Monday, November 25

BUME Pemba wajipanga mashindano UMISETA

NA SAID ABRHAMN, PEMBA.

 

WAKATI zimebaki siku 17 tu kuanza kwa mashindano ya UMISETA huko Manyara Tanzania Bara, Wizara ya elimu na mafunzo ya amali kupitia idara yake ya michezo na Utamaduni Kisiwani Pemba, imesema imesema imejipanga vilivyo ili kuhakikisha wanashiriki michezo hiyo kwa ushindani mkubwa.

 

Idara hiyo imesema kuwa tayari imeshaunda kikosi kabambe, kitakachoshiriki mashindano hayo makubwa kikiwa na jumla ya wachezaji 60 pamoja na viongozi wake wanne (4).

 

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Mratibu wa Idara ya michezo na Utamaduni kutoka Wizara ya elimu na mafunzo ya amali Pemba Mzee Ali Abdalla (Kocha), alieleza kuwa kikosi Chake tayari kimeshaanza mazoezi ili kujiweka tayari na mashindano hayo.

 

Mratibu huyo alifahamisha kwa upande wa Pemba, watakuwa na timu nne (4) hadi tano (5) za michezo mbali mbali, ikiwa ni pamoja na mpira wa miguu, mchezo wa wavu, mpira wa kikapu, riadha na mchezo wa ‘tenis table’ ambapo kwa mwaka huu ndio mara yao ya mwanzo kushiriki mchezo huo.

 

“Sisi Pemba tumejiandaa vizuri, kushiriki katika mashindano hayo makubwa kwa Skuli za Sekondari, hii ni fursa adhimu tokea mwaka 2016 kusimama kwa Idara ya michezo Zanzibar, tumepata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano yanayojuilikana kwa UMISETA, kwa namna ya kipekee sisi huku Zanzibar tumepata bahati ya kushiriki Kanda ya Unguja na kanda ya Pemba”alisema.

 

Hata hivyo Kocha Mzee alisema kwa upande wa mafanikio ni makubwa, wamekuwa na historia mzuri licha ya kuwa fursa hiyo kwa upande wao imekuja muda mchache tu, katika mashindano yaliyofanyika mwaka 2018, Pemba mpira wa miguu walifikia hatua ya robo fainali katika Mikoa 28 iliyoshiriki pale.

 

“Mwaka 2017 ilikuwa ni mara yetu ya kwanza kushiriki mashindano yale, tuliweza kupata nafasi ya tatu bora katika mchezo wa ‘basketball’ ukilinganisha na Mikoa mengine, tayari imeshashiriki zaidi ya mara 10 katika mashindano hayo, hata kwa upande wa riadha mita 200, tumeshafikia hatua ya fainali”alisema.

 

Kocha Mzee alifahamisha timu za Pemba zimekuwa na ushindani mkubwa katika mashindano hayo, hivyo kwa sasa timu zinaendelea na maandalizi yake, ili kuhakikisha wanaingia katika ushindani na sio kushiriki tu.

 

Akizungumzia suala la kambi kwa timu hizo, Mratibu huyo alisema kuwa wanatarajia kuingia kambini rasmi Juni 10 ambapo itachukuwa muda wa wiki moja, kabla ya Safari yao ya kwenda Unguja ili kuungana na wenzao kwa ajili ya Safari ya Mtwara hapo June 18.