NA ZUHURA JUMA, PEMBA
WIZARA ya Utalii na Mambo ya kale imejipanga kurejesha michezo ya zamani ambayo kwa sasa imepotea ili kuvutia watalii wa nje na ndani ya nchi.
Akizungumza Mara baada ya kumaliza kufanya usafi katika makumbusho yaliyopo mjini Chake Chake ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya makumbusho duniani, Afisa Mdhamini Wizara hiyo Zuhura Mgeni alisema, siku hiyo ni fursa adhimu katika kuutangaza utalii kwenye visiwa vyao.
Alisema kuwa, katika kisiwa cha Pemba kuna vivutio mbali mbali vya utalii ambavyo vikiboreshwa ama kurejeshwa upya vitawavutia wageni kuingia na wenyeji, jambo ambalo litaongeza pato la nchi.
Alisema, Wizara imejipanga katika kuhakikisha wanairejesha michezo ya zamani, ambayo wanaamini kwamba watavutia watalii mbali wa ndani ya nje ya kisiwa hiki.
“Kwa kweli michezo imepotea sana, hivyo tutahakikisha tunairejesha ili kuweka historia za kisiwa hiki zipate kuonekana na kuwavutia watalii”, alisema Mdhamini huyo.
Aidha aliwataka wanajamii kuwa na utamaduni wa kwenda kwenye maeneo ya kihistoria kujifunza mambo mbali mbali na kupata uelewa kuhusu utamaduni wao wa asili mswahili.
“Tunajitahidi kutoa elimu kwa jamii, lakini bado haina mwamko wa kutosha, kwani wageni wengi tunaopokea ni wale wa kutoka nje ya nchi”, alisema.
Mdhamini huyo pia aliwataka waandishi wa habari kufanya juhudi za makusudi kuvitangaza vivutio vya utalii ili wageni na wenyeji waingie kwa wingi katika kisiwa cha Pemba, jambo ambalo litainufaisha Serikali na jamii nzima kwa ujumla.
Kwa upande wake… Khamis Ali Juma alisema, wamefanya usafi katika makumbusho hayo kwa lengo la kuifanya yawe bora na yenye kuvutia zaidi.
Alieleza kuwa, kwa upande wao wameamua kuadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi sambamba na kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, ili wananchi na wageni wapate ari ya kwenda kujionea na kujifunza vitu mbali mbali.
“Kwa wananchi wengi wao wanakuja kwenye makumbusho na vivutio vya utalii ni wanafunzi, lakini tunashkuru wanajifunza sana na wanafahamu zaidi kwa sababu wanasoma kwa vitendo”, alisema.
Akizungumzia baadhi ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na uchakavu wa jengo la makumbusho ambalo linaweza kupoteza haiba yake na kuweza kusababisha kuharibika kwa vitu vya kihistoria vilivyomo ndani kutokana na kuvuja wakati wa mvua.
“Baadhi ya vivutio vya utalii vinahitaji kufanyiwa maboresho ili kuwa imara na kuvutia watalii”, alisema.
Nae mfanyakazi wa kitengo cha Utafiti katika Idara ya Makumbusho Time Mohamed Mussa alisema, wageni wanaoingia wamekuwa wakisifia sana makumbusho yaliyopo Pemba, hivyo waandishi wana jukumu kubwa la kushirikiana na Wizara kutangaza, ili kuwahamasisha wageni na wenyeji kuingia ndani ya kisiwa hiki kujionea vivutio vilivyopo.
Siku ya Makumbusho duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 18 ya kila mwaka, ambapo kisiwani Pemba wameadhimisha siku hiyo kwa kufanya usafi katika makumbusho yaliyopo mjini Chake Chake.