NA IS-HAKA OMAR ,PEMBA.
MGOMBEA Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Jimbo la Pandani Mohamed Juma Ali ,amesema ana nia ya dhati ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa vijiji vya Jimbo hilo.
Kauli hiyo ameitoa katika mwendelezo wa ziara Maalum ya kutembelea Wananchi hao katika makaazi yao kwa lengo la kuomba kura zao jimboni humo.
Alisema kwamba Jimbo hilo linahitaji mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yatakayofanywa na kiongozi makini,mchapa kazi na mwenye dhamira ya kutatua kero za Wananchi anayetokana na Chama Cha Mapinduzi.
Katika Maelezo yake Mgombea huyo Mohamed, alieleza kwamba kwa miaka mingi Jimbo hilo limekosa maendeleo kutokana na kuongozwa na viongozi waliojali maslahi binafsi badala ya kuwatumikia Wananchi.
” Wananchi nakuombeni mniamini na kunipa ridhaa ya kukutumikieni,nitatumia uwezo wangu wote kuhakikisha natatua changamoto mbalimbali zilizopo jimboni kwetu ni nyingi lakini tutazitatua hatua kwa hatua.”aliwaomba Wananchi hao Mgombea huyo.
Alieleza kwamba endapo atapewa ridhaa hiyo atakuwa kiunganishi na kiongozi mtendaji anayetatua changamoto kwa vitendo.
Mohamed,alisema baada ya kupewa dhamana hiyo atawatumikia wananchi wote bila ya kujali Itikadi zao za kisiasa kwani suala la maendeleo linawahusu Wananchi wote.
Vipaumbele vya Mgombea huyo
Alisema katika mikakati ya kukuza na kuleta maendeleo ya Jimbo hilo amepanga amepanga vipaumbe vyake atakavyotekeleza mara tu baada ya kuingia katika Baraza la Wawakilishi.
ELIMU
Katika sekta ya elimu mgombea huyo alisema atahakikisha anawajengea uwezo vijana wa Jimbo lake kwa kuwasomesha elimu ya amali (ufundi) ili kupata wataalam wa fani mbalimbali na wenye uwezo wa kujiajiri wenyewe.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano ya mwanzo atahakikisha anayenja shule za msingi na Sekondari katika maeneo ambayo huduma za shule wanazifuata mbali.
Pamoja na hayo alisema vijana wote waliohitimu elimu za vyuo
vikuu ndani ya Jimbo hilo wenye sifa ya kuajiriwa atahakikisha wanapata fursa hiyo kwa mujibu wa fani zao.
AFYA
Alisema kila mwananchi anahitaji huduma bora za afya ili kufanya kazi zao zao za kujitafutia kipato cha kujikimu katika maisha yao ya kila siku.
Alisema ataishauri atashirikiana na Serikali kuimarisha huduma za afya ya Akina Mama na Watoto kwa kuongeza vituo vya Afya vyenye vifaa tiba vya kisasa ili kupunguza masafa ya kufuata huduma hizo mbali.
Alisema atasaidia kupatikana kwa vifaa tiba katika vituo vya Afya ambavyo vipo katika jimbo na Wilaya ya Wete ili Wananchi wapate huduma hiyo.
MIUNDO MBINU
Alisema kwa upande wa miundombinu ya barabara atakuwa kuwa mstari wa mbele kuishawishi Serikali kufanya matengenezo ya barabara za ndani.
UMEME
Kwa upande wa nishati ya umeme alihadi kuwa ataishawishi Serikali kufikisha huduma hizo katika maeneo mbalimbali yenye ukosefu wa huduma hiyo.
MAJI SAFI
Alisema kwamba kwa upande wa huduma ya maji safi na salama atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Wananchi wote wanapata maji.
UCHUMI WA BULUU
Alieleza kwamba katika kutekeleza kwa vitendo falsafa ya Uchumi mpya wa buluu ambao unategemea mazao ya Baharini kwa kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na fursa hiyo.
UJASIRIAMALI
Katika sekta ya ujasiriamali atahakikisha vijana na wanawake wananufaika na fursa ya ujasiriamali kwa kuwatafutia makampuni makubwa na miradi mikubwa ya maendeleo ili wapewe mafunzo na kufanya ujasiriamali wenye tija.
SERIKALI YA SUK
Kupitia ziara yake hiyo ambayo ni miongoni mwa mfumo mpya wa kampeni za kisayansi zinazofanywa na CCM za kuwafikia Wananchi katika maeneo yao kuomba kura,alisema ataendeleza maridhiano ya kisiasa licha ya kuwepo kwa tofauti za kiitikadi lakini Wananchi wote atahakikisha wanashirikiana katika mipango yaaendeleo ya Jimbo hilo.
Alisema viongozi wakuu wa Serikali chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi , ameasisi maridhiano kwa lengo la kuweka umoja na kuondosha chuki na visasi hivyo na yeye akiwa ni miongoni mwa viongozi atafuata nyayo hizo kwa maslahi ya Wananchi wa Pandani.
SERA NA MUELEKEO
Alieleza kwamba CCM tayari imejipambanua na kueleza kwa uwazi kuwa itafanya siasa za kistaarabu huku ikielekeza nguvu zake kumdani na kumuombea kura mgombea wake kwa kueleza sera na muelekeo wake sambamba na kueleza mambo ya maendeleo yaliyotekelezwa na yanayotarajiwa kutekelezwa.
ILANI YA CCM YA MWAKA 2020/2025
Mgombea huyo aliwaeleza Wananchi hao kwamba Utekelezaji wa Ilani ndio uti wa mgongo wa vipaumbele vyake kwani tayari kitabu hicho kimetoa muongozo wa kutatua changamoto za Wananchi.
Alieleza kuwa baada ya kukabidhiwa rasmi Ilani ya Uchaguzi katika ufunguzi wa Kampeni, kazi iliyobaki ni kupanga mpango kazi wa namna ya kuitekeleza kwa kwenda katika maeneo yote ya jimbo kuratibu kero na kuzitafutia ufumbuzi.
WANANCHI
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wananchi wa Jimbo hilo katika shehia ya Pandani walizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na kukosekana kwa huduma ya umeme kwa baadhi ya maeneo ya Jimbo hilo.
Mkaazi wa shehia hiyo Fatma Mohamed Ahmad, alisema akina mama katika Jimbo hilo hawana vikundi vya ujasiriamali kutokana na ukosefu wa mitaji ya kufanya shughuli za ujasiliama katika maeneo hayo.
Naye Mjaka Masoud Hijja mkaazi wa shehia ya Pembeni ,alimuomba Mwakilishi huyo endapo akichaguliwa kuwa kiongozi wa Jimbo hilo atekeleze miradi ya ujenzi wa sikuli za kisasa,vituo vya afya na matengenezo ya barabara za ndani zinazotumiwa na Wananchi kwenda mashambani kwa ajili ya kilimo na kusafirisha mazao.
Naye Abubakar Hamad Mussa mkaazi wa Shenge Juu, alimuomba mgombea huyo endapo atachaguliwa asimamie kwa vitendo dhana ya maridhiano ndani ya Jimbo hilo wa kuhakikisha Wananchi wanashirikiana katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Tunasomesha vijana wetu kwa gharama kubwa lakini wakisha hitimu hawapati ajira na kupelekea familia kuishi kwa unyonge kwa kukosa usaidizi, tunaomba ukiwa mwakilishi suala hili ulitafutie ufumbuzi wa kudumu”.alisema Mussa.
Akizungumza kwa niaba ya vijana wa shehia hiyo Kombo Farid, alimweleza mgombea huyo kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa vifaa vya michezo hali inayokwamisha ukuaji wa kiwango cha soka na kwamba kupitia michezo wanapata kujiajiri wenyewe.
Uchaguzi huo mdogo wa Jimbo hilo unatokana na kufariki kwa aliyekuwa Mgombea Mteule wa Jimbo hilo marehemu Abubakar Khamis Bakar, ambapo uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Machi 28, 2021.