Monday, November 25

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amefanya Ziara Kiwanda cha Sukari Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja leo 6/3/2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akitembelea Kiwanda cha Sukari Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja akiwa katika ziara yake akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda hicho Ndg. Rahim Bhaloo (kushoto kwa Rais) akitowa maelezo ya uzalishaji wa sukari na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shabaan.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amevitaka Vikosi vya Ulinzi na Usalama kupanua wigo katika shughuli za kilimo cha miwa, ili kukiwezesha kiwanda cha Sukari Mahonda kuwa na malighafi ya kutosha.
Dk. Mwinyi amesema hayo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakati alipokitemebela Kiwanda hicho na kuangalia mchakato mzima wa uzalishaji wa sukari pamoja na kuzungumza na Uongozi,  wafanyakazi, wawakilishi wa wakulima wa nje pamoja na Wawakilishi wa Vikosi vya SMZ.
Alivitaka Vikosi vya Ulinzi na Usalama, ikiwemo Mafunzo, JKU na KVZ kupitia nguvu kazi waliyonayo, zana za kilimo pamoja na ardhi ya kutosha iliopo kuongeza juhudi na kuongeza uzalishaji wa miwa katika maeneo yao.
Alisema hali ya kilimo hicho ilivyo hivi sasa katika Vikosi hivyo  haiendani na uwezo halisi wa vikosi, hivyo akawataka kuongeza uzalishaji  kwa kigezo kuwa kutawaongezea kiwango cha  mapato.
Alieleza kuwa Serikali itazipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokikabili Kiwanda hicho, huku akiutaka uongozi wa kiwanda  kuyatatua matatizo ya wafanyakazi mapema iwezekanavyo.
Alisema pamoja na mambo mengine Serikali itaangalia bei ya sukari, pamoja na upatikanaji wa ardhi bora kwa ajili ya kilimo cha miwa sambamba na kuitaka Wizara ya Kilimo , Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuwawezesha wakulima wa kilimo cha miwa kutumia njia ya umwagiliaji ili kiwanda hicho kiweze kupata malighafi zaidi.
Alisema kilimo cha miwa kinaweza kuwa mkombozi wa maisha ya  wakulima, hivyo ni vyema Serikali ikatafuta maeneo mazuri ili yaweze kutumika kwa kilimo hicho.
“Watu kama wataweka mkazo katika kilimo cha miwa wataweza kubadili maisha yao”, alisema.
Aidha, akatoa wito  kwa wakulima wakubwa kujitokeza kuunga mkono ukulima wa kilimo cha miwa, sambamba na wakulima wadogo kuwezeshwa kwani kinaweza kubadili maisha yao.
Akigusia juu ya madai mbali mbali ya wafanyakazi wa kiwanda hicho, Rais Dk. Mwinyi alisema hapendi kusikia changamoto za wafanyakazi, ikiwemo kutokuwepo kwa mikataba, mishahara duni pamoja na kuchangia vifaa vya kazi, hivyo akaagiza kupatiwa ufumbuzi.
Nae, Waziri wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban alisema Wizara hiyo imekuwa ikifanya vikao mbali mbali kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto tofauti zinazokikabili kiwanda hicho.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mohamed Mahamoud alisema Uongozi wa Mkoa huo umeunda Kamati maalum inayolenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zilizokikabili kiwanda na kuchochea kushusha kiwango cha uzalishaji wa sukari.
Mkurugenzi wa kiwanda cha Sukari Mahonda, Rahim Bhaloo, alisema mashirikiano baina ya Wizara na Mwekezaji ndio njia pekee itakayowezesha utatuzi wa matatizo mbali mbali inayokikabili kiwanda hicho.
Aliiomba Serikali kusaidia kuwashajiisha wakulima kulima miwa katika maeneo mbali mbali nchini, ambako ardhi nzuri kwa ajili ya kilimo hicho  inapatikana katika mabonde madogo madogo.
Aidha, aliomba Serikali kupitia wataalamu wa kilimo, kuhakikisha maeneo yanayotolewa kwa kilimo cha miwa kwa ajili ya kiwanda hicho yanakuwa yale yenye rotuba na kuwezesha zao hilo kustawi vyema.
Katika hatua nyengine Mwakilishi kutoka Vikosi vya SMZ waliomba Uongozi wa kiwanda cha Sukari kuongeza kiwango cha bei ya miwa kutoka ile ya 55,000 kwa tani inatozwa tangu mradi huo ulipoanza.
Aidha, wafanyakazi wa kiwanda hicho walilamika kukosa mikataba ya Ajira, kiwango duni cha mishahara wanacholipwa na kutakiwa kununua vifaa vya kufanyia kazi, jambo lililopaswa kufanywa na Uongozi wa kiwanda pamoja na Kiwanda hicho kutumia kipindi kifupi cha uzalishaji.
Katika hafla hiyo Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda ulimkabidhi zawadi ya Mfuko wa Sukari Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Maapinduzi Dk. Ali Hussein Mwinyi, ikiwa ni hatua ya kuanza kwa  msimu mpya wa uzalishaji wa sukari
BAADHI ya Wakulima wa Miwa Mkoa wa Kaskazini Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza wakati wa ziara yake ya kutembelea Kiwanda cha Sukari Mahonda leo.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzib