NA MARYAM SALUM, PEMBA.
MTOTO wa miezi saba aliyekosa kunyonya maziwa ya mama yake kwa muda wa wiki mbili, mahakama ya Mkoa Chake chini ya hakimu Luciano Makoye Nyengo, imefanikiwa kumrejesha mtoto huyo kwa mama yake, ili aweze kupata haki yake hiyo.
Mahakama iliesema kuwa chanzo cha mtoto huyo kukosa haki yake hiyo, ni baada ya baba mzazi wa mtoto huyo kuamua kumchukuwa kwa muda wa wiki mbili na kwenda kuishi nae kwenye familia yake.
Mahakama hiyo ilisema kuwa ilipokea ombi hilo kutoka kwa mama mzazi wa mtoto huyo, Zulfa Hassan Ussi mwenye miaka 21, mkaazi wa Machomane, na kudai mahakama hapo kuwa mtoto wake wa miezi saba amechukuliwa na mumewake na kuishi nae katika sehemu nyengine.
“Muheshimiwa nimekuja katika mahakama yako kuleta ombi langu mtoto wangu wa miezi saba amechukuliwa na baba yake mzazi na kwenda kuishi naye kwenye familia yake”, alidai.
Alidai kuwa mahakama ndio itamsaidia kupewa mtoto wangu, aweze kubaki na mimi kupata haki yake ya kunyonya, kwani huko aliko hapati kunyonya, anateseka yeye na mimi kwani maziwa yangu yamevimba na kuniuma.
Alidai kuwa mumewake alimchukuwa mtoto na kuishi nae bila kupata kunyonya kwa siku kadhaa, jambo ambalo linamfanya mtoto wake kukosa haki yake na pia kumuhatarishia maisha yake.
Baada ya ombi la upande wa malalamikaji, hakimu huyo alikubali ombi hilo, na ndipo alipomtaka malalamikiwa amabye ni baba mzazi Said Seif Abdalla, akabidhi mahakama mtoto huyo na mahakama iweze kumkabidhi mama mzazi mtoto wake.
Hakimu huyo alisema kuwa ombi la muombaji likiwa limewasilishwa kwa hati ya dharura, mahakama baada ya kupokea ombi hilo, pande zote ziliweza kupatikana na kusikilizwa.
Katika kusikilizwa kwa ombi hilo, muombaji ambaye ni mama mzazi wa mtoto , pamoja na sababu zilizomo ndani ya hati ya kiapo, aliiambia mahakama kuwa baba mzazi alimchukuwa mtoto kwa lengo baya.
Hata hivyo kwa upande wa muombewa ambaye ni baba mzazi wa mtoto, aliiambia mahakama kuwa ni kweli mtoto anaumri wa miezi saba, na kumchukua kwake kumesababishwa na mama mzazi mwenyewe.
“Tokea kumchukuwa mwanagu Arshad Said Seif, ni wiki mbili sasa kutoka kwa mama yake, ambaye ni mke wangu, na sababu zilizonifanya nimchukue mtoto akiwa bado na umri mdogo, mama mzazi anazijua”, alidai.
Shauri hilo limeahirishwa mahaamani hapo, na kupangiwa tarehe nyengine, ambapo hakimu huyo ametaka lirudi tena mahakamani hapo novemba 2, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.