Monday, November 25

Ndege mzee zaidi duniani Wisdom apata kinda akiwa na miaka 70

Ndege mwenye umri mkubwa duniani amejifungua kifaranga akiwa na umri wa miaka 70.

Ndege huyo wa aina ya laysan albatross alipata kinda huyo tarehe mosi Februari katika kambi moja ya wanyama pori.

Ndege aina ya laysan albatrosses huishi kati ya miaka 12 hadi 40 .

Lakini Ndege huyo kwa jina Wisdom kwa mara ya kwanza aligunduliwa na watafiti mwaka 1956.

Babake kwa jina Akeakamai ni mshirika wake, ambaye amekuwa naye tangu 2012 , kulingana na maafisa wa shirika la wanyamapori nchini Marekani.

Inaaminika kwamba Wisdom alikuwa na washirika wengine awali ambao aliishi muda mrefu kuwaliko.

Ijapokuwa Wisdom alipata kinda wake mwezi februari , kuanguliwa kwa mtoto huyo kumeripotiwa wiki hii.

Wisdom alitaga mayai yake mnamo mwezi Novemba, liliandika shirika hilo la wanyamapori la Marekani katika taarifa yake likitangaza kupatikana kwa kinda huyo.

Muda mfupi baadaye, Wisdom alirudi baharini kutafuta chakula huku mwenzake Akeakamai akichukua kazi za kuangua mayai.

Wazazi wa Albatross hugawana majukumu ya kutaga mayai na wakati kinda anapotoka , hugawana majukumu ya kulisha.

Shirika la wanyama pori nchini Marekani USFWS linaamini kwamba amekuwa na takriban kati ya watoto 30 hadi 36 katika maisha yake yote.

Aina hiyo ya ndege hutaga yai moja kila baada ya miaka kadhaa.

Kambi ya wanyamapori ya Midway Atoll ni nyumbani kwa idadi kubwa ya kizazi cha Albatross duniani.