NA ABDI SULEIMAN.
WATAALAMU wa mazingira Nchini wameshauri watu binafsi, taasisi, Mashirika, Makampuni nchini Tanzania na Waandishi wa habari, kufanya biashara ya hewa ukaa (carbon trading) ili kupunguza uchafuzi wa hewa na ongezeko la joto duniani, jambo litakalosaidia kutunza mazingira.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha kuratibu Hewa Ukaa Tanzinia (National Carbon Monitoring Centre – NCMC) Profesa Eliakimu Zahabu, wakati alipokua akizungumza katika ufungu wa mafunzo kwa waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania juu ya Mabadiliko ya Tabianchi na biashara ya hewa ukaa (Carbon trading) yaliyofanyika katika ukumbi wa NCMC Morogoro.
Alisema kuwa biashara ya hewa ukaa ni mfumo katika soko la dunia, ambao unakusudia kupunguza gesi joto (GHGs) zinazochangia kuongezeka kwa Joto la Dunia, zinazotokana na shuhuli za viwandani, uchomaji moto wa uoto na ukataji wa miti.
Profesa Zahabu alisema dunia kwa sasa ikiwemo Tanzania inakabiliwa na athari nyingi za mabadiliko ya tabianchi, jambo ambalo limekua likirudisha nyuma shuhuli mbali mbali pamoja na kuathiri uchumi wa nchi.
“Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ni ongezeko la joto la dunia, ukame, mafuriko, uhaba wa chakula, maji na kuenea kwa magonjwa ya aina mbali mbali yakiwemo maradhi ya mripuko”alisema.
Aidha alifahamisha kwamba biashara ya hewa ikaa inahusiana na upandaji na utunzaji wa miti, pamoja na kuweka mifumo inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika shughuli mbalimbali, huku akibainisha kuwa biashara hiyo ili ifanikiwe inahitaji kutimiza vigezo vya kimataifa na kupata kibali cha nchi husika.
“Miradi hii inahitaji rasilimali za kutosha zikiwemo fedha na kufanya utafiti wa kina, ili ukidhi viwango vya kimataifa vinavyosimamia biashara hiyo,” alisema.
Mapema akifungua mafunzo hayo, Rasi wa Ndaki ya Misitu wanyamapori na Utalii Profesa Suzana Augostino, kutoka chuo kikuu cha Morogoro (SUA) aliwapongeza waandishi wa habari kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi (UNCFCCC) ulioanzishwa mwaka 1992.
Aidha alisema mpango huo unatoa wito kwa anchi wanachama kupunguza Gesi Joto (GHGs) katika anga ambazo ndizo sababu ya mabadiliko ya tabianchi.
Profesa Suzana alizitaja athari za mabadiliko ya tabianchi ni pamoja na kuongezeka kwa mafuriko ya mara kwa mara, uhaba wa chakula na maji, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kama Malaria na Homa ya bonde la Ufa (RVF), kuyeyuka kwa Theluji kwenye milima mirefu nan cha za dunia, pamoja na kutoweka kwa visiwa vidogo vidigo nchini.
“Moja ya mipango ni biashara ya kaboni ya misitu (hewa ukaa), ilikua ina inawezekana kupitia sera ya maendeleo safi (Clean Development Mechanism -CDM) ya itifaki ya Kyoto ya UNFCCC, ambapo shughuli za upandaji miti mipya zinaruhusiwa”alisema.
Alisema kuwepo kwa mkutano huo ili kuwahabarisha wadau juu ya shughuli za NCMC na maswala ya mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla, pia utawawezesha kuwa na uelewa mpana wa jinsi nchi ya tanzania inavyopambana na swala la mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mhadhiri mwandamizi idara ya Mazingira kutoka NCMC SUA Deo Shirima, akiwasilisha mada juu ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi na matokeo yake Tanzania, alisema shuhuli za viwanda na kibinaadamu zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa gesi joto nchini.
Alisema sekta zote zimeathiria na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo uchumi, mmomonyoko wa miundombinu, kipindi kikubwa cha kiangazi na mvua, wadudu kuathiri mazao na mifugo.
Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waandishi wa habari za Mazingira tanzania (JET), Jonh Chikomo alisema suala la kutumia takuwimu ni muhimu sana katika habari.
Aidha aliwatakam waandishi wa habari kuendelea kujikita zaidi katika kuandika habari zinazohusiana na masuala ya mazingira, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.
Kwa upande wake mwandishi wa kutoka Gazeti la Raia Mwema elix Mwakyembe, alitaka kuwepo kwa mashirikiano makubwa baina ya waandishi wa habari na kituo cha NCMC, katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na biashara ya hewa ukaa.