Friday, January 10

Mradi wa Umeme wa Rusumo kukamilika Dec, 2021

Waziri wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na Waandishi wa Habari, mara baada ya Mawaziri wa nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi zinazohusika na Mradi wa Umeme wa Rusumo kumaliza mkutano wao uliofanyika tarehe 12 Juni, 2021 mara baada ya kutembelea eneo la Mradi na kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa na wakandarasi.Kushoto kwa Waziri wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ni Waziri wa Miundombinu Rwanda, Mhe.  Balozi Claver Gatete.

Waziri wa Nishati Tanzania, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, ( wa pili kutoka kushoto) akimuuliza swali Mhandisi Mshauri Bosco Mugabo anayesimamia ujenzi wa kituo cha kufua Umeme cha Rusumo kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa Bwawa la Mradi wa Umeme wa Rusumo.Kulia kwa Dkt. Kalemani ni Waziri wa Miundombinu Rwanda, Mhe.  Balozi Claver Gatete na Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi Mhe. Ibrahim Uwizeye.

Na Dorina G. Makaya – Ngara

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema, Mradi wa Umeme wa Rusumo utakamilika Desemba, 2021.

Waziri Kalemani ametoa taarifa hiyo tarehe 12 Juni, 2021 katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao cha pamoja cha Mawaziri wa nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi zinazohusika na Mradi wa Umeme wa Rusumo kilichofanyika katika eneo la mradi la Rusumo.

Waziri Kalemani ameeleza kuwa, Mawaziri wa nchi zote tatu zinazohusika na Mradi wa Rusumo, Waziri wa Nishati na Migodi wa Burundi, Mhe. Ibrahim Uwizeye, Waziri wa Miundombinu Mhe. Balozi Claver Gatete  pamoja na yeye mwenyewe Waziri wa Nishati wa Tanzania,  wameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Rusumo ambao ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 80.

Aidha, Dkt. Kalemani amebainisha kuwa, handaki la kupitishia maji yanayotoka kwenye bwawa kwenda kwenye mitambo ya kuzalisha umeme lenye urefu wa mita 703 tayari limekamilika kwa asilimia 80 tarehe 12 mwezi Juni, 2021.

Waziri Kalemani ameeleza kuwa, njia za kusafirisha umeme zitagharimu dola milioni 113.2 na kuwa, baada ya kukamilika ujenzi zitaokolewa dola milioni 25 ambazo zitatumika katika kujengea njia nyingine ya umeme kwa nchi zote tatu ili kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika nchi hizo.

Amebainisha kuwa, jumla ya shilingi bilioni 10 za kitanzania zimetumika kwa ajili ya miradi ya kijamii katika wilaya ya ngara kwa upande wa Tanzania, ambapo miradi hiyo inahusisha ujenzi wa vituo vya afya viwili, ujenzi wa zahanati mbili, ujenzi wa shule za sekondari 3, ujenzi wa shule za msingi mbili, ujenzi wa chuo cha ufundi stadi na ujenzi wa miradi miwili ya maji pamoja na miradi ya kilimo na ufugaji wa nyuki. inayowanufaisha wakazi wa wilaya ya Ngara

Dkt. Kalemani ametoa wito kwa watumiaji wa maji ya mto Rubuvu na mto Kagera, kutumia maji ya mito hiyo kwa uangalifu pamoja na kutunza vyanzo vya mito hiyo ili Mradi wa Umeme wa Rusumo usipungukiwe na maji huku akibainisha kuwa, upo uwezekano wa kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme wa Mradi wa Umeme wa Rusumo .

Ziara hiyo ililenga kutembelea mradi huo na kuona maendeleo yake pamoja na kutoa maelekezo kwa wakandarasi  kuhusiana na umuhimu wa kukamilishwa kwa ujenzi wa Mradi huo kama ilivyopangwa.

Mawaziri kutoka Tanzania, Rwanda na Burundi walitembelea  eneo linapojengwa Bwawa, ( Dam site), Eneo la kuzalisha umeme ( Power House), na Eneo la kupokea umeme kabla haujasambazwa ( Switch yard) na kuridhishwa na kasi ya ujenzi.

Waziri Kalemani amesema, Mradi wa Umeme wa Rusumo ni  muhimu sana na kukamilika kwake kutaondoa changamoto nyingi za umeme na kuwa baada ya kikao cha pamoja cha Mawaziri wa nchi zote tatu, wamewataka wakandarasi hao ifikapo mwezi Desemba, 2021 wawe wamekabidhi Mradi na wananchi waanze kutumia umeme unaotokana na Mradi huo wa Umeme wa Rusumo.

Mradi wa umeme wa Maporomoko ya maji Rusumo ulianza mwezi Machi 2017 na utazalisha MW 80 ambapo nchi tatu husika za Tanzania, Rwanda na Burundi zitapata mgao sawa wa MW 27 zitakazoingizwa kwenye gridi ya Taifa kwa kila nchi.

Katika ziara hiyo Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani, aliambata na Kamishna Msaidizi wa Umeme, Mhandisi Innocent Luoga, wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO pamoja na Uongozi wa Serikali wa Wilaya ya Ngara.