NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amesema Serikali ya Zanzibar ya awamu ya nane inaleta mabadiliko ya kasi kwa wanawake kushika nafasi za uongozi kwenye ngazi za maamuzi.
Aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari ikiwa ni katika shamra shamra ya maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani, ambayo huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka.
Alieleza kuwa, kila mmoja anaona nchi inavyoleta mabadiliko ya kasi kwa viongozi wanawake kuingia kwenye ngazi za maamuzi, hivyo ipo haja kwa waandishi kuelimisha zaidi jamii na Serikali, ili kuhakikisha kwamba inamuinua mwanamke.
“Tuendelee kuelimisha kwa hali ya juu ili ifike pahala tutambue uoni na mtazamo wa jamii na Serikali juu ya kumuinua mwanamke, kwani sehemu anapokuwaepo mwanamke na maendeleo yanapatikana kwa haraka”, alisema Mkuu huyo.
Aidha alieleza kuwa, zamani wanawake hawakupata fursa ya kusoma, jambo ambalo limesababisha kukosekana viongozi wanawake katika vyombo vya kutoa maamuzi.
“Hata hii leo ambapo wanawake wanashika nafasi mbali mbali za uongozi bado kuna baadhi ya wanajamii hawajajua lengo na umuhimu wa mwanamke kuwa kiongozi, hivyo ni jukumu lenu waandishi kutoa elimu kuhakikisha kila mmoja atashiriki kumpa mwanamke nafasi”, alisema.
Aidha Mkuu huyo alisema kuwa, kuwepo kwa Sheria kandamizi ilisababishwa na kukosekana kwa viongozi wanawake wakati wa kutunga Sheria, jambo ambalo ni kikwazo kwa wanawake na watoto.
Nae akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Katibu wa Klabu ya Waandishi wa habari Pemba (PPC) Ali Mbarouk Omar alisema, kukiwa na vyombo vya habari madhubuti na jamii itakuwa imara, hivyo kila mmoja ajue kwamba ana umuhimu wa kuleta mabadiliko kwenye jamii.
Alisema kuwa, ili kufikia lengo ni vyema kufanya kazi ya kupambana katika kutanua fikra za watu, kufanya hivyo watakuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa uwajibikaji katika utendaji wa kazi zenu.
Mapema akizungumza na waandishi hao Afisa Uwezeshaji wa Wanafunzi wa kike na vijana kupitia elimu kutoka UNESCO Viola Muhangi Kuhaisa alisema, elimu inahitajika zaidi katika kuhakikisha wanajamii wanapata njia bora ya kutatua changamoto zinazowakumba wanawake na watoto.
“Tunapigania haki za wanawake na watoto, ili wasipatwe na udhalilishaji wa aina yeyote na kuhakikisha kwamba wanakuwa salama dhidhi ya ukatili, ubakaji, ndoa na mimba za umri mdogo”, alifafanua.
Kwa upande wake Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Elimu, Sayansi, Utamaduni la Umows wa Mataifa ‘UNESCO’ Tirso Dos Santos alieleza kuwa, lengo la kutoa mafunzo hayo kwa waandishi ni kwamba jamii ipate kujikinga kutokana na hatari inayoweza kutokea, hivyo watoto wapewe elimu tangu wakiwa skuli.
“Tuna mradi unaitwa ‘Tuseme Sehemu Salama’ ambao utatekelezwa Wilaya ya Mkoani katika skuli 15 msingi na Sekondari, ili kuweza kuwaelewesha mapema kuhusu usawa wa kijinsia pamoja na kuondosha ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wa kike”, alieleza.
Kwa upande wa waandishi wa habari wameuomba mradi huo kuwajengea chumba maalumu wanafunzi wa kike kwa ajili ya kwenda kubadilisha taulo za kike, ili kuepuka kutokwenda skuli wakati wanapopatwa na hedhi.
Mafunzo hayo ya siku moja kwa waandishi wa habari yamefanyika katika Ukumbi wa TAMWA Mkanjuni Chake Chake.