RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,kuziimarisha Taasisi zake ipasavyo hasa ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo ndio uti wa mgogo wa uchumi wa Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo, ikiwa ni mkutano kwa ajili ya kuripoti utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha.
Alieleza kwamba Wizara hiyo inapaswa kuchukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha inatekeleza vyema majukumu yake kutokana na Taasisi zake kutegemewa kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa bado inaonekana hatua inayotakiwa haijafikiwa ikiwa ni pamoja na kufanywa mabadiliko katika kuhakikisha mafanikio makubwa yanapatikana katika Taasisi za Wizara hiyo na zile zisizo na tija kuondolewa.
Aliongeza kuwa Wizara hiyo ina kazi kubwa zikiwemo zile za kushughulikia barabara, viwanja vya ndege, bandari pamoja na mawasiliano hivyo ni vyema ikajitathmini ili kuweza kujua majukumu hayo yanatekelezwa vipi.
Aidha, alisisitiza haja kwa Wakala wa Barabara kutofanya kazi ambazo hawaziwezi ikiwemo ujenzi wa barabara na badala yake wakajishughulisha zaidi na kuziba viraka na barabara kubwa zipewe Kampuni zenye uwezo.
Rais Dk. Mwinyi alisikitishwa na taarifa ya kuharibika kwa barabara ya Ole-Kengeja huko kisiwani Pemba ambayo imegundulika kuwa na kiwango kisichoridhisha huku akiitaka Wizara hiyo husika kuchukua hatua.
Dk. Mwinyi akaeleza kutoridhishwa na utendaji pamoja na ukusanyaji wa mapato katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume Zanzibar na kuitaka Wizara hiyo kuhakikisha inaweka miundombinu rafiki ya ukusanyaji wa kodi.
Kwa upande wa bandari, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba bado kuna uvujaji wa mapato kwa meli zinazotoa huduma za ndani na kuitaka Wizara hiyo kulifanyia kazi suala hilo huku akisisitiza kuhakikisha fedha zote za Serikali zinakusanywa kwa njia ya elektroniki.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi huo kukaa pamoja na uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ili kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na kuitaka Benki hiyo kufanya shughuli zake muda wote kama ilivyo kwa Bandari.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa watendaji wa Mawizara kuwa na mabadiliko ya utendaji huku akieleza iwapo kama kuna haja ya kuwepo kwa utitiri wa Bodi zinazosimamia utendaji wa kazi kwa Taasisi za Wizara hiyo.
Nae Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Rahma Kassim Ali alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa umahiri wake wa kusimamia utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Nane ambapo wka kipindi kifupi Zanzibar inashuhudia mabadiliko makubwa ya maendeleo na hasa katika suala zima la usimamizi wa mapato ya Serikali.
Halikadhalika, usimamizi wa Miradi ya maendeleo, kupiga vita uzembe pamoja na ubadhirifu wa mali za umma sanjari na miongozo anayowapa muda wote ambayo imesaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Alisema kuwa Wizara hiyo imepewa jukumu la kusimamia sekta kuu mbili ambazo ni sekta ya usafirishaji inayojumuisha huduma na miundombinu ya usafiri na sekta ya mawasiliano inayojumuisha huduma na miundombinu ya mawasiliano.
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alisisitiza haja ya kuwepo umakini katika miradi inayoendeshwa na Wizara hiyo ikiwemo ile ya barabara.
Mapema Katibu Mkuu, Wizara hiyo Amour Hamil Bakari alieleza utekelezaji wa maagizo ya Rais ambapo katika maelezo yake alieleza kuhusu baadhi ya miradi kuonekana kuwa na kasoro ikiwemo mradi wa Barabara ya Ole hadi Kengeja.
Alisema kuwa hatua za kumuandikia Afisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa ajili ya ukaguzi wa ubora na fedha imeshachukuliwa.
Pia, Katibu Mkuu huyo alieleza hatua zilizochukuliwa na Wizara kwa kuunda kikosi kazi kilichojumuisha Wahandisi na Wataalamu wa ICT kwa ajili ya usimamizi wa karibu katika utekelezaji wa Mradi wa jengo la Abiria (Terminal 3).
Alieleza kwamba kwa upande wa Shirika la Bandari, limeweza kutoa huduma za Makontena kwa masaa 24 ambapo hivi sasa linahudumia Makontena 10-11 kwa saa badala ya Makontena 5-7 hapo awali ambapo pia, alieleza jinsi Wizara hiyo ilivyotekeleza maagizo mengineyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar