Monday, November 25

Watu wenye ulemavu kisiwani Pemba wamesema wamechoka kusikia sikia wanatafutiwa haki zao bila kuziona zikitekelezwa.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WATU wenye ulemavu kisiwani Pemba wamesema, pamoja na kwamba wadau mbali mbali wanachukua jitihada za kuwatetea ili kupata haki zao za msingi, bado wanaendelea kuzikosa fursa ambazo walitakiwa kuzipata sawa na watu wengine.

Wamesema, wamekuwa wakiona na kusikia kuanzishwa jumuiya, mashirika na taasisi mbali mbali za kuwatetea, lakini wameelewa kwamba, kumbe wameekwa kama ngazi tu ya kuwafikisha wadau hao kwenye malengo yao waliyoyakusudia na sio kupigania haki za wenye ulemavu.

Wakizungumza katika mkutano wa Agenda za Jukwaa la wadau wa mradi wa Maendeleo Jumuishi katika jamii (CBID), watu wenye ulemavu walisema, wamechoka kusikia sikia wanatafutiwa haki zao bila kuziona zikitekelezwa.

“Kila siku tunaambiwa fursa sawa, lakini hatuzioni, tunaendelea kuteseka kwa hali hizi tunazoishi nazo, tunataka yanayosemwa ambayo ni haki yetu tutekelezewe na sio kudanganywa, maana tumefanywa kama ngazi ya kupanda nyiyi juu zaidi na sisi kuendelea kuteseka”, walisema wenye ulemavu.

Suleiman Mansour mwenye ulemavu wa uoni kutoka Jumuiya ya watu wenye ulemavu (ZANAB) Wilaya ya Chake Chake alisema, hali ya maisha wanayoishi yamekuwa magumu kiasi ambacho wanashindwa kupata huduma stahiki, hivyo wanaomba wasaidiwe kama wanavyosaidiwa wazee wanaopewa pensheni.

“Kwenye ajira hatupewi kipao mbele, mambo mengine ya kijamii tunawekwa nyuma, tunavyotaka tuchague wabunge na wawakilishi wenyewe wapate kwenda kututetea, ila haya yote hatusikilizwi”, alisema Suleiman.

Mratibu wa Kituo cha Masuala ya Ulemavu na Maendeleo Jumuishi Pemba (ZACEDID) Kombo Ali Hamad ambae ana ulemavu wa viungo alisema, bado hawajapewa fursa na haki zao za msingi, jambo ambalo linawahuzunisha na kuwakatisha tamaa ya kuishi.

“Hatujaomba huu ulemavu ila Mungu ndie alietujaalia, hivyo tunaomba mtusaidie tusidhalilike, tunahitaji nguvu zenu kwa pamoja ili na sie tujione sawa na watu wengine”, alisema mratibu huyo.

Nae Mudathir Khamis mwennye ulemavu wa ngozi alisema, kuna changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo, ingawa wamesonga mbele kidogo tofauti na zamani.

“Kweli tunaziona izo juhudi zinazochukuliwa lakini bado tunanyimwa baadhi ya fursa na haki zetu za msingi, ila nawaomba wenzangu tusivunjike moyo kwani Serikali na wadau wanajitahidi, ya leo sio ya jana, naamini ipo siku tutasonga mbele”, alisema.

Mapema akifungua mkutano huo Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi inayohusika na malezi na makuzi bora ya watoto Zanzibar (MECP-Z) Sharifa Suleiman Majid, alisema juhudi za makusudi zinahitaji katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao na fursa.

“Lengo la kuwakutanisha wadau ni kuwaweka pamoja, kila mmoja kwa nafasi yake anafanya juhudi gani ili kuona watu wenye ulemavu wanapata haki zao”, alifahamisha

Afisa Utetezi kutoka Idara ya watu wenye Ulemavu Unguja Ali Yussuf alifahamisha kuwa, kubadilisha fikra na mitazamo ya watu juu jambo fulani kunahitaji muda, hivyo aliwataka watu wenye ulemavu kuwa na subra wakati jitihada za kuwatetea na kuwatafutia haki zao zikiendelea kufanyika.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo Afisa huyo alifafanua, ikiwa muongozo wa Kimataifa utafanyiwa kazi ipasavyo, maisha ya watu wenye ulemavu yatakuwa katika mazingira mazuri.

“Muongozo huo wa Shirika la Afya Ulimwenguni wakishirikiana na wadau wengine wa CBR/CBID, ili kusudi kufanya marekebisho ya kiafya kwa watu wenye ulemavu”, alisema Afisa.

Mwasilishaji Mbaya Ali Haji ambae ni Afisa Jinsia na Maendeleo ya Watu wenye ulemavu kutoka Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais alisema, Tanzania iliridhia mkataba wa Kimataifa wa watu wenye ulemavu Machi 30, mwaka 2007, hivyo inaonesha wazi kwamba kuna jitihada mbali mbali za kuwatetea watu hao ili wapate haki zao.

“Wanatakiwa kuwekewa mazingira rafiki kwenye kazi, wasipewe kazi nzito ambazo hawazimudu, tuwajengee mazingira mazuri ili wasidhalilike, pia kuhakikisha wanawake na watoto wenye ulemavu hakumbani na aina yoyote ya ubaguzi na ukatili”, alisema.

Mradi wa Maendeleo Jumuisho Katika Jamii (CBID) ambao unashughulika na utetezi wa watu wenye ulemavu na elimu mjumuisho, unatekelezwa Wilaya ya Chake Chake kwa Pemba, Wilaya ya Kusini na Mjini kwa Unguja.