RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhadj Dk. Hussein Ali Mwinyi amemuomba Mwenyezi Mungu kuwajaalia kheri na malipo mema ya swaumu, wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi waliojumuika pamoja nae katika hafla ya Iftari.
Dk. Mwinyi ameomba dua hiyo leo katika Iftari aliyoianda kwa ajili ya wananchi wa Mkoa Mjini Magharibi katika hafla iliofanyika Ukumbi wa Jengo la Michenzani Mall, jijini Zanzibar, ikiwa ni muendelezo wa utaratibu wake wa kufutari pamoja na wananchi wa Mikoa yote mitano ya Zanzibar .
Amemuomba Mwenyezi Mungu atakabali swaumu za wananchi hao na kuwalipa malipo mema , huku akiwashukuru kwa dhati kwa kuitikia wito wake wa kujumuika na kufutari pamoja.
Aidha, Dk. Mwinyi ameushukuru Uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kwa maandalizi mazuri yaliofanikisha Iftari hiyo pamoja na zawadi mbali mbali walizomtunukia.
Katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi amepata fursa ya kufutari pamoja na makundi mbali mbali ya wananchi wa Mkoa huo, ikiwemo kundi la watu wenye Ulemavu, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla.
Nae, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa amemshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa takrima aliyofanya kwa wananchi hao na kumuomba Mwenyezi Mungu amzidishie kheri nyingi yeye na familia yake.
Aidha, aliwashukuru wananchi wote walioitikia wito wa kiongozi huyo na kujumuika pamoja na katika Iftari hiyo, sambamba na kumtunukia zawadi mbali mbali, ikiwemo mas-hafu, saa ya ukutani (kwa ajili ya mama Mariam) pamoja na marfaa’gh kwa ajili yake na familia yake.
Mapema, akitoa neno la shukurani, Mwinyichande Haruna Mohamed kutoka kundi la watu wenye Ulemavu, alimuombea kheri Rais Dk. Mwinyi na kumuomba Mwenyezi Mungu amuwezesha kutekeleza kwa mafanikio yale aliyolenga kuyafanikisha katika uongozi wake.
Aidha, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo, amesema wananchi wamefarijika mno kutokana na uongozi wa Dk. Mwinyi kwa kuwasogeza karibu na Serikali yao.
Viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Mama Mariam Mwinyi, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, masheikh na wananchi walihudhuria katika hafla hiyo ya Iftari.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar