Monday, November 25

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesaini hati za makabidhiano na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za mitaa na Idara Maalumu za SMZ ili kurejesha Skuli za Maandalizi na Msingi kwa Wizara hiyo.

Hafla ya utiaji wa saini pamoja na makabidhiano hayo ya sekta nyengine zilizogatuliwa umefanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakiil Mnazimmoja Mjini Unguja.
Kwa upande wa Wizara ya Elimu saini hizo zimetiwa na Waziri wa Wizara hiyo mhe Simai Mohammed Said pamoja na Katibu mkuu wake bwana Ali Khamis Juma.
Akizungumza baada ya utiaji saini pamoja na makabidhiano hayo, wakati alipofanya mahojiano na Waandishi wa Habari, mhe Simai amesema  kurudi kwa Elimu ya Msingi katika Wizara hiyo kutaendeleza mashirikiano yaliopo na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ ili kuhakikisha lengo la kuimarisha huduma za Elimu zinapatikanwa kwa Wakati.
 Amesema mashirikiano lazima yaendelezwe kwani wizara zote ni za Serikali  moja na zinafanyakazi kwa lengo la kuleta maendeleo katika nchi.
Mhe Simai amewataka wananchi kuachana na dhana ya kuwa  kuhamisha elimu kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyengine ni kuishusha hadhi sekta hiyo  bali  ni kuhakikisha elimu inaimarika  kutokana na kukua kwa sayansi na teknolojia duniani, pamoja na kwenda sambamba na mitazamo ya wananchi walio wengi, kwani Serikali ya awamu ya nane ni serikali inayowasikiliza wananchi  wake.
Kwa upande wake Waziri wa nchi Ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum  za SMZ  Mhe  Masoud Ali Mohamed  amesema kutokana na kuwa na vyanzo vidogo vya mapato katika Wizara yake ukizingatia  na ongezeko  kubwa la  vituo vya Afya na Skuli za msingi ni vyema kurudi Wizarani mwao ili Wizara zijipange kuendesha kwa huduma bora.
Nae Mkurugenzi Uratibu Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Dkt Haji Salum Khamis akitoa maelezo mafupi juu ya majukumu ya ugatuzi kwa muda wa miaka mitatu amesema tathmini  inaonesha kuwa kumekuepo na uzorotaji wa baadhi ya huduma  na kupelekea na ufanisi mdogo  katika majukumu ya kimaendeleo,  hivyo Serikali imeamua kila sekta kurudi katika Wizara yake ili wananchi waweze kunufaika na huduma bora.
Amesema mashirikiano baina ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ na Wizara zilizogatuliwa utaendelezwa ili kuzidi kuleta ufanisi katika maendeleo kwenye  jamii.
Hati za makabidhiano ya sekta zilizogatuliwa yalisainiwa na Mawaziri wa Wizara na Makatibu Wakuu wao ambapo Wizara hizo ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Wzara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto pamoja na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi.