Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ
WAKULIMA wa Mwani kisiwani Pemba wameiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuingilia kati upatikanaji wa soko la zao hilo ili kuwanusuru na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo kutokana na wanunuzi kusitisha ununuaji zao hilo.
Hayo yamebainishwa na wanakikindi cha Muungano kilichopo Shehia ya Makangale Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba wakati wakizungumza na mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa alipowatembelea kukagua maendeleo ya kikudi hicho.
Haji Hamad Haji mmoja wa wanakikundi hicho amesema licha ya wananchi wengi Zanzibar kuhamasika kuzalisha kwa wingi zao hilo lakini kukosekana kwa soko inazidi kudumaza hali za wakulima hao bila kujua nini cha kufanya zaidi.
“Ukija vijijini watu tunateseka sana na zao hili, migongo imevunjika kwa kuzalisha mwani lakini manufaa hapana. Saizi tumevuna lakini tumebaki kuuweka ndani kutokana na hatuna wa kumuuzia,” alisema
Aidha alisema tatizo hilo linatokana na wananchi kukosa taaluma zaidi ya namna ya kusarifu mwani kwa matumizi mengine jambo ambalo linapelekea wakulima wengi kutegemea njia moja ya uuzaji bila kuwa na mbadala wake.
Alisema, “wakulima tunakumbana na shida hii kutokana na kwamba bado tunakosa taaluma ya kusarifu mwani. Kila siku tunaambiwa mwani unamatumizi mengi lakini sisi wakulima hatuijui taaluma hiyo na hivyo kupelekea kutegemea soko eneo moja kwa kampuni za mwani na matokeo yake ni haya wamesitisha kununua na mwani tumesalia nao majumbani.”
Kwa upande wake Time Ismail Ali mwenyekiti wa kikundi hicho, alisema tangu wanunuzi wasitishe kununua zao hilo ambalo kwa kiwango kikubwa linazalishwa na wanawake imepelekea familia nyingi kukumbwa na hali ngumu ya maisha.
“Kusema ukweli soko la mwani limetuathiri sana wakulima hapa Makangale hasa sisi wanawake kwani wanawake wengi hiki ndicho kilimo chetu na tulikuwa tukipata angalau pesa kidogo ya kujikimu na familia zetu lakini hali imekuwa tofauti tangu makampuni yasitishe kununua mwani. Tunavuna sana lakini upo ndani unaoza hatuna pa kupeleka,” alisema.
Aidha aliongeza kutokana na tatizo hilo imepelekea wakulima wengi kukata tamaa ya kuendelea na uzalishaji wake jambo ambalo linazidi kuhatarisha uchumi wa familia hizo.
“Angalia chumba hiki chote kimejaa mwani, tumevuna lakini umekuwa wa kutunza ndani kutokana na hakuna mteja wa kumuuzia,” alisema Time huku akionesha chumba ambacho amehifadhia mwani wake.
Kutokana na hilo aliiomba serikali kusaidia kumaliza tatizo hilo kwani hali kuendelea kuwa hivyo inahatarisha kutokea madhara zaidi kwa wananchi wanaotegemea zao hilo ikiwa ni pamoja na tatizo la njaa kwani wakulima wengi hutegemea kuuza mwani ili wapate pesa za kununulia chakula kwenye familia.
“Tunaiomba sana serikali kama ilivyofanya kwenye Karafuu basi ituangalie nasisi wakulima wa Mwani kwani hali ni mbaya kwa sasa.Tunatumia nguvu nyingi kuzalisha lakini ikifika wakati wa kuuza wateja hakuna kama ambavyo ilivyo sasa na hata mteja akipatikana bei yake bado ni ndogo sana kulingana na gharama za uzalishaji wake,”alisema.
Aliongeza, “bei ya mwani kwasasa ni shilingi 600 sasa embu jifikirie mkulima utauza kilo ngapi ili upate pesa za kutosha kununulia chakula cha familia?”
Kwa upande wake Khadija Masoud Ali alisema licha ya kukabiliana na changamoto hizo lakini pia ukosefu wa zana bora za kuwawezesha kuzalisha ni kikwazo kwao jambo ambalo linapelekea kukumbana na viumbe hatarishi wanaotishia usalama wao wawapo baharini.
“Sisi wakulima bado tunafanya kazi katika mazingira magumu sana kwani hatuna zana bora za kujilinda tunapokuwa baharini. Wakati mwingine tunang’atwa na wadudu hatarishi na kusababisha kukaa ndani miezi zaidi ya mitatu na wengine kupata ulemavu wa kudumu,” alisema mwanakikundi huyo.
Mapema mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa aliwataka wakulima hao kutokata tamaa na uzalishaji ili kujiendeleza kichumi licha ya changamoto zinazowakabili.
“Kikubwa tuendelee na uzalishaji tusirudi nyuma kwani ndiyo shughuli zetu. Nasisi wadau tutajitahidi kuwasilisha changamoto zenu sehemu husika ili angalau ziweze kutafutiwa ufumbuzi na kilimo hiki kiweze kuwa mkombozi kwa wakulima kama mazao mengine yanayolimwa hapa Zanzibar,” alisema Mkurugenzi.
Ziara ya Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa kisiwani Pemba ililenga kutembelea na kukagua maendeleo ya vikundi vya wanawake wajasiriamali vinavyowezeshwa na TAMWA ZNZ kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake Kiuchumi Zanzibar WEZA unatotekelezwa Zanzibar na TAMWA ZNZ kwa ufadhili wa taasisi ya Zanzibar Milele Foundation.