Monday, November 25

Asasi za kiraia zatakiwa kushirikiana na Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokomeza Kifua Kikuu.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

ASASI za kiraia kisiwani Pemba zimetakiwa kushirikiana pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa kifua kikuu ambao unaathiri jamii siku hadi siku.

Akizungumza na wanachama kutoka asasi za kiraia pamoja na watu wa tiba asilia, katika Ukumbi wa Ofisi ya Ukimwi Machomane Chake Chake dk. Khamis Abubakar kutoka Kitengo Shirikishi Kifua kikuu, Homa ya ini, Ukimwi na Ukoma Zanzibar alisema, ushirikiano unahitajika katika kuhakikisha ugonjwa huo unamalizika.

Alisema kuwa, kifua kikuu kipo ingawa wenye dalili hawafiki kwenye vituo vya tiba, hivyo kupitia asasi za kiraia pamoja na watu wa tiba asilia, washirikiane na Serikali kuwatafuta wagonjwa hao, jambo ambalo litasaidia kuwagundua mapema na kuzuia kuambukiza wengine.

“Wagonjwa wengine wanafika hali ya kuwa wameshachelewa (hali ya dharura), jambo ambalo ni vigumu kutibika kwa haraka, hivyo tunaamini ushirikiano wenu tutawaibua wagonjwa na tutafanikiwa kwa kiasi kikubwa kuondosha ugonjwa huu”, alisema daktari huyo.

Kwa upande wake Mratibu wa Kitengo Shirikishi Kifua Kikuu, Homa ya Ini, Ukimwi na Ukoma kanda ya Pemba Hamad Omar Hamad alisema, lengo la mkutano huo ni kuweza kuibua kesi za ugonjwa wa kifua kikuu ambazo zipo mitaani, ili waweze kuwatibu wagonjwa hao.

“Watu wa tiba asilia wanapokujieni mgonjwa ana dalili za TB muelekezeni kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi, hii mutatiusaidia sana kuyaondosha maradhi haya”, alieleza mratibu huyo.

Alisema kuwa, elimu inahitajika zaidi katika kuhakikisha inawafikia wanajamii walio wengi, ili kuepusha maambukizi kwa wengine, kwani mtu mmoja mwenye TB anaweza kuambukiza watu kumi (10) hadi 20 kwa mwaka.

Aidha alisema, matumizi mabaya ya dawa za kifua kikuu yanaweza kusababisha kifua kikuu sugu, ambacho kinachukua muda mrefu kutibika kwake, hivyo atakaegundulika anatakiwa awe na msimamizi mzuri ambae atamfanya mgonjwa kuweza kutumia dawa kwa uangalifu.

Akizungumzia dalili za ugonjwa huo mratibu huyo alisema ni pamoja na kukohoa wiki mbili au zaidi, homa za mara kwa mara, kutokwa na jasho jingi kuliko kawaida hasa nyakati za usiku.

“Nyengine ni kutoka makohozi yaliyochanganyika na damu, udhaifu na uchovu pamoja na kupungua uzito, hivyo mutakapomuona mtu ana dalili hizo tunakuombeni mutuletee kwetu au mutuletee makohozi”, alisema Mratibu.

Mratibu huo aliitahadharisha jamii kuacha tabia ya kuzitumia dawa za kifua kikuu kwa kuziweka kwenye vidonda, kwani wanaweza kujisababishia matatizo mengine ikiwemo ya ngozi.

“Tuna kazi kubwa ya kubadilisha mtazamo wa wanajamii, lakini tujitahidi sana kuelimisha, tumegundua kwamba kuna baadhi ya wagonjwa hawatumii dawa na wanaziweka kwenye vidonda, hii sio sahihi kwani wanasabaisha kifua sugu”, alisema.

Nae Mkuu wa kitengo hicho Pemba Hasnuu Fakih Hassan alisema, watu wa tiba asilia wana mchango mkubwa katika kupiga vita ugonjwa wa TB, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake apambane, ili ifikapo mwaka 2035 kiwe hakipo.

“Wana asasi za kiraia muna jukumu la kutoa elimu kwa jamii na watu wa tiba asilia tunahitaji mchango wenu sana, kwa sababu wagonjwa wengi wanakuja kwenu, kama hukuwa makini unaweza kuambukizwa na ukaambukiza wengine”, alisema.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake Ahmed Issa Mohamed kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) alisema, wamefarajika sana kupata mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi katika kuhakikisha vita dhidi ya ugonjwa huo unafanikiwa.

 

Mkutano huo wa siku moja uliwashirikisha wadau wa asasi za kiraia pamoja na watu wa tiba asilia, lengo ni kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu na kuwafikisha katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi.