Monday, November 25

JAMII imeshauriwa kuwacha kuwatenga na kuwanyanyapaa, Vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya.

NA SAID ABRAHMAN.

 

JAMII imeshauriwa kuwacha kuwatenga na kuwanyanyapaa, Vijana wanaoacha kutumia madawa ya kulevya na kurudi katika jamii zao, kufanya hivyo ni kuwakosesha haki zao za msingi.

 

Hayo yalielezwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa 2021 Luteni Josphine Paul Mwambashi, wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa vijana ambao wameondokana na matumizi ya madawa ya Kulevya huko Wete.

 

Kiongozi huyo aliwataka wananchi kuacha kuwanyanyapaa waathirika wa madawa hayo, badalayake kushirikiana nao pamoja katika shughuli mbali mbali za kimaendeleo.

 

Aidha kiongozi huyo aliwasihi kutokujiingiza katika vishawishi vya utumiaji wa madawa ya kulevya, wakizingatia wao vijana ndio nguvu kazi ya taifa na ndio tegemeo kuwa viongozi hapo baadae.

 

“Niwaombe vijana wenzangu tuache kutumia madawa ya kulevya, dawa ni hatari kwa maisha yetu tunapotumia dawa hizi kuna matukio mengi tunayafanya, dawa zinatupelekea jamii kutokua na imani na sisi, ikizingatiwa sisi ndio tegemeo la taifa hapo baadae”alisema.

 

Mapema akisoma taarifa ya mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Chama Cha Uzazi na Malezi bora Tanzania ( UMATI)  Violeta Alphonce alieleza kuwa shughuli zinazofanywa na Chama hicho ni kutoa elimu ya mabadiliko kwa watumiaji wa dawa ya kulevya.

 

Alisema chama hicho kimekuwa kikitoa elimu ya afya juu ya kujikinga na VVU, homa ya ini, kifua kikuu, Corona na maradhi ya kujaniana, pamoja na kutoa ushauri nasaha na upimaji wa VVU na kifua kwa hiari.

 

Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa UMATI, ilianzisha nyumba ya kurekebishia tabia (sober house) kwa ajili ya kuwasaidia vijana, walio jiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya, ili waweze kupata taaluma sahihi juu ya kuacha kutumia madawa hayo.

 

“Sober House hutumika kubadilisha mienendo ya vijana, wale waliojiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, ili waweze kuacha na matumizi ya madawa hayo na kubadilika tabia na kuishi wakiwa raia wema na wazalishaji katika jamii,”alisema.

Alisema tokea kuanzishwa kwa soba hiyo mwaka 2019, tayari vijana 66 waliokua wakitumia dawa za kulevya, amepokelewa katika soba hiyo na kuachana na utumiaji huo.

 

“Lakini tokea kuanzisha kwa Kituo hichi Cha Sober House hapo mwaka 2019 tayari kituo chetu kimeshapokea jumla ya vijana 66 ambao walikuwa ni watumiaji wa madawa hayo,” alisema Violence.

 

Kwa upande wao vijana ambao wameacha kutumia dawa za kulevya na wapo katika soba hiyo, wamesema kuanzishwa kwa Sober House hapa nchini kumeweza kupunguza wimbi kubwa la vijana, ambao walikuwa ni watumiaji wakubwa wa madawa ya kulevya.

 

“Sisi sio kama tunapenda kutumia madawa haya, ila ni vishawishina mazingira ambayo tunakaa, hivyo hupelekea mtu kujiingia katika masuala haya”walisema.

 

Thani Salim Said mmoja wa vijana walioko katika soba hiyo, aliyomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia dawa aina ya methein, kwani upande wa pemba wanahitaji kutumia dawa hizo kama ilivyo Unguja.