MWENYEKITI wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kusini Pemba Yussuf Ali Juma, amewataka wananchi na wananchama wa CCM Kisiwani Pemba, kutokujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 27 badala yake kubaki majumbani kwa siku hiyo.
Alisema siku ya kupiga kura kwa wananchi wa Zanzibar ni Oktoba 28 ambayo imetangazwa kihalali na tume ya uchaguzi Zanzibar, kwani siku ya Oktoba 27 ni siku ya watu maalumu.
Mwenyekiti huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akiwanadi wagombea wa CCM jimbo la Wawi, Mbunge, Mwakilishi na Udiwani katika mkutano wakufunga kampeni za jimbo hilo uliofanyika skuli ya Maandalizi Machomanne Chake Chake.
Aidha aliwasihi wananchi kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kwenda kupiga kusa Oktoba 28 mwaka huu, pamoja na kuacha kuvaa sare za chama chochote cha siasa kwa siku hiyoo.
Naye katibu wa CCM mkoa huo Mohamed Ali Khalfan aliwataka wanaccm kutokujitokeza Oktoba 27 kwenda kupiga kura badala yake kubaki majumbani mwao.
Alisema siku hiyo ni siku ya watu maalumu ambao wanatambulia wa tume ya uchaguzi, huku akiwasihi Oktoba 28 baada ya kupiga kura kurudi majumbani na kusubiri kushangiria ushindi wa CCM kwa kishindo.
Mwakilishi Mkongwe wa jimbo hilo Hamad Abdalla Rashid (Gerei), aliwahakikishia wagombea hao wa jimbo la Wawi kuwa bega kwa began a kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Naye aliyekuwa mgombea wa jimbo la Wawi Ubunge ambaye jina lake halikuweza kurudi, Juma Omar Khamis aliwataka wanaCCM kuunganisha nguvu zao kwalengo la kuhakikisha wanashinda viongozi waliopo.
“Mimi kwa sasa niko pamoja na wagombea wetu, chama ndio kimeamua sasa sina la kufanya, kilichobaki ni kuhakikisha ushindi unapatikana”alisema.
Mgombea uwakilishi Jimbo la Wawi Bakari Hamad Bakari, aliahidi kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, kwa kushirikiana na serikali.
Alisema iwapo atapata ridha atahakikisha anarudisha tena vuguvugu la vikundi vya ushirika kwa ajina mama na vijana, ili kuweza kuwasaidia vijana na akinamama kujiajiri wenyewe.
Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo Khamis Kassim Ali, alisema atahakikisha suala la kilimo linarudi katika uhalisia wake, kwa wananchi kutumia mbinu za kisasa katika kilimo.