NA GASPARY CHARLES-TAMWA PEMBA.
MASHEHA, wanasiasa, wanafunzi na wadau mbalimbali wa amani katika jamii wamekumbushwa kuendelea kuhamasisha amani na mshikamano ili kusaidia kufanikisha malengo ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dk, Hussein Ali Mwinyi wa kujenga Zanzibar ya uchumi wa buluu
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa amani ulioandaliwa na taasisi ya Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF) kwa kuwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, meneja miradi kutoka taasisi hiyo Almas Mohamed alisema mkutano huo umekuja kwa lengo la kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa amani hasa kuelekea Zanzibar ya Uchumi wa buluu.
Alieleza ili taifa liweze kupiga hatua katika nyanja mbalimbali kunahitajika kuwepo na mshikamano baina ya wananchi na viongozi na wadau wengine katika masuala ya uzalishaji pasipo kujali tofauti zao kisiasa, kidini na kimitazamo.
“Ni lazima kuwe na misingi ya amani ambayo inajengwa kila uchwao, na sisi ZYF tumekuwa tunafanya shughuli hizi kwa miaka kadhaa sasa, na tumefanya hili leo ili kuona kwamba kupitia nafasi zao wanakuwa ni chachu ya ujenzi wa amani,”alisema.
Hata hivyo pia aliitaka jamii kulibeba neno la amani na kulipeleka kwa jamii ili kuona kila mtu anaweza kushiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa pasipo kuwa na kikwanzo chochote.
Mapema mwezeshaji wa mkutano huo, Moh’d Hafidh alisema suala la utatuzi wa migogoro katika jamii huhitaji busara kwa kila mtu katika maamuzi anayoyafanya kwa kuzingatia masilahi ya wengi.
“Katika makosa ambayo watu wanayafanya ni pale wanapochukuwa maamuzi au hatua katika kipindi ambacho hisia za watu zipo katika jambo fulani hasa kipindi cha uchaguzi kwani maamuzi mengi yanayofanywa kipindi hicho wananchi huyahusisha na uchaguzi,ni lazima watu wafanye maamuzi kwa kutumia busara zaidi,” alisema.
Aidha Hafidh aliitaka jamii kujenga utaratibu wa kuwa na ustahimilivu katika uchukuaji wa maamuzi ili kuepukana na uchukuaji wa maamuzi mabaya ambayo yanalenga kuchochea vurugu katika jamii.
“Tunatakiwa tuwe na akili za kuchambua badala ya kuwa na macho ya kuangalia tu, ikiwa kila mtu atajitahidi kuwajibika katika hilo hakuwezi kutokea mifarakano ya aina yoyote,” alisema.
Salama Said Mwinyi, mshiriki wa mkutano huo alishukuru kutolewa kwa taaluma hiyo kwani inalenga kubadili tabia za wananchi katika kukabiliana na migogoro.
Mkutano huo uliowashirikisha wadau wa amani kutoka makundi tofauti wakiwemo masheha, wanafunzi, watendaji wa serikali na viongozi wa vyama vya siasa kwa kuandaliwa na Zanzibar Youth Forum (ZYF) umefadhiliwa na The Foundation for Civil Society (FCS).