Tuesday, November 26

WANAJAMII wanatakiwa kuacha tamaa ili kuepuka rushwa kwani inachangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji.

 

JAMII imetakiwa kucha tamaa ili kuepuka rushwa ambayo inachangia kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa skuli mbali mbali katika Ukumbi wa skuli ya Chasasa Wete, Afisa Taaluma kutoka Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Khamis Kombo alisema, rushwa inatendeka sana kwenye kesi za udhalilishaji.
Alisema kuwa, kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kujua na kupigania, hivyo ni vyema jamii ikaepuka rushwa, ili kuondosha janga hilo la vitendo vya udhalilishaji.
“Rushwa ni tatizo sugu linalokwamisha maendeleo, hivyo tushirikiane kuhakikisha tunadhibiti mianya ya rushwa, ili l vitendo vya udhalilishaji visiendelee kufanywa”, alisema.
Alieleza kuwa, kuna mikakati mbali mbali ambayo imewekwa na Serikali katika kuhakikisha wanaondoa rushwa, ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakizipa mgongo juhudi hizo, jambo ambalo linakwamisha upatikanaji wa haki na kudumaza maendeleo ya nchi.
“Sasa tumeweka mikakati kuhakikisha kesi za udhalilishaji zinaenda mahakamani na mshitakiwa anapata hatia, kwa sababu kesi nyingi zinafutwa na kuondolewa mahakamani kwa kisingizio cha kutofika kwa mashahidi”, alisema Afisa huyo.
Aliwataka viongozi na wanaoshughulikia kesi hizo kuwa mfano mzuri wa kutojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye udhalilishaji, kwani inasababisha kukwamisha upatikanaji wa haki kwa wahanga wa kesi hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Taaluma kutoka ZAECA Mkoa wa Kaskazini Pemba, Shuwekha Abdalla Omar alisema, jamii imekuwa ikitoa na kupokea rushwa katika kesi za udhalilishaji, jambo ambalo linachangia ongezeko la vitendo hivyo siku hadi siku.
“Kumekuwa na ubadilishwaji wa umri wa watuhumiwa na wahanga ili watuhumiwa waachiwe huru, hapa kuna rushwa inatendeka lakini sasa ZAECA tuko makini na tunafuatilia”, alisema Mkuu huyo.
Alisema kuwa, watoto wanatakiwa wapate elimu kwani ndio mkombozi wao wa maisha na sio kufanyiwa vitendo viovu, hivyo watendaji wa makosa hayo wachukuliwe hatua za kisheria na sio kuachwa.
Nae Mkuu wa Programu kutoka Shirika la Action aid Pemba Omar Salim Ali alieleza kuwa, kulalamika ni kushindwa kutetea haki yako, hivyo aliwataka wanafunzi hao wajue haki zao za msingi na kuweza kuzitetea pale ambapo zimevunjwa.
“Tunatoa elimu kwa jamii ili kila mmoja ajue haki yake na kuweza kutetea wakati anapoona zimevunjwa”, alisema.
Othman Ali Juma kutoka Shirika la Action aid Pemba alifahamisha kuwa, bado ZAECA ina kazi kubwa ya kupambana na rushwa, kwani wanapoandaa mikakati ya kudhibiti, nao wala rushwa wanaanda mbinu mpya ya kula rushwa.
“Siku hizi rushwa zinapitia kwenye miamala ya kwenye mitandao, hivyo sio rahisi watu kuwakamata, hivyo tujitahidini lakini tujue kwamba tuna kazi kubwa”, alisema Othman.
Mapema Afisa Elimu Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanaepuka rushwa katika nyanja zote na wajue athari zake, ili wasaidie mapambano.
“Nyinyi ndio viongozi wa baadae, hivyo ikiwa mtajihusisha na rushwa pamoja na vitendo vya udhalilishaji, Taifa litakuwa halina uimara na maendeleo hayatopatikana”, alifafanua.
Nao wanafunzi hao walishukuru kupatiwa mafunzo hayo na kusema kwamba watayafanyia kazi kadiri walivyoelikezwa ili kupata taifa lililobora zaidi.
Mkutano huo wa siku moja ulioandaliwa na Shirika la Action aid Pemba, ukiwa na lengo la kuwapa wanafunzi elimu ya rushwa, ili kuwajenga zaidi na kusaidia mapambano dhidi ya rushwa.