Tuesday, November 26

WIKI ya Maadhimisho kuelekea siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa Dawa za kulevya Duniani, imeanza Kisiwani Pemba.

WANAFUNZI kutoka Chuo cha Afya Pemba, wakifuatilia kwa makini mafunzo ya siku juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa jina, ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya siku ya kupiga vita Matumizi na Usafirishaji wa dawa za kulevya Zanzibar, shamrashamra hizo Pemba zimeanza Juni 20 mwaka huu.
WATENDAJI kutoka tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya Pemba, pamoja na vijana walioacha kutumia dawa kulevya kutoka Soba House ya Mkoroshoni, wakifanya usafi katika Hospitali ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya siku ya kupiga vita Matumizi na Usafirishaji wa dawa za kulevya Zanzibar, shamrashamra hizo Pemba zimeanza Juni 20 mwaka huu.

(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NA ABDI SULEIMAN.

WIKI ya Maadhimisho kuelekea siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa Dawa za kulevya Duniani, imeanza Kisiwani Pemba kwa shuhuli mbali mbali ndani ya Kisiwa cha Pemba.

Miongoni mwa shuhuli ambazo zimeanza kufanyika katika wiki hiyo, ni mkutano wa Tiba ya Kifamilia, Mkutano wa wazazi shehia ya Ndagoni, Ufanyaji usafi Hospitali ya Wete na utoaji wa elimu kwa wanafunzi wa chuo cha afya Wete.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa shuhuli za Usafi katika Hospitali ya Wete, Afisa uwendeshaji tiba kutoka wizara ya afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee wanawake na watoto Pemba Dkt.Yussuf Hamad Iddi, alisema vijana walioko soba House ni walimu wakubwa kwa vijana wengine wanaotumia dawa za kulevya.

Alisema kujiunga kwao katika Soba house ni elimu tosha, kwani inaonyesha wamekubali na kuwa mfano mzuri katika jamii, sambamba na kuwa waelimishaji wakubwa wa jamii na vijana wengine kujiunga katika Soba house.

“Sisi tuliomo humu tunapaswa kufuata taratibu na sheria zote, tunapaswa kuacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya zaidi kuwaelezea vijana walioko mitaani”alisema.

Kwa upande wa wanafunzi wa Chuo cha afya Wete Pemba, Dkt Yussuf aliwasihi wanafunzi hao baada ya kumaliza chuo kuelindelea kuelimisha jamii juu ya elimu ya afya na sio kujiona ni wanataaluma.

“Lazima suala la elimu ya afya kuendelea kutolewa, nyinyi ni mfano mzuri kwa jamii kuwapatia elimu hiyo,lazima tutumie taaluma zetu katika suala la kuelimisha jamii, tunajua jamii inachangamoto nyingi za kielimu”alisema.

Kwa upande wake Mratib wa tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya Pemba, Omar Juma Mbarouk alisema katika kuadhimisha siku ya kupiga vita matumizi na usafirishaji wa dawa za kulevya mwaka 2021 imefuatana na shuli mbali mbali za jamii.

Alisema lengo kubwa ni kuwaonyesha wanajamii athari za matumizi ya dawa hizo kwa jamii, huku akiwataka vijana kuachana na matumizi ya dawa hizo.

“Hizi dawa ni hatari sana kwa jamii, zinaweza kukuondoshea utu na heshima ya utu wako, vizuri sasa kuwa mstari wambele katika kupiga vita dawa hizo”alisema.

Akizungumza na wananchi wa ndagoni shehia ya Wesha, Dkt.Ali Yussuf Ali kutoka tume ya Kitaifa ya kuratibu na udhibiti wa Dawa za kulevya Pemba, aliwataka vijana kutambua athari za matumizi ya dawa za kulevya kwani zinapoteza nguvu kazi ya taifa.

Hata hivyo aliitaka jamii kukemea na kuwafichua waletaji na wauzaji wa dawa hizo kwa jamii, sambamba na kuachana na muhali kwa jamii.

Naye afisa sheria kutoka Tume hiyo Pemba Daudi Juma Nunga, aliwapongeza vijana ambao wamekubali kuachana na matumizi ya dawa za kulevya na kujiunga na soba house, kwani kujiunga humo kunawafanya kubadilika tabia kwao.