Tuesday, November 26

SIKU 100 za Rais Samia madarakani na Vijana.

NA ABDI SULEIMAN.

 

TANZANIA ni miongoni mwa nchi Duniani ambazo zimekua na idadi kubwa ya vijana, ikizingatiwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa lolote lile.

 

Kwa mujibu wa makadirio ya idadi ya watu Tanzania, kati ya mwaka 2013 hadi 2035 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeonyesha kuwa idadi ya vijana walio na umri wa miaka 15-35 mwaka 2019 ni asilimia 34.6 ya watu wote nchini na itaongezeka hadi kufikia asilimia 35.6 mwaka 2025.

 

Kwa sasa zaidi ya theluthi moja au mtu mmoja, kati ya watu watatu nchini ni kijana mwenye umri kati ya miaka 15 na 35, ikizingatiwa vijana ndiyo kundi lenye watu wengi nchini na huchangia kwa sehemu kubwa nguvu kazi ya Taifa, inayohitajika katika shughuli za uzalishaji mali ili kuboresha maisha na kukuza uchumi wa nchi.

Wakati Umoja wa Mataifa ukizindua ripoti yake ya kimataifa kuhusu vijana, imesema ushirikishwaji wa vijana bilioni 1.2 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 ni muhimu katika kufanikisha jamii endelevu, jumuishi na thabiti.

Kwa mujibu wa ripoti iliyoandaliwa na idara ya uchumi na masuala ya kijamii, DESA ya Umoja wa Mataifa, imesema vijana wanaweza kuchangia katika kuepusha hatari na changamoto zinazokabili utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa ajira, umasikini, ukosefu wa usawa wa kijnsia, mizozo na uhamaji.

Licha ya kwamba wana uwezo mkubwa bado wanakabiliwa na elimu duni, ambayo kiwango chake ni cha chini kuweza kuajiriwa katika viwango vinavyokubalika, huku Vijana milioni 71 hawana ajira na wengine wakiwa katika ajira zisizo na uhakika au zisizo rasmi.

Wakati hayo yakijiri jumla ya vijana 65,008 katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020, wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi ikiwemo mafunzo ya uanagenzi katika fani za ujenzi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, ufundi magari, ufundi bomba.

Ujuzi wengine ni utengenezaji wa vifaa vya aluminium, uchomeleaji na uungaji vyuma, kilimo na ufugaji, ushonaji, uchongaji vipuli, uchapaji nyaraka na TEHAMA.

Wakati akizungumza na Vijana wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani wakiwakilisha vijana nchini hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, aliwataka vijana nchini kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

Amesema baadhi ya miradi hiyo ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, kuwa ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa daraja la Magufuli (JPM Bridge) katika eneo la Kigongo–Busisi, ujenzi wa Bwawa la kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji, Reli ya kisasa yaani SGR na ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege.

Rais Samia amesema mbali na fursa hizo za miradi ya kimkakati, vijana hawana budi kutumia fursa zilizopo kwenye kilimo na mifugo, ambapo Tanzania ni ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika.

Hata hivyo aliwataka vijana kutumia fursa za uchumi mtandao, ambapo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha kwenye Mkongo wa Taifa na Kituo cha taifa cha kuhifadhi kumbukumbu (Data Centre).

Naye Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Juan Somaiva alisema vijana ni watu wanaoongoza maendeleo ya kiuchumi, karibu Vijana Milioni 73 walikuwa hawana ajira mwaka 2007, ambapo kitendo cha vijana kukosa ajira kinawasababisha vijana hao kujiingiza katika makundi maovu, kutokana na kukaa bure bila kuwa na shughuli ya kufanya na baadhi yao kujihusisha na uhalifu.

 

Hali hiyo inakuja licha ya jitihada za Serikali na wadau wengine mbalimbali wa maendeleo, kufungua fursa mbalimbali za ajira kwa vijana, jambo linaloonyesha bado kuna safari ndefu ya kutokomeza ukosefu wa ajira nchini, kutokana na kuongezeka kwa kasi kwa idadi ya vijana wanaoingia sokoni.

Vijana ni nguvu kazi inayohitajika zaidi, katika ujenzi wa uchumi ikizingatiwa kuwa Serikali imedhamiria kuifikisha Tanzania, katika uchumi wa kati ifikapo mwaka huo wa 2025.

Hata hivyo, hali ya mtaani bado siyo nzuri sana, kwa sababu vijana wengi wanaomaliza masomo yao katika ngazi mbalimbali hawana kazi, kutokana na kasi ya uzalishaji wa ajira kutoshabihiana na mahitaji ya ajira nchini.

Hii inamaanisha kwa kila watu 10 wenye uwezo wa kufanya kazi basi takriban mtu mmoja hana ajira nchini, Pia kufanya kazi kwenye sekta isiyo rasmi au kujiajiri kwa kufanya biashara imekuwa ni vigumu kutokana changamoto za kupata mitaji, nyenzo na mahali pa kufanyia kazi zao.

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 inaeleza kuwa kijana ana haki ya kupata kazi na ujira wa haki, ili kumudu maisha yake kwa sababu jamii inategemea kumuona akishiriki katika shughuli za maendeleo na kuanza kujitegemea kwa kiasi fulani.

Baadhi hujiingiza katika vitendo viovu kama vile wizi, ujambazi, uzururaji, uvutaji bangi, utumiaji wa madawa ya kulevya, umalaya n.k,” inaeleza sehemu ya sera hiyo.

Katika siku za hivi karibuni, Serikali imekuwa ikitumia miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), majengo ya Serikali jijini Dodoma kutengeneza ajira mpya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Takwimu Muhimu za Tanzania, jumla ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini mwaka 2017/18 kulikuwa ikilinganishwa na ajira 453,466 kwa mwaka 2016/17.

Kati ya ajira zilizozalishwa mwaka 2017/18, asilimia 75 zilikuwa ni ajira kutoka Serikalini, zikijumuisha ajira 18,000 kutoka Serikali Kuu na ajira 397,009 kutoka katika miradi ya maendeleo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Kwa upande wa sekta binafsi, mwaka 2017/18 ilizalisha ajira 137,054 sawa na asilimia 25 ya ajira zote zilizozalishwa. Hata hivyo, ajira zilizozalishwa na sekta hiyo inayotegemewa zaidi kutoa ajira ulimwenguni zilipungua kutoka ajira 239,017 zilizozalishwa mwaka 2016/17.

Vijana wametakiwa kuangalia fursa nyingine za kujiajiri na kuwa huru kufanya shughuli za ujasirimali ambazo zitawasaidia kuinuana kuliko kusubiri ajira za serikalini na sekta binafsi ambazo hazitoshelezi mahitaji yao ikizingatiwa kuwa idadi yao inaongezeka kila mwaka.

Katika kujiajiri, vijana wanaweza kutumia vipaji na ujuzi walivyonavyo kubaini na kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, Mfano wanaweza kutumia changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi kutoa suluhisho la uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.

Pia mashirika ya kijamii nayo yamekuwa yakianzisha programu mbalimbali za kuwaongezea ujuzi na maarifa vijana ili kujiajiri katika shughuli za ufundi na ujasiriamali kupunguza ukali wa maisha.

Nidhahiri kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano ya awamu ya sita, inayoongozwa na Rais Samia, imedhamiria kwa dhati kuwaondoshea vijana changamoto mbali mbali zilizokuwa zikiwakabili kwa kuwawekea mazingira mazuri.

Licha ya changamoto kubwa kwa vijana ni suala la ajira kwao, kutokana na mikakati mbali mbali iliyopo chini ya Rais mama Samia, vijana wamehakikishiwa kuondoshwa changamoto hiyo.

Nidhahiri na wazi sasa vijana kujipanga na kujiweka utayari katika suala zima la kupokea ajira hizo, ikiwa serikalini, taasisi binafsi au mashirika.

Hongera mama samia kutimiaza siku 100 madarakani.