Monday, November 25

SMZ yaendelea kuimarisha mahusiano ya kimataifa na misingi imara ya utawala bora

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kujenga misingi imara ya utawala bora, uchumi na uwekezaji kwa lengo la kuiona Zanzibar inaendelea kukuwa na kuwa sehemu muhimu kwenye medani za kilimwengu.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo (Mei 25) alipokuwa akizungumza na baadhi ya mabalozi wanaowakilisha mataifa ya Nordic katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mabalozi hao kutoka  Sweeden, Denmark na Finland, walifika ofisini kwake Migombani mjini Unguja kwa lengo la kufanya mazungumzo ya kuona namna Zanzibar ilivyojiandaa kushirikiana na nchi hizo katika maeneo ya shughuli za kijamii, kiuchumi na utawala bora.
“Serikali ya Zanzibar inakusudia kujenga mazingira bora kwa wawekezaji pamoja na kuendeleza amani na mshikamano uliopo ili kufikia maendeleo nchini”, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar aliwaahidi mabalozi hao, huku akisisitiza kwamba vitu hivyo ndivyo vitakavyowavutia wawekezaji kuja nchini kwa wingi.
Kwenye mazungumzo hayo, Mheshimiwa Othman aliorodhesha maeneo kadhaa ambayo nchi za Nordic, ambazo zimekuwa na mahusiano ya kijadi na Zanzibar, zinaweza kuyafanyia kazi kiuwekezaji.
Nao ujumbe wa mabalozi hao ulimueleza Mheshimiwa Othman nia yao ya kutaka kuisaidia Zanzibar kujenga misingi imara ya utawala bora kwa kuimarisha uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa pamoja pia na kuchangia kwenye maendeleo ya sekta za afya, jamii na sekta ya uhifadhi wa mazingira.
Tangu Zanzibar kurejea tena kwenye muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ambao upo kikatiba, washirika wengi wa maendeleo kutoka mataifa ya kigeni wameendelea kumiminika visiwani Zanzibar kuonesha imani yao kwa uongozi uliopo na utayari wao wa kushirikiana na serikali na wananchi kwa ajili ya mustakabali wenye tija kwa pande zote