Saturday, October 19

SOS yatumia Milioni 6,391,000/= kuwapatia wanafunzi chakula.

JUMLA ya shilingi Milioni 6,391,000/= zimetumiwa na SOS kwa ajili ya kununulia chakula, wanafunzi wanaokaa kambi katika skuli 10, ambazo wanafunzi wake wamo katika mpango wa kuimarisha familia unaosimamiwa na shirika hilo.

Skuli hizo ambazo zimenufaika na chakula hicho ni pamoja na Vitongoji Msingi na Sekondari, Tumbe Msingi na Sekondari, Ngwachani Msingi na Maendeleo Sekondari, Mjawiri Msingi na Mjawiri Sekondari na Michenzani Msingi na Sekondari.

Vyakula hivyo vilivyotolewa ni sukari kilo 150 zenye thamani ya shilingi 231,000/=, maharage kilo 600 yenye thamani ya shilingi 132,000/=, Mchele liko 2100 zenye thamani ya shilingi 294,000/=, sukari kilo 500 yenye thamani ya shilingi 830,000/=, Unga wa ngano kilo 500 wenye thamani ya shilingi 590,000/= na mafuta ya kula lita 200 yenye thamani ya shilingi 480000/=.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa chakula kwa skuli mbali mbali mratibu wa mradi wa kuimarisha familia kutoka shirika la SOS Pemba, Abdalla Omra Kidimu alisema lengo la kutoa msaada huo wa chakula ni kusaidia juhudi za serikali katika kuhakikisha jitihada za ufaulu zinaongezeka.

Alisema panapokosekana chakula mambo mbali mbali yanakosekana, hata utulivu wanafunzi wanakosa, hivyo SOS imeona bora kutoka msaada wa vyakula kwa wanafunzi wanaolala kambini kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao ili kufanya mitihani hayo kwa utulivu wa hali ya juu.

“SOS intake kuongeza ufaulu hii ni fursa kwetu wanafunzi kusoma kwa bidii, hii ni fursa pekee kwenu wanafuzi wafadhili wetu wanahitaji kuona mabadiliko makubwa”alifahamisha.

Aisha alizitaka kamati za skuli na walimu wakuu wa skuli hizo, kuhakikisha msada huo unatumiwa kwa wanafunzi walioko kambini, kwa lengo la kuinua sekta ya elimu kwani ndio sekta muhimu sana, huku vijana kuweza kuongeza uwelewa.

Kwa upande wake afisa elimu Wilaya ya Mkoani kutoka baraza la Mji Mkoani, Seifa Mohamed Seif alisema moja ya mikakati yao ni kunyanyua viwango vya ufaulu kwa wanafunzi maskulini.

Alisema SOS imekuwa mdau mkubwa kwa skuli zilizomo ndani ya wilaya ya Mkoani, zikiwa na lengo la kushajihisha mwamko wa elimu, sambamba na kuwataka wanafunzi kurudisha inhasani hiyo kwa kusoma kwa bidii na kufaulu kwa wingi.

“Bado muda upo wanafunzi kujikita katika masomo, licha ya mwaka huu kukubwa na matukio mengi na kufanya wanafunzi wasisome vizuri, ikiwemo kipindi cha COVID 19 na uchaguzi mkuu”alisema.

Nae mwanafunzi Omar Yussuf Ali alisema msaada huo kwao umekuja wakati muwafaka, kwani ili mwanafunzi aweze kufanya vizuri mitahani yake hapaswi kuwa na mawazo mbali mbali, ikiwemo kufikiria suala zima la chakula.

Aidha aliishukuru SOS kwa msaada wa chakula waliowapatia, kwani chakula hicho kitaweza kuwasaidia katika kuwafanya wasome kwa bidhii na kuonyesha mfano kwenye mitihani yao mwaka huu kwa kuongeza ufaulu.

Mariyam Iliyasa Shariff aliziomba taasisi nyengine kuongeza juhudi katika kusaidia sekta ya elimu, hususana kipindi hiki ambacho wanafunzi wamekaa makambini kujiandaa na mitihani.