Friday, October 18

Mdhamini awataka wazazi kuwa karibu na walimu.

 

RAIYE MKUBWA – WVUSM.

 

AFISA Mdhamini Wizara ya Vijana Utamaduni Sanaa na Michezo, Fatma Hamad Rajab, amewaomba wazazi kuwa karibu na walimu ili kuchangia maendeleo ya watoto wao.

Aliyasema hayo alipokua akizungumza katika Ugawaji wa Zawadi kwa wanafunzi, waliofanya Vizuri katika mitihani ya ndani na Mtihani wa Taifa Katika skuli ya Sekondari Chasasa wilaya ya wete Pemba.

Alisema mashirikiano yao yataweza kupelekea watoto kufanya vizuri, sambamba na kujuwa changamoto za watoto wao skulini hapo.

Aidha aliutaka uongozi wa skuli kuwa na mashirikiano ya pamoja na ofisi ya wilaya, pamoja na skuli nyengine kwa kufanya mitihani ya pamoja, ili kupima viwango vya wanafunzi wao na kupeleka mbele suala la elimu.

“Mashirikiano lazima yawepo katika elimu, walimu, wanafunzi na wazazi, lakini pia tusiisahau ofisi ya wilaya kwani itaweza kutusaidia kusonga mbele”Alieleza.

Hata hivyo aliwasihii wanafunzi wa skuli hiyo, kuwa na wigo wa maendeleo kwa kutumia wakati wao vizuri, kuongeza bidii katika kusoma ili kuweza kufikia malengo yao ya baadae na hatimae kuwa viongozi bora.

Alisema nivyema wanafunzi wakaacha kutumia mambo yamitandao, kwani huenda yakawapeleka pabaya na kuwaharibia katika maisha yao.

Katibu tawala Wilaya ya Wete Mkufu Faki Ali,aliwapongeza wanafunzi wa skuli ya sekondari Chasasa na kuwataka kuwa makini, na kutokubali kutumiwa vibaya katika kipindi hichi, huku akiwasihi kutumia muda wao kwenye kusoma na sio mambo mengine yasio kuwa ya elimu.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Mwanafunzi Zubeda Bakar Hemed, aliwataka wasikate tamaa wanapata alama ndogo kwenye mitihani, kwani kufeli mara moja ni njia moja kwa wao kusonga mbele, wanachotakiwa ni kujitahidi ili kuhakikisha wanafanikiwa katika malengo yao.

Zubeda ni Mwanafunzi alieitangaza Zanzibar kwa kupata nafasi ya Sita kwa Tanzania nzima, na nafasi ya pili kwa Zanzibar katika mitihani ya taifa ya kidato cha sita iliyofanyika Juni mwaka huu.