Saturday, October 19

Wananchi kuchukua tahadhari juu ya Kichocho.

WATAALAMU wa maradhi ya kichocho kutoka kitengo cha maradhi yasiopewa kipau mbele kilichopo Mkoroshoni Chake Chake,wakisaidiwa na wataalamu kutoka China wakiua makonono yanayosababisha maradhi hayo katika moja ya mabonde huko Mgagadu Wilaya ya Mkoani.(PICHA KWA HISANI YA DK.SALEH JUMA)

WANANCHI Kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea kujitahidi kuchukua tahadhari juu ya maradhi ya Kichocho, katika kipindi hiki cha mvua za Vuli zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali.

Wito huo umetolwa na mratib wa kitengo cha Maradhi yasiopewa Kipau Mbele Pemba, Dk.Saleh Juma Mohamed huko Ofisini kwake mkoroshoni Chake Chake Pemba.

Dk.Saleh alisema katika kipindi hiki cha mvua za vuli zinazoendelea kunyesha, vizuri wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kubwa juu ya maradhi hayo, kwa kuacha kutumia maji katika madimbwi au kwenye mabwa badala yake kutumia maji ya mfereji kwa shuhuli zao mbali mbali.

Alisema maradhi ya kichocho ni miongoni mwa maradhi yanayo uwa kidogo kidogo kwani, baktiri wa maradhi hayo anayojulikana kwa jina la Bilharzia(Schistosomiasis) hushi katika maji kwa muda mrefu na kusababisha madhara kwa wananchi.

“Katika kipindi hiki wananchi wanapaswa kujitahidi kujikinga na kujilinda, kuingia katika mabonde muda mrefu ili kuepuka maradhi hayo”alisema.

Alifahamisha kuwa kwa sasa hali iko nzuri tokea kutolewa dawa mwezi wa Agosti mwaka huu, hadi Novemba ni watu kumi tu ndio waliofika katika kitengo hicho mkoroshini kupatiwa dawa, kutokana na muda wa dawa zilipotolewa walikuwa hawapo majumbani kwao.

Aidha aliipongeza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi mbali mbali wanazozichukua, katika kukabiliana na maradhi hayo kwa jamii, baada ya kuondoka kwa wafadhili wao kutoka China kwa ajili ya Covid 19, kitengo kiliweza kuifikia miti ya maji 214 na mabwawa 141 Pemba.

Hata hivyo alisema jitihada zilizochukuliwa ni katika shehia ambazo maradhi hayo, waliweza kuwapima wananchi wakubwa na wadogo, kwa upande wa uwandani ilikuwa na asilimia 8.5 ya kichocho katika kipindi cha miaka mitatu kutoka 2017 hadi 2019 iliweza kupungua mpaka 0.5%.

Kwa upande wa Wingwi ilifikia hadi 0%, Mtangani imefikia 0.4% na kushuka hadi 0%, Kiuyu Minungwini ilifikia 1.4% na kushuka hadi chini ya asilimia moja.

Alifahamisha kwamba maradhi ya kichocho yanahitaji mashirikiano kutoka katika taasisi mbali mbali, ikiwemo Wizara ya Elimu, ZAWA, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Michezo kwa lengo la kushajihisha wananchi kujikinga na kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa huo.

Kwa upande wao wananchi wa Uwandani wamesema kuwa bado wanaendelea kuchukua juhudi kubwa katika kujikinga na maradhi ya kichocho, hususan katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Ali Omar Khamis alisema wamekuwa wakali katika kuwalinda na kuwakatadha watoto kuwenda kwenye mabwawa ya maji, huku akinamama wakishauriwa kuosha nguo zao na vyombo kwenye mifereji ya maji yaliyopo nje ya majumba yao.

“Tumewekewa mirefeji ili watu watumia maji ya bomba na sio maji ya kwenye mabawa, watu kupunguza kwenda au kuachana kabisa kutumia maji ya kwenye mabawa”alisema.

Mariyam Halfan Hamada wa Uwandani, alisema wananchi wameelimika kwa kiasi kikubwa katika kujilinda na maradhi ya kichocho, kwani wameacha kabisa kutumia maji kwenye mabwawa.