SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeweka utaratibu mpya wa uuzaji wa zao la karafuu ambapo sasa wakulima watalipwa kuendana na bei ya soko la nje badala ya ile inayopangwa na serikali bila kuzingatia thamani sokoni.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda wa Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema uamuzi huo umezingatia hali ya sasa ya kiuchumi duniani kote na dhamira ya serikali kuhakikisha inabaki kusaidia ukuaji na uboreshaji wa sekta nzima ya zao hilo badala ya bei peke yake.
“Katika msimu huu, serikali imeamua kwamba itakuwa ikinunua karafuu kutoka kwa wakulima kwa bei ya soko. Utaratibu wa nyuma ulikuwa ni kwa serikali kuongeza kati ya shilingi 4,000 hadi shilingi 4,500 kwa kilo moja kutoka katika bei ya soko lakini sasa soko ndilo litaamua bei.
“Kwa mfano, bei ya soko kwa karafuu ya daraja la kwanza kwa sasa ni shilingi 10,350 kwa kilo moja lakini mkulima alikuwa akilipwa shilingi 14,000. Kwa hiyo, badala ya kumlipa mkulima shilingi 14,000 kwa kilo, sasa mkulima atapata asilimia 80 ya bei iliyoko sokoni.
“Maana ya hatua hii ni kwamba bei ya karafuu sasa itakuwa ikipanda na kushuka kulingana na hali ya soko badala ya kubakia katika bei moja ambayo imewekwa na serikali. Ahadi ya serikali yenu kwenu ni kuwa itahakikisha inatafuta masoko zaidi ya karafuu duniani ili karafuu zote zinazozalishwa Zanzibar ziweze kupata masoko ya uhakika na pia kwa bei nzuri,” alisema waziri huyo.
Waziri Shaaban alisisitiza kwamba katika miaka ijayo wakati hali ya uchumi itakapokuwa imetengemaa, serikali inaweza kurejea katika utaratibu ulizoeleka wa kufidia bei na akatumia nafasi hiyo kuwataka wakulima wa karafuu kuzidisha juhudi katika ubora wa karafuu wanayolima kwa sababu jambo hilo pekee ndilo litaongeza mahitaji ya wateja sokoni na bei nzuri.
Kiongozi huyo huyo ambaye ni mmoja wa mawaziri wawili kutoka Chama cha ACT Wazalendo walio katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, alisema uamuzi huo haukuwa rahisi lakini hali ya sasa ya uchumi duniani iliyovurugwa na ugonjwa wa Corona unazilazimisha serikali kuchukua maamuzi magumu na yanayozingatia hali halisi.
Alisema katika utaratibu uliokuwa ukitumika awali, serikali imekuwa inawafidia wakulima wa zao hilo kwa kubeba mzigo wa gharama ambapo fidia hiyo ni shilingi 4000 hadi 4500 kwa kilo moja ambayo ni sawa na shilingi bilioni nne hadi bilioni 4.5 kwa tani moja – kiasi ambacho ni kikubwa kwa mazingira ya kiuchumi ya wakati huu.
Waziri huyo alisema SMZ imechukua uamuzi huo mgumu kwa lengo la kuhakikisha yenyewe inajikita katika ujenzi wa miundombinu ya zao hilo ikiwamo; mikopo kwa wakulima, utoaji wa miche ya karafuu bila ya malipo, ujenzi na ukarabati wa vituo vya ununuzi, huduma ya bima kwa wanaopata ajali wakati wa uchumaji karafuu, , ujenzi wa barabara maeneo yanayozalisha karafuu kwa wingi, elimu kwa wakulima na mengineyo.
Waziri Shaaban alitoa taarifa pia kwamba kwa sasa soko la karafuu limezalisha kiasi kikubwa kuliko mahitaji ya wateja wake. Alisema mahitaji ya karafuu sokoni kwa kipindi cha 2018/2019 na 2019/2020 yamepungua kutoka wastani wa tani 120,000 hadi tani 80,000 kwa mwaka ambapo uzalishaji katika nchi wazalishaji wa karafuu umekuwa ukiongezeka na kufikia tani 130,000 kwa mwaka 2019/2020
Imetolewa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar