingi imara ya taasisi za umma.
Misingi imara ya uwajibikaji na uadilifu. Misingi imara ya haki za kijamii. Misingi imara ya Sheria na usimamizi wa sheria na misingi imara ya uchumi kwa uwekezaji wa Serikali na ushiriki wenye tija wa sekta binafsi. Zanzibar ina fursa ya kipekee kwa kutumia rasilimali watu, vipawa na uwezo wa watu wake waliopo ndani na nje. Kinachohitajika ni mashirikiano ya wote, mashirikiano ya dhati.
Sasa tunakwenda mbele kwa pamoja. Nawashukuru kwa namna ya kipekee.
Ahsanteni sana.
Othman M. Othman Shariff,
Makamu wa Kwanza Mteule wa Rais wa Zanzibar,