Sunday, November 24

Matokeo ya uchaguzi Tanzania 2020: Je, nani na nani kuingia Baraza jipya la Mawaziri wa Rais Magufuli?

CHANZO CHA PICHA,AFP • Na Markus Mpangala • Mchambuzi, Tanzania

Saa 1 iliyopita

 

Leo Ijumaa rais mteule wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuhutubia Bunge la nchi hiyo katika jiji la Dodoma lililopo katikati ya taifa hilo la Afrika mashariki ambayo itazindua rasmi Bunge la 12. Tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka huu kuliongoza taifa hilo katika kipindi cha pili wa miaka mitano 2020-2025, hivi karibuni akiwa jijini humo mbele ya wabunge wa CCM alibainisha kuwa hana mpango wa kuteua wakuu wapya wa mikoa, wilaya, makatibu wakuu wa wizara, wakurugenzi wa Halmashauri na taasisi mbalimbali za umma badala yake amewataka waendelee kuchapa kazi kama walivyoanza pamoja na hivyo wamalize wakiwa wamoja.

Mbali ya hilo, rais huyo anakabiliwa na kibarua kizito cha kuunda baraza jipya la mawaziri la serikali yake, huku baadhi ya viongozi wa chama na serikali wakisema ni vema wateule waliopo madarakani wakachukua tahadhari kwa kile kilichoitwa Rais Magufuli ametoka kwenye kampeni za uchaguzi mkuu kwa kuzunguka mikoa mbalimbali hivyo ameona hali halisi na malalamiko ya wananchi maeneo aliyopita.

Aidha, vyanzo vya habari kutoka ndani ya chama tawala CCM na serikalini vimedokeza kuwa msimamo wa Rais Magufuli hauwezi kuchukuliwa kirahisi na wateule wake ambao wana uzoefu wa miaka mitano ya uteuzi na utenguzi wa mawaziri, wakurugenzi wa taasisi za umma, wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala mikoa na wilaya pamoja na mengine yaliyomo kwenye mamlaka yake, wakirejea matukio mawili yaliyovutia hisia za watu ya kutumbuliwa Nape Nnauye aliyekuwa waziri wa habari pamoja na Wilson Kabwe aliyekuwa Mkurugenzi wa Dar es salaam, utenguzi wa aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dkt. Methodius Kapilimba na mawaziri kadhaa.

Kiongozi mmoja wa CCM amemwambia mwandishi wa makala haya, “Tunatoka kwenye uchaguzi, na Rais amezunguka takribani mikoa 19 nchini, amepata malalamiko ya wananchi na changamoto zao, naamini atakazoshughulikia kwa miaka hii mitano. Sasa ili kuondoa changamoto hizo ni lazima wasaidizi hao washiriki kikamilifu, siamini kama yupo mzembe atavumiliwa kisa kauli yake ya kutobadili watendaji, uzoefu tunao miaka mitano wote tumeona,”

Imeelezwa na wandani wa CCM na serikali kuwa uamuzi wa kuwabakiza wateule wake unalenga kuonesha mshikamano katika mafanikio waliyopata katika kipindi cha miaka mitano pamoja na kuimarisha timu aliyoteua na kuvunja utamaduni wa siasa na uongozi nchini humo ambapo marais huteua viongozi wapya mara baada ya kuchaguliwa upya.

“Hilo kutobadili wateule hasa wakuu wa mikoa,wilaya,wakurugenzi,makatibu tawala mikoa na wilaya, makatibu wa wizara ni ishara ya kukubali utendaji wao, na kama sote tunakiri Tanzania imepiga hatua ndani ya miaka mitano basi hatua hiyo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na wateule hao wa Rais. Japo hii haiwapi nafasi watajwa hao ya kujisahau na kuchukulia mambo kimazoea, Rais naamini sio muumini wa kufanya mambo kwa mazoea, mara zote anapenda matokeo yaonekane na hatua zichukuliwe kwa haraka ili kuwahudumia wananchi,” anasema George Ndimbo, mchambuzi wa siasa na utawala bora nchini Tanzania.

Namna gani Rais Magufuli anaweza kuteua mawaziri wake?

Mosi, mgawanyo wa kanda ni sababu mojawapo itakayounda baraza la mawaziri.

Uwakilishi wa kanda mbalimbali kuanzia kusini mpaka kaskazini, pwani mpaka kanda ya ziwa ni moja ya mambo ambayo kwa kawaida huchangia usukaji wa baraza kwa nafasi za mawaziri na manaibu wao.

Rais pia atateuwa mawaziri kutoka pande zote mbili za Muungano, Tanzania Bara na Zanzibar.

Pili, uwiano wa jinsia ni sababu nyingine itakayowaibua baadhi ya wanasiasa wanawake kuingia kwenye baraza la mawaziri. Kwamba baraza jipya la mawaziri linatakiwa kuwa na wastani fulani wa uwiano kulingana na jinsia kama sehemu ya kuchagiza haki sawa au asilimia 50-50 kama ilivyokubaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo Tanzania ni mwanachama wake.

Tatu, uzoefu, hii ni miongoni mwa sababu nyingine ambayo inawapa nafasi kubwa mawaziri wa baraza lililopita kurudishwa kwenye nyadhifa zao ama kupatiwa mpya. William Lukuvi ni mwanasiasa mzoefu aliyehudumu wizara mbalimbali ikiwemo ardhi anatajwa kupenya kutokana na hoja hii, sawa na Jenista Mhagama aliyekuwa Waziri wa Nchi na mnadhimu wa serikali Bungeni.

Nne, wabunge wa kuteuliwa, ni eneo lingine linalompa nafasi kupata mawaziri watakaounda baraza lake. Katiba ya Tanzania inampa nafasi Rais kuteua wanasiasa 10 kuwa wabunge, ambapo mara kadhaa wabunge hao huunda sehemu ya baraza la mawaziri. Katika baraza lililopita mathalan, Dkt. Philip Mpango, Profesa Joyce Ndalichako, Profesa Palamagamba Kabudi, Profesa Makame Mbarawa wote walikuwa ni wabunge wa kuteuliwa na rais. Hata hivyo, mpaka sasa rais bado hajateuwa mbunge hata mmoja katika nafasi zake 10.

Tano, umri na suala la vijana kukabidhiwa nafasi za uongozi linatarajiwa kuibukia kwenye uundwaji wa Baraza la Mawaziri.

Wakili wa Kujitegemea Stanislaus Kigosi, amesema, “Baraza la Mawaziri naamini litakuwa na sura nyinyi mpya hasa vijana ambao walikuwa kwenye nafasi za uteuzi awali kama Wakuu wa mikoa na Wilaya. Hili kundi la wateule wa Rais Magufuli mwenyewe na kwamba aliliridhishwa na utendaji wao na pia akaridhia wapiti kwenye mchakato wa kuwania ubunge ndani ya chama, akiwa Mwenyekiti wa CCM. Kubwa na la msingi ni kwamba sasa hivi sehemu kubwa ya wabunge yeye ndiye aliyewawezesha kupita, hivyo anao uwanja mpana wa kuchagua mawaziri na Naibu Mawaziri, tofauti na kipindi cha kwanza ambapo alikuta wabunge wote wameandaliwa na mtangulizi wake hivyo kukosa fursa ya kuunda timu aliyoitaka yeye. Kisheria hakuna mahala ambapo amekiuka au atakuwa kinyume kwenye hili la uteuzi. Katiba imemuachia uwanja mpana wa kuteua amtakaye kufanya kazi azitakazo.”,”

Je, ni upi mwelekeo wa Baraza jipya la Mawaziri?

Siasa za CCM mgombea mpya wa urais hana uamuzi juu ya wanasiasa gani wateuliwe kuwania nafasi za ubunge. Uongozi wa rais anayemaliza muda wake ndiye hufanya kazi zote, hivyo basi wakati Magufuli anaanza ngwe ya kwanza hakushiriki kuwateua wabunge aliokuwa nao 2015-2020. Katika kipindi chake cha pili ameshiriki kupitishwa kwa wingi wanasiasa ambao anatarajia kuwatumia katika Baraza la mawaziri. Mwelekeo wake ni kuunda kikosi kipya kuelekea uchaguzi wa ndani mwaka 2022 pamoja na Rais,Bunge na Udiwani mwaka 2025 chenye taswira yake.

“Bunge la sasa lina wabunge wapya, wapo 170, ni wengi sana na tufahamu bunge la 12 linaundwa na makada wa CCM hivyo kumpa Rais Magufuli machaguo ya kutosha miongoni mwao. Rais anaweza kuyakwepa makundi ya siasa za uchaguzi kuelekea mwaka 2025 ama kulipa kundi nguvu kundi mojawapo kwa kumteua mtu wao huku makundi mengine akiyaweka pembeni yasipate kuonekana kupitia uwaziri. Kwa vile hiki ni kipindi chake cha mwisho, basi makundi yatakuwa wazi bila kificho ingawaje ninazo taarifa za ndani ya chama hicho kuwa makundi hayo yamekwishakuanza tayari. Najaribu kulichambua kundi la wanasiasa vijana mfano Januari Makamba, Nape Nnauye, Abdurahman Kinana, bila wasiwasi lina ufuasi imara na hilo, na tujue rais ajaye atapatikana ndani ya bunge hili hili,” amesema Richard Ngaya, Mhahiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine.

Nani kupaa au kutunguliwa Baraza jipya?

Mawaziri wa zamani Jenista Mhagama, Ummy Mwalimu, Stella Manyanya, Hussein Bashe, Dkt.Hamis Kigwangala, George Simbachawene,Seleman Jaffo, Profesa Joyce Ndalichako, Mwigulu Nchemba, William Lukuvi ni miongoni mwa majina yanayotarajiwa kupaa kwenda Baraza hilo. Hata hivyo halitakuwa jambo la kushangaza kutunguliwa Kapteni George Mkuchika licha ya uzoefu alionao lakini umri umemtupa mkono kuendana na kasi ya rais.

Kimsingi mawaziri hawa ni wazoefu kisiasa na uongozi tofauti na wabunge wengine wapya wa CCM ambao wamo kwenye kundi la wabunge wapya 170 ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Hawa ni baadhi ya mawaziri ambao walifanya kazi katika baraza lililopita kwanza huenda wakarejeshwa tena.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mchambuzi wa siasa, George Ndimbo, ambayo amesema, “Kwenye baraza la mawaziri, wale waliokuwepo baraza lililopita wana nafasi kubwa kwani wamefanya kazi kwa weledi mkubwa na kuifanya nchi kuingia kwenye uchumi wa kati. Lakini tutashuhudia tengua teua awamu hii kama ile iliyopita, kwani wabunge wengi walioingia safari hii wako vizuri kwa maana ya kuwa na uwezo mkubwa kiutawala na kiutendaji”

Kwenye siasa yapo mazingira yanang’arisha nyota ya mwanasiasa kupaa zaidi. Wapo wanasiasa ambao wanatarajiwa nyota zao kung’ara katika baraza hilo. “Profesa Kitila Mkumbo atakuwa ingizo jipya kwenye baraza hili bila shaka. Ukumbuke Rais akiwa mkoani Singida kwenye mkutano wa kampeni za jimbo la Mwigulu Nchemba, alisema amemtuma kugombea ubunge Ubungo kwa vile wote wawili anawahitaji. Kisiasa hii ni tafsiri ya dhahiri kuwa Kitila anakwenda kuingia barazani, lililobaki ni uamuzi wa Rais Magufuli amweke wizara ipi.” Ameeleza Mbunge mmoja wa CCM.

Je, ni wizara zipi zinazolengwa zaidi?

Linapoundwa baraza la mawaziri jambo lingine la kutazamwa ni wizara nyeti. Hizi ni wizara ambazo zinalengwa zaidi, ambapo zinagusa uti wa mgongo wa serikali.

Tayari Rais Magufuli ameshafanya uteuzi katika Wizara mbili nyeti Fedha pamoja na Mambo ya Nje ambapo Dkt Philip Mpango na Profesa Palamagamba Kabudi wamerudi katika nafasi zao mtawalia.

Macho na masikio ya watu sasa yanaelekezwa kwenye wizara nyeti nyengine kama Ulinzi, Madini, Mambo ya Ndani, Elimu na Afya.

Gabriel Mushi, Mwandishi wa habari wa masuala ya siasa na utawala bora amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa Baraza la mawaziri litakuwa na mapya. Jambo la kwanza, Rais Magufuli ameshapata uzoefu kwa wateule wake mwenyewe aliokuwa nao kati ya mwaka 2015-2020, iwe wale walioishia njiani na kutumbuliwa ama wale walioendelea naye hadi mwisho kabla ya kuingia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Pili, wapo wateule ambao wameshindwa kuendana na kasi yake ya utendaji katika kipindi cha kwanza kisha wakatemwa.

“Jambo la tatu, tayari Rais Magufuli amepata wabunge wa kutosha. Ingawa sio wote lakini imemsaidia kupunguza wimbi kubwa la waliokuwa omba omba kwake, maana tumemsikia akizungumzia suala la kutumiwa meseji za wateule wake hao,” ameeleza Mushi.

Kutamatisha ni dhahiri baraza hili litaunda mwelekeo wa CCM na serikali kuelekea uchaguzi wa mwaka 2025. Ndicho kipindi ambacho wateule watahakikisha wanatumia kila mbinu kubaki wizarani na kujitengenezea njia ya kumrithi bosi wao ama kujenga ushawishi ambao wenye maamuzi watalazimika kuwatazama na watakuwa wazi kujali matokeo chanya ya harakati zao. Ni kete muhimu kwa kila mteuliwa.