Monday, November 25

Ushirikina chanzo cha wanawake kutogombea nafasi za uongozi.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

Waweza kumbwa na tatizo kubwa, na kukata tamaa ya jambo unalotaka kulifanya.

Changamoto nyengine ni za kawaida tu ambazo unaweza kukabiliana nazo kwa kadiri alivyokuwezesha Mungu, ingawa nyengine ni vigumu kukabiliana nazo.

Kila mmoja, hukumbwa na changamoto katika eneo lake la kazi, iwe ni fundi umeme, dereva, mwandishi wa habari, kiongozi, ama mwengine aliyeko ofisini.

Pamoja na kuwa Katiba, Sheria na Mikataba ya kikanda na Kimataifa kumpa mtu haki zake za msingi, lakini kuna baadhi ya watu hutumia nguvu kuzuia haki za wengine.

Wapo wanaouzia kwa kuzipinda sheria, rushwa au hata wengine wamekuwa wakitumia nguvu za ushirikina ambazo Serikali wakati mwengine hazikubaliwi.

Na hilo hutendeka maeneo mengi ambayo watu hupigania haki zao, ikiwa ni pamoja na majimboni ambako baadhi ya wanachama hupigania kupata nafasi za uongozi.

Jambo hilo linawakwaza sana wanawake wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi, kutokana na kile wanachodai kuwa, wanaogopa kufanyiwa ushirikina.

Mwananchi mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe mkaazi wa shehia ya Kiuyu Minungwini anasema, hatojaribu kugombea nafasi hata ya udiwani, kwani anaogopa kufanyiwa vitimbi vya kishirikina.

Mwanamama huyo anasema, hataki nafasi hata moja ya kuongoza na anahiari aishi maisha magumu, kuliko kuingia katika uongozi ambao una vikwazo vinavyoweza kukuweka pabaya.

“Pamoja na mikutano hii tunayofanyiwa katika shehia zetu kwa lengo la kutushajihisha, lakini mimi sipo tayari kugombea kwa sababu watu wanatupiana ndumba (ushirikina)”, anaeleza.

Anafahamisha kuwa, hayo ndo yanayowaumiza na kushindwa kugombea nafasi za uongozi, kwani hakuna kitu kibaya kama pigo la siri, maana hajui anaekupiga wala anaekuumiza.

“Sikufichi mwandishi, licha ya kuwa sitaki kugombea, lakini hata ile nafasi ya usheha siitaki pamoja na kuwa ni ya kuteuliwa na hali hii itazidi kuturudisha nyuma sisi wanawake”, anaeleza.

Dada mmoja mkaazi wa Madenjani Wilaya ya Wete ambae pia hakutaka jina lake litajwe anahadithia, katika jimbo lao kuna mgombea mmoja alimwambia mwenzake hawezi kulipata jimbo hilo na akijaribu atakiona cha moto.

“Kwa kweli hali kama hizi zinarudisha nyuma jitihada za kugombea nafasi za uongozi hasa kwetu wanawake kwa tulivyo waoga, maana usisikie la kuambiwa roho tamu wee”, anafafanua.

Anaeleza kuwa, wanawake wa sasa wana hamu ya kuwa viongozi lakini wanakwama hapo, kwani ni waoga sana kwenye mambo ya ushirikina.

“Mwanamke haogopi kupambana na mwanamme kugombea uongozi, wala haogopi kukosa, kwani ule ni ushindani kukosa na kupata ni jambo la kawaida, lakini kibaya zaidi ni ule ushirikina ndio”, anasema.

Mayasa Ali Hamad wa Jimbo la Mtambwe anasema, mtu anaogopa kuwekwa kitandani kwa maradhi anayopewa na sio kwamba hawajiamini kama baadhi ya watu wanavyodai.

“Kwa kweli nafasi za uongozi ni ngumu sana kwa sababu mtu anaweza kumuua mwenzake hivi hivi wala asiwe na wasi wasi, halafu mtu huyo anakuja na pesa eti anasaidia masikini, mayatima au anajenga msikiti, huu ni mtihani”, anaeleza.

Mama mmoja ambae hakutaka jina lake litajwe kutoka Jimbo la Konde anasema, ushirikina sana wanaufanya wanaume kunatokana na kuona kwamba wanawake sasa wamechangamka wanataka kuchukua uongozi.

“Utasikia mtu anakwambia tangu lini mwanamke kuwa kiongozi, hemu tokeni hapa, na wakiona mwanamke ameshikilia msimamo wake ndio hatimae wanafanya ushirikina ilimuradi asiingie kugombea”, anasema.

Ali Salum Juma kutoka jimbo la Wete anasema, ushirikina aghalabu hufanywa takribani na watu wote wanaogombea jambo na sio kwa wanaume tu kama inavyoonekana.

“Unajua ukiwa kiongozi ikiwa ni mwanamke au mwanamme sio rahisi kutaka kuiachia ile nafasi kwa sababu ya maslahi yaliyopo pale, hivyo inakuwa ni vigumu na ndio maana wanafanya ushirikina”, anaelezea.

Anasema, kwa vile wanaume ndio ambao walikuwa wanashika nafasi za uongozi kwa muda mrefu, ndio maana inaonekana wao wanawafanyia ushikirina wanawake, lakini ifahamike kwamba hata uyo mwanamke kama alikuwa kiongozi anaweza kufanya suala hilo.

“Hiyo ni tabia ya mtu tu na sio jinsia fulani, hivyo pamoja na changamoto zilizopo wanawake wasirudi nyuma, kwani kutafuta uongozi ni mapambano”, anafafanua.

Shaame Hassan Sheha kutoka Jimbo la Mgogoni anasema, masuala ya uongozi yana mtihani wake, si kwa wanaume wala kwa wanawake, kwani kitu chochote chenye maslahi hakikosi fitina ndani yake.

“Unaweza kusema umefanyiwa ubaya na mgombea mwenzako, kumbe kuna jamaa yako, au jirani, ama ndugu wa karibu hawataki lile jambo upate kwa sababu utanufaika, hivyo mpigwa na wengi hajui amuumizae”, anafahamisha.

Anawataka wanawake wenye nia ya kuingia katika uongozi wasivunjike moyo, kwani ni jumla ya changamoto unazopitia katika kutafuta riziki na hakuna mafanikio yanayokuja kirahisi rahisi bila ya vikwazo.

Dada mmoja ambae aligombea Jimbo la Tumbe anasema kuwa, uwe na moyo kweli kugombea nafasi za uongozi, kwani wagombea wenzako wanaweza kukutoa roho bila ya kujali hasa wakishaona una muelekeo wa kufanikiwa.

“Mimi na mwenzangu mwanamme tulikuwa tunachuwana, basi kilichofanyika pale kura ya mwisho ambayo ilikuwa ni ya kwangu, Katibu alinipitishia akaniambia kura yako hii, kilichonishangaza akampa yule mwanaume”, anahadithia.

Pale alipigwa na butwaa pamoja na wale wapiga kura wengine mpaka walikuja kuzinduka siku tatu baadae kwamba kura yake alipewa mwenzake ambae ni mwanaume.

“Alinionesha ili nijue tu kuwa ni yangu ile kura, halafu akampa yule mwanaume lakini kilichonishangaza mimi na wengine pale, tulikuwa kama tuliozibwa midomo, hakuna alitamka kitu”, anaelezea.

“Siku ya tatu tulianza kuzinduka na wengine wakaanza kunipigia simu na kuniuliza kwa nini ile kura yako hukupewa na sababu gani zilizotufanya tusiitetee ile kura yako pale?”, waliulizana wenyewe kwa wenyewe.

Dada huyo anasema, kilichomsikitisha ni kuona kwamba alimpokonya kura yake na kumpa mwengine ni Katibu ambae anaaminika kichama, hivyo lilimuuma sana jambo hilo.

Anasema, pale alipata nafasi ya pili ingawa hakukata tamaa kutokana na kuwa yanakopelekwa majina hawamuangalii mtu bali wanaangalia CV ya mtu mwenyewe.

“Yule kijana alihisi jina litarudi la kwangu, hivyo alikwenda kunifanyia ushirikina, niliumwa sana mpaka ikawa siwezi kutembea, nilipelekwa hospitali lakini maradhi hayakuonekana”, anahadithia dada huyo.

Anaeleza kuwa, alifanyiwa dawa lakini hakupata ahuweni hata kidogo ingawa yaliporudi majibu na akawa yeye ndie aliesimamishwa kugombea ndipo akaanza kupona kidogo kidogo.

“Ingawa sijapona moja kwa moja, lakini hali yangu sio nzuri hata kidogo, kutembea masafa marefu sijaweza, ila kwa hali hii iliyonikuta sifikirii kama nitagombea tena katika maisha yangu”, anaeleza.

Mtu wa karibu wa dada huyo ambae na yeye alikuwa ni mpiga kura siku hiyo anasema, kitendo alichofanyiwa shoga yake huyo sio cha kiuungwana, kwani walitaka kumtoa roho.

“Bora tu wangechukua hivi hivi ingetosha kuliko kumtia maradhi, mpaka leo hajawa, kwa kweli mtihani maana siku ile tulifanywa kama mazuzu vile, mwenzetu anapokonywa kura sisi hatukuweza kumtetea”, anahadithia.

Tatu Abdalla Mselem kutoka Jumuiya ya TUJIPE anasema, katika vyama hakuna utaratibu mzuri wa kuonesha kuwa wanawataka wanawake wagombee nafasi za uongozi na ndio maana hawaweki mikakati ya kuzingatia jinsia.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘CHADEMA’ mkoa wa Kusini Pemba, Hafidh Abdi Said, anasema sio rahisi kwa mwanamke kupata nafasi kubwa, kwani inakuwa tayari zimeshashikwa na watu, hivyo ni vigumu kuziacha.

“Ule ni ushindani, alietangulia huwa na nguvu zaidi kuliko anaekuja leo, yule mpya inakuwa ni vigumu kuipata nafasi ile, lakini wasivunjike moyo wachukue fomu na kugombea”, anaeleza.

Mbunge wa CCM mstaafu wa lililokuwa Jimbo la Vitongoji na sasa Wawi Omar Mjaka Ali anasema bado wanawake wana hofu ya kuingia kwenye uongozi kutokana na kuwa hawakujekwa mapema.

“Changamoto zinakuwepo popote pale, kitu cha msingi unatakiwa usikate tama, hivyo kupitia elimu wanazopewa sasa wajiamini tu hakuna sababu nyengine ya kuwakwamisha”, anafahamisha.

Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Chake Chake Pemba Yussuf Abdalla Ramadhan anasema, unapotafuta riziki lazima ukumbane na matatizo, hivyo wasiwe waoga na waamini kwamba kila kitu kinapangwa na Allah Subuhanahu Wataala.

“Katika dini ya kiislamu mwanamke anayo nafasi ya kuwa uongozi, lakini hasa katika nafasi za kawaida, ila sio kwa nafasi za juu kama Waziri, Rais, hivyo wasiwe woga kuingia majimboni”, anafahamisha.

“Bibilia haijakataza mwanamke asiwe kiongozi, kwa hiyo vikwazo vinavyowakumba viwe ni fursa na kusonga mbele kuusaka uuongozi”, anaeleza Isack Maganzo Nzilamoshi ambae ni Kiongozi wa Kanisa la RGS Makangale Wilaya ya Micheweni.

TAMWA

Fat-hiya Mussa Said ambae ni Mratibu wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba, anawataka wanawake wasikate tamaa kwani uongozi ni haki ya kila mwananchi kisheria na kikatiba.

TAMWA kupitia mradi wake wa kuwahamasisha wanawake kuingia majimboni kugombea nafasi za uongozi, chini ya ufadhili wa Shirika linaloshughulikia masuala ya wanawake la Umoja wa Mataifa (UN WOMEN) inaendelea kutoa elimu kwa jamii ikishirikiana na Timu maalumu ya wanaume Mawakala wa mabadiliko.